Jukwaa la wapenzi wa mambo ya muziki wa Tanzania-

Breaking

Sunday, February 23, 2014

MAPENDEKEZO YA WASANII KATIKA RASIMU YA KATIBA MPYA. Utangulizi
Baada ya maagizo kutoka Tume ya Katiba ya kuwa kila kundi kutayarisha mapendekezo ya rasimu ya Katiba, wasanii nao chini ya mashirikisho yao manne Shirikisho la Filamu, Shirikisho la Muziki, Shirikisho la Sanaa za maonyesho na Shirikisho la Sanaa za ufundi  waliweza kuja na mapendekezo kadhaa ambayo waliyawasilisha katika Tume, kwa bahati mbaya hakuna kipengele chochote cha mapendekezo hayo kilicho ingizwa katika Rasimu ya Katiba. Kwa ushirikiano, Mashirikisho haya ya sanaa yameamua kufikisha mapendekezo yao moja kwa moja kwa Wabunge wa Bunge la Katiba ili kuwezesha vipengele hivyo kuweko katika Katiba yetu mpya.
 Mapendekezo
1.    Kutambuliwa kwa wasanii kama kundi maalumu katika Katiba.
Katika Rasimu ya Katika kuna makundi maalumu kadhaa ambayo yametajwa, kama vile wakulima, wavuvi, wafugaji, na kadhalika  na hivyo kutambuliwa kikatiba. Wasanii ni kundi kubwa katika jamii ya Kitanzania. Wasanii wapo karibu katika kila kaya Tanzania. Wafinyanzi, wasusi, wapambaji, wanamuziki waigizaji, mafundi mbalimbali wa ushonaji ujenzi na kadhalika, wako wengi wala hata wao hawajitambui kama ni wasnii kutokana na mazingira waliyomo. Katika ripoti mojawapo ya BASATA ya mwaka 2006, idadi ya wasanii nchini wakati huo ilikuwa ni milioni 6, ni wazi kuwa idadi hiyo kwa sasa itakuwa imepanda.  Katika miaka ya karibuni vijana wengi wamekuwa wanaongezeka kujiunga na kundi hili kwani katika sanaa kumekuwa na uwezekano wa kujipatia ajira, tena isiyokuwa na ukomo. Na hivyo sanaa kwa sasa si utamaduni peke yake bali ni sehemu muhimu ya uchumi wa Tanzania. Wasanii ni sehemu muhimu katika sekta ya Hakimiliki, takwimu za ripoti ya WIPO(World Intellectual Property Organisation) ya mwaka 2010, kuhusu mchango wa sekta ya hakimiliki katika uchumi wa Tanzania, inaonaonyesha  kuwa sekta hii, kati ya 2007-2010 ilichangia kati ya asilimia 3-4.6% ya gross domestic product(GDP). Na kiasi cha kati ya TSH 38.930 bilioni na 86.686 billion kilipatikana kama kipato cha walioajiriwa katika sekta hiyo. Kati ya watu 28, 202 na 44, 331 waliajiriwa rasmi, na hiyo ilikuwa kati ya asilimia 4.5 na 5.2% ya kundi zima la waajiriwa wa Taifa hili. Kwa kipimo cha GDP, sekta hii ilikuwa zaidi ya sekta ya madini, ambayo wote ni mashahidi imekuwa katika mazungumzo kila kona ya nchi. Na katika ajira sekta hii ilikuwa juu zaidi ya sekta nyingi zikiwemo madini, usafirishaji, mawasiliano, afya na ustawi wa jamii, maji, gesi, na hata ujenzi. Kwa mchango wa sekta hii wa 3.2% katika GDP kwa mwaka 2009 , umeweka sekta hii kuwa bora kuliko sekta za aina yake katika nchi  kama Croatia 3%, Singapore 2.9%, Latvia 2.9%, Lebanon 2.5%, Kenya 2.3%. Na katika mchango wa ajira sekta hii ilikuwa juu ya Romania, Bulgaria, Lebanon, Jamaica, Colombia, Kenya na Ukraine. Takwimu hizi hazijionyeshi katika takwimu za serikali kwa kuwa sanaa bado inaonekana ni utamaduni tu, na thamani yake katika uchumi haitiliwi uzito. Kutambuliwa kwa kundi hili kutawezesha kutungwa sheria na taratibu za kuwezesha Wasanii kuongeza ajira na mapato, na Taifa kufaidika na uchumi wa  raslimali hii.
2.     Kutajwa kwa  MilikiBunifu Intellectual Property ) katika Katiba.
Mali ziko za aina 3. Kuna mali zinazohamishika, mali zisizohamishika na mali zitokanazo na ubunifu. Aina mbili za kwanza zimetajwa katika katiba na ulinzi wake hujulikana na ni wa jadi. Lakini hii aina ya tatu ya mali huwa ni ngumu kuilinda kutokana na mfumo wake kuwa haushikiki hivyo sheria maalumu hutungwa kulinda aina hii ya mali (IP Laws). Mali zitokanazo na ubunifu kwa sasa ndio mali zenye kipa umbele duniani. Uvumbuzi wa teknolojia mbalimbali, ugunduzi wa njia mbalimbali za kuboresha maisha, sanaa na mengi yanayolindwa na milikibunifu, vimeweza kutoa ajira kubwa na kutoa mchango mkubwa wa kipato kwa wagunduzi na nchi ambazo wagunduzi hao wamekuwa wakiishi au kuzisajili kazi zao. Kama wasanii, haki zetu katika milikibunifu zinajulikana kama Hakimiliki, lakini kama Watanzania tunaona ni muhimu kulinda haki zote za Milikibunifu kwa maendeleo ya nchi yetu.
Nchi zote ambazo zimeweka taratibu imara za kulinda Milikibunifu duniani, zimewezesha wabunifu wake kubuni mambo ambayo yameweza kubadilisha maisha ya binadamu wengine duniani kote. Marikani iliweka kipengele cha Ulinzi wa hakimiliki katika katiba yake tangu mwaka  Agosti 1787, na kazi za wagunduzi wa Marekani tunaziona kila wakati katika kazi za sanaa na teknolojia. Korea kusini ilinakiri sehemu ya katiba ya Marekani kuhusu ulinzi wa Milikibunifu kuanzia mwaka 1948, kwa wakati huu wote ni mashahidi wa bidhaa kama Samsung, Ld Daewoo, Hyundai na kadhalika.
Milikibunifu pamoja na kulinda haki katika kazi za sanaa ambazo picha ndogo ya mapato yake zimetajwa hapo juu, Milikibunifu italinda haki za wabunifu wetu, tafiti za wasomi wetu, ugunduzi mbalimbali, taratibu mbalimbali za mambo yetu ya kiasili, dawa za asili za miti yetu, na taratibu za matumizi ya dawa hizo, na mali asili zetu nyingine nyingi tunazozifahamu na ambazo bado hatujazifahamu .
Kuna hasara nyingi ambazo hupatikana kama nchi haina ulinzi wa Milikibunifu, mifano michache hapa Tanzania, ni kupoteza kwa Milikibunifu ya jina Tanzanite, ambayo licha ya kuwa inachimbwa Tanzania tu lakini jina linamilikiwa na kampuni ya Afrika ya Kusini. Vazi la kikoi, pamoja kuwa ni la asili ya Tanzania, milikibunifu imesajiliwa Kenya, staili ya michoro maarufu ya Tingatinga milikibunifu yake iko Japan. Na haya ni machache ambayo yameshitukiwa Milikibunifu ikifuatiwa vizuri ndipo haswa ukubwa wa tatizo utakapojulikana. Kuna ulazima mkubwa wa kutaja Milikibunifu katika katiba na kuanisha ulazima wa kulinda kuendeleza na kwezesha wabunifu wan chi kwa manufaa ya kizazi hiki na vizazi vijavyo
No comments:

Adbox