Monday, May 31, 2010

SABA SABA 2

Wanamuziki kadhaa wa zamani walikutana kuongela onyesho la wanamuziki wa zamani litakalofanyika siku ya Sabasaba. Mazoezi yataanza wiki ijayo. Pichani toka juu, Muhidin gurumo, Abdul Salvador, King Kiki na Rehani Bitchuka, Kabeya Badu na Ally Jamwaka, Jeff

Thursday, May 27, 2010

Mayaula Mayoni hatunae tena

Mayaula mayoni si jina geni kwa Watanzania. Pamoja na kuwa mwanamuziki mtunzi katika lile kundi maarufu la TP OK Jazz,chini ya Franco Luambo, Mayaula aliwahi kuwa mchezaji wa Young Africans. Mayaula alikuwa msomi mzuri wa Teknolojia ya Computer. Kwa miaka mingi karibuni alikuwa akaiishi Magomeni Mikumi Dar Es Salaam, huku akifanya kazi Ubalozi wa nchi yake hapa Tanzania.
Mayaula amefariki asubuhi ya tarehe 26 May 2010 huko Brussel Ubelgiji. Alikuwa na miaka 64. Mungu amlaze peponi pema. Sikiliza tungo yake hii akiwa na TP OK Jazz.

Wednesday, May 26, 2010

Shakaza Eddy Sheggy
Mara baada ya kutoa ule wimbo maarufu wa Kisambaa Shakaza, Eddy Sheggy mwenyewe na Wasambaa wengine wakaanza kuitwa Shakaza. Eddy Sheggy alikuwa mwimbaji mzuri na mtunzi mzuri sana. Kati ya bendi alizopitia ni Super Rainbow, Vijana Jazz, Bantu Group, Washirika Stars. Picha mbili za juu ni Eddy akifanya onyesho na Super Rainbow katika uwanja wa Mnazi Mmoja, chini ni wakati akiwa Vijana Jazz

SABA SABA


Ile siku ya kuvaa slimfit,jackson 5, raizon na muziki ulioendana na kipindi hicho inazidi kukaribia. Vikao vya matayarisho vinaendelea. Wanamuziki ambao watapanda jukwaani siku hiyo ni wale wa enzi zile na kupiga muziki wa enzi zao, tunategemea kusikia wakongwe hao wakiporomosha muziki kutoka sehemu mbalimbali za dunia. Pichani ni washiriki wa kikao kilichoendelea leo 26/5/2010. Waliohudhuria Waziri Ally,Ahmad Dimando, Juma Ubao,Crispin Stephan, Godfrey Mahimbo,Kanku Kelly, Jerry Tom, John Kitime.

Sunday, May 23, 2010

Patrick Pama Balisidya

Mwaka 1996 kwa ufadhili wa Ubalozi wa Netherlands lilifanyika tamasha kubwa la muziki Mnazi Moja, bendi kama Vijana Jazz, Polisi Jazz, Zaita Muzika, Maquis Original, Namtu Group, Shikamoo Jazz, zilishiriki. Hapa Patrick akishirikiana na Vijana Jazz, nyuma yake ni Fred Benjamin mwimbaji wa sauti ya kwanza Vijana Jazz, ambae naye ametangulia mbele ya haki. Siku hii alipiga wimbo wa Ni mashaka na hangaiko akishirikiana na Shikamoo Jazz

Thursday, May 20, 2010

Top Ten Show


1989/90 Radio Tanzania kwa ushirikiano na Umoja wa Vijana na CHAMUDATA waliweza kuendesha mashindano makubwa ya bendi yaliyoshirikisha karibu bendi zote Tanzania. Haijawahi kutokea project kubwa namna hiyo ya muziki na vigumu kuelewa kama itawezekana tena katika mazingira ya sasa. Pichani ni Vumbi na marehemu Mbwana Cocks katika picha iliyotoka gazeti la Uhuru wakiwa katika jukwaa Vijana Kinondoni. wakati huo Cocks alikuwa ndo ametoka Vijana Jazz na kuhamia Orchestra Maquis Original, akawa anapiga second solo, rythm akisindikizwa na William Masilenge, solo akiweko Vumbiiiiiiiiiiii

Choggy Sly

Nahisi najua Choggy Sly angesema nini angekuwa hai kama angejua nimeweka picha hii hapa, God he was a great guy. Pembeni yake ni mwanamuziki kutoka South Africa Vuli, aliyefanya mengi katika muziki nchini akiwa na dada yake Nini aliyekuwa akiimbia Afro70.Vuli baadae alikuwa akipiga trumpet katika kundi la Lucky Dube

Mabrothermen get together

Pamoja na yote vijana walipenda sana kuparty, kwa kila kisingizio ilitengenezwa party kulikuwa na party every week end. Unamtambua nani hapa? Kati ya hawa ni wachangiaji wakubwa wa blog hii pengine watakumbuka walikuwa wapi siku hiyo mabitozi hawa.Katika picha 'soul brother no 1' yumo. Na MJ nae ndani hahahahahaha those were the days. Wazee Maro mnamuona? Dimando huyo wa pili toka kushoto picha ya juu, mpaka leo hataki kunenepa anataka kuvaa slimfit bado.Angalia walivyovaa!!!!

Tunawakumbuka


Panjula na Kitonsa

Wednesday, May 19, 2010

Magwiji wa kweli

Hawa wanamuziki kama unavyowaona wanapiga saxophone , walikuwa na mengi zaidi wanafanana walikuwa pia wanaweza kupiga vizuri vyombo vingine, japo hawakuwahi kuwa bendi moja lakini wote waliwahi kuwa katika bendi zilizorekodi muziki ambao unapendwa mpaka leo ni akina nani na walipiga vyombo gani na walipitia bendi gani?

Simba wa Nyika

Tanga ni mji ambao umekuwa chimbuko la mambo mengi katika ulimwengu wa muziki. Hata muziki wa dansi uliingia nchini kupitia Tanga. Kilimo cha katani chini ya mpango wake wa SILABU (Sisal Labourers Beureau) iliwezesha watu kutoka sehemu mbalimbali kukutana Tanga kwa ajili ya ajira ya kukata mkonge, na hivyo mchanganyiko huo wa makabila ulileta uchangamfu wa kimuziki katika jiji la Tanga mapema sana kuliko miji mingine. Kati ya mazao ya Tanga ni bendi maarufu ya Simba wa Nyika ambayo wanamuziki wake walitoka Tanga na kuweka makao yao kwa muda Arusha wakiitwa Arusha Jazz na mtindo wao Wanyika. Vijana hawa walipohamia Kenya wakajiita Simba wa Nyika na waliwasha moto wa nyika kimuziki na nyimbo zao tamu. Hapa ni picha yao mojawapo.

Kitendawili tena

Naleta picha nyingine ya wanamuziki wa zamani, bahati mbaya kuna mmoja katika picha hii amekwisha tangulia mbele ya haki, wa kwanza kushoto ni Salim Willis, drummer, na baadae mpiga gitaa wa Afro70, wa kwanza kulia ni mwanamuziki wa toka enzi hizo na mpaka leo bado yuko jukwaani je unamfahamu ameshiriki katika miziki mingi inayopendwa sana. Unakumbuka bendi alizopitia?

Tuesday, May 18, 2010

Afro 70

Afro 70 wakati wako juu. Waimbaji Monte Gomes na Steven Balisdya (alikuwa pia anapiga drums), Dick Unga,Shabby Mbotoni(alikuwa pia anapiga saxophone na bass). Magitaa Patrick balisdya, Owen Liganga(second solo), Salim Willis(second solo), Jack Matte (rythm guitar),Charle Matonya(Bass guitar), Paul Mdasias (drums), Didi Musekeni(Hayuko pichani mwimbaji).

Taarab ya Tanga


Katika miaka ya 50 wanawake tisa wa Tanga walijikusanya na kuanzisha wakaanzisha kikundi cha kuimba walichokiita Raha til Fuad maana yake Raha ya Moyo. Akina mama hawa chini ya bibie aliyeitwa Mama Akida au aka Mama Lodi, waliendesha kikundi chao wakiwa wanaimba nyimbo za Siti Binti Sadi na tungo zao ambazo waliimba katika melody ya nyimbo za kihindi zilizotamba wakati huo. Kundi hili liliendelea na kuanza kuruhusu wanaume kujiunga hasa wakiwa wapiga vyombo. Hata mtoto wa Mama Akida, Akida Jumbe hatimaye alijiunga na kundi hili kama mpiga accordion kwenye mwaka 1962. Kundi hili ambalo baadae lilikuja kuitwa Young Noverty,liliendelea mpaka kukaweko na mgawanyiko uliozaa kundi la Shaabab Al Waatan. Hapa ndipo kukaanza mtindo wa kuweko kundi pinzani jambo ambalo kwa njia ya ajabu sana limekuwa linadumu kiasi cha miaka kumi kumi. Miaka ya 1960s Young Noverty na Shabaab al Waatan, 1970s Lucky Star Musical Club na Black Star Musical Club, 1980 Golden Star Taarab na White Star Taarab, 1990, Babloom Modern Taarab na Freedom Modern Taarab. Taarab ya Tanga ndo haswa inastahili kuitwa modern Taarab, kwani wao hawkufuata taarab ile iliyoletwa Zanzibar enzi ya Sultan Seyyid Barghash, kundi la taarab hii lilikuwa dogo na vyombo vyake vilikuwa pamoja na Gitaa la besi, gitaa la solo, drums bongos ,akodion au kinanda. Nyimbo zao zilikuwa fupi na si ndefu kama za Kizanzibari., nyimbo zilitegemea mipigo ya ngoma za asili za kumbwaya na chakacha na hata baadaye mitindo kama rumba,bossa nova ilitumika kama mapigo. Na Taarab ya Tanga ndio iliyoanzisha moto wa vikundi vya taarab Tanzania Bara. Moshi kulikuwa na New Alwatan,AzimioTaarab, na Blue Star Taarab , Arusha-Blue Star Taarab,Dodoma-Dodoma Stars,Kondoa –Blue Stars,Mbeya-Magereza Kiwira, Mwanza-ujamaa Taarab, Bukoba –Bukoba Stars, na muendelezo huu uliingia mpaka Burundi kutokana na mwana muziki mmoja alie julikana kama Athmani Mkongo, alitoka Burundi na bendi yake kufika Tanga akawa mwanamuziki mahiri wa Taarab na hata kuipeleka kwao Burundi.(Pichani Waziri Ally wa Kilimanjaro Band, wakati huo akiwa Lucky Star akipiga kinanda)

Monday, May 17, 2010

Orchestra Lombelombe

Niliahidi kuwa nitaweka kipande cha gazeti chenye habari ya Orchestra Lombelombe, bendi ambayo wanamuziki wake walitoka katika bendi ya Morogoro Jazz. Bendi hii ilikuja baadae kuitwa Kurugenzi Jazz baada ya kuwa chini ya Ukurugenzi wa Mkoa wa Arusha, pichani ni Gumbo ambae alikuwa mpiga Bass, miaka ya sabini alihamia Iringa ambako alikuwa mfanya biashara.

Friday, May 14, 2010

Lady JD na Gadna Habash

Lady JD na Gadna G. Habash hongera kwa kutimiza miaka mitano ya ndoa.
Lady JD ni mwanamuziki ambaye amekuwa akiongeza kiwango cha ufanisi kwa wanamuziki siku hadi siku, na kila nyuma ya mwanamuziki mwanamke aliyeolewa, na mwenye mafanikio lazma kuna mume anaeungana nae kwa kila hatua. Shukrani kwako Gadna, wanamuziki wazuri wa kike wengi wamepotea katika fani kutokana na waume zao kuwazuia kuendeleza kipaji. Tunawatakia miaka mingi mingine ya furaha

Tuesday, May 11, 2010

Nani hawa? Picha ilipigwa Dodoma 1961


Nimepigiwa simu leo na mzee mmoja akanambia amesikia kuhusu blog hii na ana kitu cha kuchangia. Kanipa picha hii ambayo pengine ni ya zamani kuliko nyingi humu ndani. Kanambia siku moja 1961 alitoroka shule ili aweze kumwona mwanamuziki ambaye alimpenda kuliko wote. Alikuwa anasoma Dodoma wakati huo, na aliweza kupata picha siku hiyo picha hii naiweka kwenu. Swali, nani anaweza kuwataja wanamuziki waliomo katika picha hii.? Wanaoimba hapo wote ni marehemu, anaepiga gitaa yu hai na picha yake ya sasa iko katika blog hii.

Zahir Ally Zorro


Muziki una mengi ya kushangaza, unaweza ukafika wakati ambapo mwanamuziki fulani kila akitoa nyimbo inatokea kupendwa. Hali hii inanikumbusha kipindi Zahir Ally Zorro alipokuwa JKT Kimulimuli Jazz , bendi iliyokuwa katika kambi ya Mafinga huko Iringa. Wakati huo ambapo JKT ilikuwa na makundi mawili ya askari kuna wale waliojitolea kwa ridhaa kujiunga na jeshi hilo na kulikuweko na wale waliolazimika kujiunga kwa mujibu wa sheria. JKT ilianzisha bendi mbili ambazo zote zilikuwa na muziki mkali. Dar es Salaam kulikuwa na JKT Kimbunga Stereo, jina lililotokana na staili yao ya Kimbunga, na Iringa kulikuwa na JKT Kimulimuli, hii ilitokana na kuwa na taa za steji zenye kuwakawaka. Bendi ya JKT Kimulimuli ilipata umaarufu sana baada ya mwanamuziki Zahir Ally Zorro kujiunga na bendi hii. Ilikuwa ni kama lazima usikie vibao vya bendi hii kila siku radioni. Kabwe..tungo kuhusu mtoto mtukutu alieanza uhuni toka mdogo na kulazimika kufungwa hata jela ya watoto. Kitu mapenzi kilianza zamani.....maneno ya kibao kingine kilichogusa sana hisia za watu, Tausi...wimbo unaohusu mwanamuziki aliyemtungia wimbo mpenzi wake. Ilikuwa kama vile kila kibao anachotunga Zahir kinakuwa hit.

Sunday, May 9, 2010

Mkongwe mwingine


Wengi tutakuwa tunamfahamu sana marehemu Ndala kasheba alieko kulia, je unamfahamu huyo anaesalimiana nae. Subiri usikie mchango wake katika muziki wa Tanzania

Saturday, May 8, 2010

Abdalla Gama


Kwa wapenzi wa DDC Mlimani Park, jina la Abdallah Gama ni jina muhimu katika historia ya bendi hiyo. Mwanamuziki huyu mpigaji wa gitaa la rythm alipata umaarufu zaidi baada ya wimbo wa uliotungwa na Assossa -Gama, ambao mpaka leo bado unafurahisha sana. Gama na wenzie kama Joseph Mulenga, Abel Balthazar, Cosmas Chidumule chini ya King Michael Enoch waliweza kutunga na kutengeza nyimbo ambazo bado zinaleta burudani miaka thelathini baada ya kutungwa. Abdallah Gama tena atakumbukwa kwa kazi zake alipokuwa BimaLee wakiwa na watunzi kama Jerry Nashon, Shaaban Dede, solo la Mulenga , nba besi la Mwanyiro, hapo ilikuwa utamu kolea. Pichani Gama(mbele)akiwa na mpiga gitaa mwingine Huruka Uvuruge ambae sasa yuko Msondo, na mpiga drum Matei Joseph ambae kwa sasa anendesha bendi yake African Minofu

Friday, May 7, 2010

Wanamuziki ndugu 3


Kitendawili kingine. Picha hii ilipigwa Seaview 1974, kuna wanamuziki wa Afro70, na wanamuziki ndugu ambao nao wametoa mchango mkubwa katika fani ya muziki, unawatambua ni akina nani hapo?

Monday, May 3, 2010

Wanamuziki ndugu


Katika kila nyakati kunatokea ndugu ambao ni wanamuziki. Pengine hii inatokea kwa kuwa mtu anakulia katika mazingira ya nduguze kupiga muziki hivyo inakuwa rahisi kwake kuwa mwanamuziki, na nduguze wakiwa wanamuziki inamrahisishia njia, lakini hilo si jibu sahihi kwa kweli kuna mengi zaidi ya hilo. Katika picha hii ni wanamuziki ambao ukoo wao wako wanamuziki wengi na hii imekuwa inaendelea kwa vizazi vitatu sasa jina la ukoo huu kila mara likiwemo katika historia ya muziki. Ni akina nani hawa?

Mitindo ya Bendi

Nikisema tuanze kutaja mitindo ya bendi ni mingi sana maana kila bendi imekuwa inakuja na mtindo wake. Majina mengine ya mitindo yana historia na maana na mengine yana kuwa yakutunga na kwa kweli hata waliokuwa wanayatumia hawana maelezo ya maana ya maneno hayo. Mundo,Msondo, sokomoko, dondola, kiweke, segere matata,super mnyanyuo, vangavanga, chikwalachikwala, libeneke na kadhalika ilikuwa mitindo ya bendi mbalimbali, na muziki wa bendi ulikuwa ndiyo unaonyesha utofauti huo. Kwa mfano katika mji wa Tanga ulikuwa na bendi kubwa mbili, Jamuhuri Jazz na Atomic Jazz. Jamhuri ilikuwa na mtindo wa Toyota, na baadae Dondola, hata muziki katika awamu hizi mbili katika bendi hiyohiyo ulikuwa tofauti. Atomic walikuwa na mtindo wa Kiweke. Muziki wao ulikuwa tofauti na ule wa Jamhuri. Na wapenzi wa Jamhuri hata wakizeeka husifu mtindo wa upigaji wa Jamhuri na rythm la Harrison Siwale(Satchmo). Kadhalika wapenzi wa Atomic watakwambia hakuna kama Kiweke, upigaji solo wa John Kijiko, bass la Mwanyiro na kadhalika. Mtu ambae kisha sikia muziki katika mtindo wa Ambianse wa Cuban Marimba, hawezi kuchanganya na Likembe wa Moro Jazz. Nimeanza kwanza kwa kutaja bendi zilizokuwa katika mji mmoja tena huko mikoani ambapo watu walikuwa wachache na wanamuziki wanajuana na kuishi jirani. Hali hiyo ndio iliyokuwa Tabora, ambako pamoja na Tabora Jazz, kulikuweko na Nyanyembe Jazz, Kiko Kids, muziki wa kila bendi ulikuwa tofauti na mwingine. Dar es salaam kulikuwa na bendi nyingi na hivyo mitindo mingi. Hakuna aliyeweza kuchanganya Maquis na OSS, wala Sikinde na msondo, Sokomoko, afrosa, Katakata vumbi nyuma ya Kyauri voice havikuwa na mpka wa kulinganishwa. Kikubwa ninachotaka kueleza ni kuwa bendi kuwa na mtindo ilikuwa si jina tu bali kulikuweko na kazi ilifanyika ili kupata kulinda na kuendeleza mtindo ambao bendi iliamua kuwa nao. Nakumbuka wakati wa mazoezi enzi hizo unaweza ukatunga wimbo ukianza kuimba wenzio watakwambia mbona unafanana na bendi fulani na hapo utakarabatiwa mpaka uwe katika mtindo wa bendi husika.

Mwanzo