YOUTUBE PLAYLIST

Tuesday, August 31, 2010

The Upanga Story


Upanga ni eneo muhimu sana katika historia ya muziki Tanzania. Hata katika miaka ya karibuni kulizuka kilichoitwa East Coast, muungano fulani wa wasanii wa Bongoflava toka maeneo ya Upanga, hii haikuwa mara ya kwanza kwa Upanga kuwa na wanamuziki waliotingisha mji. Enzi hizo za muziki wa soul, vijana wa Upanga walilipa eneo hili la mji jina la Soulville.Kwenye kona ya barabara ya Mindu na United Nations, nyumbani kwa familia ya Jengo, hapo ndipo palikuwa mahala pa mazoezi pa kundi lile la Groove Makers. Baadhi ya wanamuziki wa kundi hili walikuwa Mohamed Maharage, Joseph Jengo, Emmanuel Jengo, Herbert Lukindo, Willy Makame, na mpiga Drums ambae mpaka leo yupo katika anga za muziki Jeff. Kipindi hiki kilikuwa ni wakati wa muziki wa soul na kundi hili lilikuwa kundi la ubora wa juu wakati huo. Upanga ilikuwa na kundi jingine The Strokers, hili lilikuwa na awamu mbili, awamu ya kwanza ilikuwa na wanamuziki akina Donald Max, David Max, Harry Chopeta, Vincet Chopeta, Pino Makame na Ochiwa na Freddy Lukindo. Awamu ya pili ya kundi hili lilkuwa na Sajula Lukindo,Onesmo Kibira,Innocent Galinoma,Ben Galinoma, Denis Pad,Francis Kasambala,Vicent na Harry Chopeta, Ally Mwarabu, Sabri Mmanga na wengineo. Barlocks ni Bendi nyingine iliyochipukia Upanga, jina la Barlocks lilitokana na kuweko kwa kundi la Barkeys ambalo leo linaitwa Tanzanites. Barlocks walikuwa wakitumia vyombo vya Barkeys kwani kwa wakati huo bendi hizi zilikuwa kama mkubwa na mdogo. Barlocks hiyo ya awamu ya kwanza ilikuwa na wanamuziki akina Jimmy Jumba,Pimbi Sokoine, huyu alipewa jina la utani Pimbi kutokana na kuwa mrefu sana, Said Mbonde kaka yake Amina Mbonde mwanamuziki mwingine muimbaji,Sajula Lukindo, Abraham. Kulikuweko na makundi mengine mengi hapo Upanga, kama White Horse, Aquarius hapa walikuweko producer maarufu Hendrico Figueredo, Joe Ball,Joel De Souza, Mark De Souza,Roy Figueredo, Yustus Pereira,Mike De Souza. Baadhi ya wanamuziki wake walienda na kuungana na wengine Arusha na kuvuma sana na kundi la Crimson Rage, baadae wakarudi Dar na kujiita Strange. Baadhi ya kumbi walizokuwa wakipiga zilikuwa DI, Marine,Gymkhana,Maggot, St Joseph na kwenye shule mbalimbali.
(Picha ya juu-Emmanuel 'Emmy' Jengo, Joseph 'Joe' Jengo, Herbert 'Herby' Lukindo. Kati-Jeff 'Funky' nyuma yake ni Willy Makame. Picha ya chini Willy Makame)

Thursday, August 26, 2010

Marijani Rajabu

Marijani Rajabu kwa vyovyote ni mmoja wa wanamuziki ambao wametoa mchango mkubwa katika ulimwengu huu wa muziki. Japo ni miaka mingi toka mauti yake yalipomfika, bado nyimbo zake zinapigwa na wanamuziki mbalimbali majukwaani na hata kurudiwa kurekodiwa tena. Marijani alizaliwa maeneo ya Kariakoo mwaka 1954. Mama yake alikuwa mama wa nyumbani wakati baba yake alikuwa na shughuli za uchapishaji. Maisha yake ya utoto yalikuwa ya kawaida ila alikuwa kipenda sana uimbaji wa Tabu Ley na mwimbaji mmoja wa Guinea Sorry Kandia. Alilelewa vizuri kwa misingi ya dini ya Kiislam kwa hivyo alihudhuria mafunzo ya dini utotoni kama inavyotakiwa. Akiwa na umri wa miaka 18 hivi, alijiunga na STC Jazz, ikiwa chini ya mpiga gitaa maarufu wakati huo Raphael Sabuni, kabla ya hapo bendi hii ilikuwa unajulikana kama The Jets. Katika bendi hii Marijani aliweza kutoka nje ya Tanzania kwa mara ya kwanza ambapo alikwenda Nairobi na kurekodi nyimbo zilizotoka katika label ya Phillips. Mwaka 1972 Marijani alihamia bendi ya Safari Trippers. Hapa ndipo ubora wake ulifunguka haswa na kuweza kuinyanyua Safari Trippers kuwa moja ya bendi maarufu za wakati huo. Waliweza kutoa vibao vilivyopendwa mfululizo na kuweza kuzunguka nchi nzima. Vibao kama Rosa nenda shule, Georgina,Mkuki moyoni, viliweza kuuza zaidi ya nakala 10000 za santuri na hivyo kuwezesha bendi kuwa na vyombo vyake vizuri. Bendi wakati huo ikiwa na wanahisa wanne, ambao kwa bahati mbaya wakati bendi ndio iko juu, wakakosa kuelewana na ukawa ndio mwisho wa bendi hiyo. Miezi michache baadae Marijani na wenzie waliibukia Dar International. Pia huku kulikuwa na wanamuziki wazuri na haraka bendi ilipata umaarufu wa hali ya juu kwa vibao vyake kama Zuena na Mwanameka. kutokana na hali wakati huo bendi ilirekodi vibao hivi RTD na kuambulia sh 2500/- tu. Kilichosikitisha zaidi ni kuwa nyimbo zao tisa ziliuzwa kwa kampuni ya Polygram bila ridhaa yao. Kati ya mwaka 1979 na 1986 bendi ilipiga karibu kila wilaya nchi hii na kufurahisha sana watu na mtindo wao wa Super Bomboka. Uchakavu wa vyombo hatimae mwaka huo 1986, ukamaliza mbio za bendi hii. Kwa miezi michache Marijani akashiriki katika lile kundi kubwa la wanamuziki 57 waliotengeneza Tanzania All Stars, kundi hili lilirekodi vibao vinne ambavyo si rahisi kwa bendi zilizopo sasa kufikia ubora wake kimuziki. Marijani alipitia Mwenge Jazz kw muda mfupi, na kukaa kama mwaka mmoja Kurugenzi Jazz ya Arusha, kisha akajaribu kuanzisha kundi lake la Africulture na mtindo wa Mahepe lakini kwa ukosefu wa vyombo mambo hayakuwa mazuri. Kufiki1992 hali ya Marijani ilikuwa ngumu akiishi kwa kuuza kanda zake ili aweze kuishi.Pamoja na nyimbo nyingi, za kuimbia Chama tawala na serikali, na hata tungo yake Mwanameka kutumiwa katika mtihani wa kidato cha Nne. Rajabu Marijani hajawahi kukumbukwa rasmi kama mmoja wa wasanii bora Afrika ya Mashariki

Wednesday, August 25, 2010

Blog Mpya ya haki za wasanii Tanzania

Nimekuwa napewa changamoto kubwa kuhusu namna ya kusaidia wasanii wenzangu katika mapambano yao ya kupata haki kutokana na kazi zao mbalimbali walizorekodi au kushiriki. Hivyo basi nimeanzisha blog inayoitwa Wasanii wa Tanzania na Haki Zao ambapo patakuwa jukwaa la kutoa elimu kuhusu haki kama vile Hakimiliki, mikataba ya kazi mbalimbali, pia sehemu ya kupeana maoni na taarifa mbalimbali kuhusu biashara nataratibu nzima za shughuli za sanaa hapa nchini Tanzania. Nategemea wadau mtaweza kuchangia maoni na kuitangaza ili iwe kweli chombo muhimu kwa wasanii wa Tanzania

Saturday, August 21, 2010

Kinguti System


Ramadhan Maulid Kinguti maarufu kama Kinguti System ni mzaliwa Ujiji, Kigoma.
Bendi yake ya kwanza ilikuwa Super Kibissa ya Kigoma.
Super kibissa ni bendi iliyoanziswa 1968 na Kinguti akajiunga nayo mwaka 1977. Wakati huo kiongozi wa bendi alikuwa Mlolwa Mussa Mahango ambaye alikuwa ni binamu yake Kinguti. Bendi ilikuwa mali ya watu watatu, Gollo Saidi, Haruna Mahepe, n Maulidi. Kinguti alitunga nyimbo kadhaa katika bendi hii kwa mfano-Kazi ni uhai, Mapenzi tabu,na Zaina. Mwaka 1979 alichukuliwa na Ahmed Sululu ambae alikua katibu wa Dodoma International na kuhamia Dodoma, ililazimika Dodoma International wamchukue kujaza nafasi ya Shaaban Dede ambaye alikuwa kahama Dodoma International na kuhamia JUWATA. Katika bendi hiyo alikutana kwa mara ya kwanza na mpiga gitaa mahiri Kassim Rashid. Baada ya hapo alihamia Orchestra Makassy ambapo wakati huo walikuweko wanamuziki akina Marehemu Masiya Raddi ambaye alifariki kwa kukanyagwa na daladala, Doctor Remmy, Andy Swebe, Keppy Kiombile, John Kitime, Issa Nundu, Kyanga Songa, Choyo Godjero na wengineo, pia alikuweko Mzee Aimala Mbutu kwenye solo, na Kassim Mganga kwenye rhythm. 1986 alijiunga Afrisso ngoma chini ya Lovy Longomba, hapa alitunga nyimbo sita, Pesa ni maua, Amana mpenzi, Estah Usituchonganishe, waimbaji wakati huo walikuwa Kinguti, Lovy na Anania Ngoliga,kwenye solo alikuweko mzee Kassim Mponda, na rhythm Maneno Uvuruge, Kwa muda mfupi alikuwa DDC Mlimani Park, na hapa akatunga kile kibao maarufu Visa vya mwenye nyumba, ambapo aliimba na Hassan Bitchuka, Francis Lubua,Hussein Jumbe na Benno Villa. Mwaka 1989 alikuwa moja ya wanamuziki waanzilishi wa Bicco Sound, wakiwa na Mafumu Bilali, Asia Darwesh, Andy Swebe, Mzee Aimala Mbutu, walitikisa na vibao kama Muuza chips, Leyla, Magreth maggie, Kitambaa cha kichwa, Nyumba ya kifahari, na nyingine nyingi tu. 1999 alijiunga na kilimanjaro Connection, alikaa bendi hii na Kanku Kelly kwa miaka miwili kisha kuanzisha bendi na akina Hassan Shaw The Jambo Survivors ambayo yupo mpaka leo

Vijana Jazz enzi za Ngapulila




Kati ya awamu nyingi za Vijana Jazz Band moja iliyoleta changamoto na furaha ni ile awamu ya nyimbo , Ngapulila, Ogopa Tapeli, Adza. Pichani baadhi wa wanamuziki wa wakati huo. Picha ya kwanz a juu- Mzee Joseph Nyerere akiwa na Kulwa Milonge na Hamis Mnyupe, picha ya pili wapiga trumpet marehemu Chondoma, Hamis Mnyupe, na Kulwa Milonge. Picha ya chini ni kundi zima la Vijana Jazz wakiwa na Mheshmiwa Seif Khatib, hapa wanaonekana akina Shaaban Dogodogo, Hemed Maneti,Shaaban Wanted, Abou Semhando na wengine wengi.Kama unavyoona alama za x wengi hawapo tena nasi duniani.

Wednesday, August 18, 2010

Shaw Hassan Shaw


Kwa wapenzi wa Vijana Jazz wanakumbuka vile vipande vya keyboards vilivyokuwa vikianzisha zile nyimbo mbili alizokuwa akiimba Kida Waziri, Penzi Haligawanyiki na Shingo feni, mpigaji wake alikuwa Shaw Hassan Shaw Rwamboh. Mwanamuziki huyu alizaliwa

tarehe 25/sept/1959, Dar Es Salaam. Alianza kujifunza kupiga gitaa na wenzie kando ya Ziwa Tanganyika huko Kigoma, wakitumia magitaa ya tajiri mmoja aliyekuwa na meli ya uvuvi. Aliporudi Dar es Salaam akakutana na mwanamuziki Zahir Ally Zorro, Zahir ndiye aliyeboresha upigaji wake wa gitaa kiasi cha kukubaliwa na Patrick Balisidya kupiga gitaa la rythm katika bendi yake ya pili PAMA Band, chini ya Afro70.

Ni chini ya malezi ya Patrick alipojifunza kupiga Keybords (Kinanda). Baada ya hapo aliacha muziki na kujiunga na Dar Technical College. Lakini 1980 alijiunga na Vijana Jazz kama mpiga Keyboards, alishirikiana na wanamuziki wengi lakini wengi pia wametangulia mbele ya haki. Waliobaki kati ya aliyokuwa nao wakati huo ni John Kitime, Abuu Semhando, Kida Waziri, Saad Ally Mnara, Hamisi Mirambo, Hassan Dalali, Hamza Kalala na Rashid Pembe. Mwaka 1990 alijiunga na Orchestra Safari Sound, chini ya Maalim Muhidin Gurumo (MJOMBA), na Marehemu Abel Baltazar , hapa alikutana na wanamuziki kama Benno Villa Anthony na Mhina Panduka (Toto Tundu) .Aliacha bendi baada ya miezi sita tu, mwenyewe anasema, ‘….kutokana na muhusika kutozingatia mkataba wangu…’. Alihamia Zanzibar na kujiunga na bendi iliyokuwa ikipiga Mawimbini Hotel, hakukaa sana kwani Washirika Tanzania Stars walimwita. Hapa akakutana na Zahir Ally, Ally Choki Rwambow, Musemba wa Minyugu,Tofi Mvambe, Abdul Salvador na wengine, ilitokea kutoelewana baina ya wanamuziki na yeye kama kiongozi wa bendi ilibidi aachie ngazi kuepusha bendi kuzidi kujichanganya. Baada ya hapo Kanku Kelly ambaye ni mume wa dada wa mke wake alimuita ajiunge na Kilimanjaro Connection Band. Anasema Kanku alimvumilia sana kwa kuwa alikuwa hajawahi kufanya kazi ya kukopi nyimbo za wanamuziki wengine wakubwa duniani, pili hii bendi ilikua inazunguka kwa kupiga muziki hotel mbalimbali Malaysia,Singapore, Indonesia,Thailand na Japan jambo ambalo lilifanya aone kila kitu ni kigeni. Katika bendi hiyo alishirikiana na akina Kanku Kelly, Mafumu Bilal, Maneno Uvuruge, Burhan Adinan, Shomari Fabrice, Bob Sija, Fally Mbutu, Raysure boy,Delphin Mununga na Kinguti System. Baadaye Shaw, Kinguti na Burhan Muba waliamua kuanzisha kundi dogo wakitumia sequencer keyboards na kumuaga Kanku Kelly. Group hiyo ilijiita Jambo Survivors Band, itakumbukwa kwa ule wimbo Maprosoo uliokuwa katika album ya MAPROSOO. Baada ya hapo bendi ikaanza kuzunguka nchi mbalimbali ikipiga katika mahotelini. Wameshapita Oman , Fujairah, U.A.E, Singapore, Malaysia na sasa wapo Thailand. Shaw anasema wanamuziki ambao hatawasahau kwa kuwa wamemfikisha alipo ni Zahir Ally Zorro, Marehem Patrick Balisdya, Waziri Ally, Kinguti System, Burhan Muba na Kanku Kelly. Kituko ambacho hawezi kusahau ni nchini Malasyia akiwa na Kanku Kelly kwa mara ya kwanza kupiga muziki akiwa amezungukwa na watu weupe Anasema nyimbo zote zilipotea kichwani akawa hakumbuki hata nyimbo moja.

(Picha ya juu Burhan Muba, Kinguti System ,Hassan Shaw, ya chini ni Vijana Jazz, Hassan Shaw wa mwisho kulia)



Tuesday, August 3, 2010

Lister Elia














Huyu ni mwanamuziki mpiga keyboards, zao la Dodoma, kule alikotoka Patrick Balisdya, Anania Ngoliga, Rahma Shally na wengi wengine. Lister mtoto wa mchungaji atakumbukwa sana kwa kazi yake katika bendi ya Sambulumaa lakini baada ya hapo alipitia Afriso Ngoma ya Lovy Longomba na Orchestra Safari Sound wale vijana wa Kimara, na hatimae akatua MK Sound(Ngoma za Magorofani). Hiyo ilikuwa baada ya wanamuziki akina Andy Swebe, Mafumu Bilali, na Asia Darwesh kuhamia Bicco Sound, alitua huko wakati mmoja na Ally Makunguru, Rahma Shally na hivyo kujiunga na Joseph Mulenga , Makuka, Matei Joseph na wengineo. Lister pia ni mtunzi wa vitabu na mwanamuziki ambae amesoma vizuri muziki kwa sasa yuko Japan habari zake za sasa zinapatikana kwenye website yake http://www.listerelia.com/

(Pichani Sambulumaa katika picha kabla tu ya uzinduzi wa bendi hiyo, picha ya pili Lista akiwa OSS)

Sunday, August 1, 2010

Harison Siwale-Satchmo


Kwa mara ya kwanza niliwaona 'Live', Jamhuri Jazz Band wakipiga katika ukumbi wa Community Centre Iringa, ukumbi maarufu kwa wenyeji wakati huo kwa jina la Olofea senta (Welfare Centre). Ni vigumu kuelezea jinsi nilivyokuwa najisikia kwani nilikuwa sidhani kama kutakuja kuweko na wanamuziki wanapiga vizuri namna ile. Lakini katika wote mpiga rythm guitar Harison Siwale, aliyejulikana kwa jina la Satchmo, alikuwa na anabakia kuwa mpiga gitaa aliyenifurahisha kuliko wote. Kwanza alikuwa na staili ya peke yake, na mpaka leo nikisikiliza nyimbo zake kama vile Blandina, Mganga no 1, Maria bembeleza mwana au Ewe ndege, nabaki kusifia kuwa huyu bwana alikuwa na kipaji cha pekee. Kuna rafiki yangu aliwahi kumuuliza wakati ule huwa anapataje mawazo ya kupiga gitaa lake kwa staili ile? alijibu kuwa huwa anajaribu kupiga sauti za viumbe mbalimbali wa porini katika gitaa lake.
Wanamuziki waliokuwa katika bendi ya Mkwawa High School, watakumbuka jinsi walivyoweza kupata nafasi ya kupiga pamoja na bendi hii kila ilipokuja Iringa mjini, maana hizo ndiyo zilikuwa taratibu wakati huo. Bendi ikifika katika mji, kama mji ule una bendi basi nao watapata nafasi ya kushirikiana na wageni. Wakati huo Mkwawa ilikuwa na wanamuziki kama vile Sewando, Manji, Mpumilwa,Kakobe waliweza pia kubadili hata muziki wao kutokana na kupiga na bendi hizi zilizokuwa kubwa wakati huo. (Pichani toka kushoto- Harison Siwale, Mbaraka Mwinyshehe na Abdul Mketema)

Kuzaliwa kwa Bana OK


Baada ya kifo cha Franco, Lutumba Simaro ndie alie liongoza kundi zima la TPOK Jazz kwa miaka minne. Ilionekana kuwa ili warithi wa Franco waendelee kufaidi matunda ya kundi hilo, wazo lilitolewa kuwa Simaro abakie na wanamuziki wote na familia iendeshe utawala mwingine wote, na warithi wawe wanapata asilimia 40 ya mapato yote, ambapo dada yake Franco ambaye ndiye alikuwa kiongozi wa familia angeyasimamia shughuli hizo. Dada wa Franco, baada ya kushauriana na nduguze aliamua kuwa familia ipewe asilimia 30,na isijihusishe kabisa na mambo ya bendi. Baada ya makubaliano haya bendi ilianza kazi na safari yake ya nje ya kwanza ilikuwa Tanzania na Kenya. Hali ilikuwa ngumu baada ya kifo cha Franco, lakini mambo polepole yalianza kuwa mazuri. Ghafla magazeti yakaanza kuwa na barua za wasomaji zikimlaani Simaro kuwa anaendesha bendi kama mali yake peke yake na kutokutoa msaada wa maana kwa watoto wa Franco. Hatimae akaandikiwa barua rasmi kuwa arudishe vyombo vyote vya muziki nyumbani kwa Franco.Hiyo ilikuwa mwishoni mwa mwaka 1993. Wakati huo huo mwanasheria wa familia ya Luambo alienda kwenye TV na kutangaza kuwa Simaro si kiongozi tena wa bendi.

Ilikuwa ni pigo kwa Simaro ambaye alijiunga na OK Jazz tangu 1961, na kupitia kwake wanamuziki kama Femi Joss, Kwammy, Isaac Musekiwa, Defao, Albino Colombo waliweza kuwika katika OK Jazz, na wote walikuwa wameondoka akabaki mwenyewe na sasa alikuwa akifukuzwa kupitia TV.

Katika onyesho lake la mwisho aliwaomba watu wa TV ya RTNC kuhudhuria,na kwa kutumia nafasi hiyo nae akatangaza kuwa yeye si mwanamuziki wa TP OK Jazz tena, ilikuwa ni tangazo la kusikitisha lililoleta simanzi kwa wengi. Na ndio ukawa mwanzo wa Bana OK, wanamuziki walikutana walikutana katika ukumbi wa Bar ya Zenith na kuamua kuanzisha bendi chini ya Rais wa Lutumba Simaro. Ilikuwa tarehe 4 January 1994. (Habari na picha kutoka www.afropop.org kwa ruksa ya Banning Eyre)

Upinzani...........

Leo hii kuna neno maarufu limetokana kwa wasanii wa Kimarikani-BIF. Si kwamba ni utamaduni mgeni, ila utekelezaji wake ndo umekuwa tofauti siku hizi, na kwetu hapa kumekuweko na utamaduni wa ushindani ambao kwa kuchochewa mara nyingine na vyombo vya habari ukageuka upinzani. Katika kipindi fulani cha miaka ya sitini muziki wa jiji la Dar katika nyanja ya Band za rumba ulitawaliwa na bendi mbili, Dar es Salaam Jazz- Majini wa Bahari na mtindo wao wa Mundo, na upande wa pili Kilwa Jazz. Ulikuwa mpambano mkali uliofikia hata wapenzi wa bendi hizi mbili kutandikana makonde. Bendi zilitungiana nyimbo za mafumbo moja maarufu ulikuwa ule wimbo wa Dar Es Salaam Jazz Mali ya mwenzio siyo mali yako, ukiwadhihaki kilwa Jazz kutokana na eneo la Klabu yao kuwa na utata wa kodi. Morogoro kulikuwa na miamba wawili, Morogoro Jazz na Cuban Marimba, ushindani wao uliweza kuwasha moto wa upenzi Afrika ya Mashariki nzima, watu walikuwa wanajitahidi kuwepo Morogoro siku za wikiendi, Morogoro Jazz wakiwa na mtindo wao wa Sululu, Cuban Marimba na mtindo wa Ambianse. Nao pia walitunga nyimbo zenye vijembe nyingi zilizowatia kiwewe wapenzi wao, Cuban walikuja na mtindo wao Subisubi, wakijisifu kuwa wao ni Jini Subiani linanyonya. Tanga kulikuwepo na vijana wa Barabara ya 4 Atomic Jazz wana Kiweke , wakipambana na Jamhuri Jazz Band na mitindo yao mingi kama vile Dondola na Toyota. Ushindani huu uliendelea katika bendi mbalimbali, kama vile Juwata na Sikinde. Kuna ushindani mwingine ulikuwa zaidi wa kufikirika kama ilivyokuwa inadhaniwa na wengi kati ya Vijana Jazz na Washirika Stars, kiasi cha kwamba kuna wakati ule wimbo wa Nimekusamehe lakini sintokusahau ulitafsiriwa kuwa ulikuwa umetungwa na Hamza Kalala kwa ajili ya kumtaarifu Hemed Maneti, japokuwa si Maneti wala Hamza ambae niliongea nae kuhusu wimbo huo karibuni aliyesema kuwa aliutunga kwa ajili hiyo. Kwa wapenzi wa muziki enzi za uhai wa Maquis Du Zaire, na Orchestra Safari Sound wanakumbuka ushindani mkubwa ulio kuwepo kati ya hizi bendi mbili ambazo kuna wakati huo zote zilikuwa zikiwa na makao makuu jirani, Maquis wakiwa Ubungo na OSS Kimara. Maquis walipoasisi mtindo wao wa Ogelea piga mbizi, OSS wakaja na Chunusi, wakiwa na maana ukiogelea kiboko yako Chunusi. Katika mtiririko wote huu wa ushindani mara chache sana ulifikia wanamuziki binafsi wakashikana mashati kwa sababu za ushindani. Na ushindani ulikuwa wa maana kwa kuwa kweli bendi zilipiga muziki tofauti, Jamhuri na Atomic zote za Tanga lakini kila moja ilikuwa na muziki tofauti, na vivyo hivyo Moro Jazz na Cubano, au Tabora Jazz na Nyanyembe Jazz. Kila Jumanne asubuhi, Radio Tanzania ilikuwa na kipindi kilichorusha nyimbo zilizorekodiwa katika studio yake, Misakato. Ilikuwa si ajabu kukuta wanamuziki wa bendi yenye ushindani ukisikiliza nyimbo mpya za washindani wao. Na hata kutoa sifa pale ambapo zinastahili, na kutokea hapo watu wanajipanga kutengeza kazi bora kuliko hiyo. Nakumbuka Tancut Almasi ilikuwa Morogoro wakati Vijana Jazz wakirushwa nyimbo zao za Ngapulila, Adza kwa mara ya kwanza katika kipindi cha misakato, ilikuwa uhimu kusikiliza kazi yao kwani wakati huo Shaaban Wanted ndio alikuwa kahama Tancut na kujiunga na Vijana, na mfumo wa vyombo wa Vijana ulikuwa sawa na Tancut na Washirika pia yaani Solo gitaa, Rythm Gitaa, Second solo, Keyboards, bass, na vyombo vya upulizaji. Hii haikuleta upinzani bali iliongeza ushindani, hapo tulikaa chini na hata kurekibisha baadhi ya nyimbo tulizoziona ziko chini ya kiwango cha vijana, matokeo yake ndio ile album, yenye nyimbo kama Helena Mtoto wa Arusha, Masikitiko na kadhalika

SAFARI ZANGU NA BENDI sehemu ya kwanza.

  TANCUT ALMASI ORCHESTRA  wakiwa Jamhuri Stadium Dodoma   Sikumbuki ni safari ngapi za kimuziki nilizowahi kuzifanya hapa nchini katika m...