Jukwaa la wapenzi wa mambo ya muziki wa Tanzania-

Breaking

Sunday, September 19, 2010

Western Jazz BandMzee Iddi Nhende ndiye aliyepata wazo la kuanzisha bendi maarufu ya Western Jazz. Iddi Nhende alianza muziki akiwa bado mdogo katika bendi ya shule alipokuwa Primary huko Nzega, mwaka 1944 alijiunga na Tabora Boys Secondary na hapa akajiunga na Brass Band ya shule ambapo alikuwa mpigaji wa Cornet. Alimaliza shule na kuja Dar es Salaam kujiunga na Chuo cha Afya, Sewa Haji Medical Training Center. Baada ya kumaliza mafunzo akaajiriwa Bohari ya madawa na kisha mwaka 1957 alihamishiwa Muhimbili. Upenzi wake wa muziki ulimfanya mwaka huohuo ajiunge na Rufiji Jazz Band kama mpiga trumpet, bendi hii wakati huo ilikuwa ikifanya maonyesho yake Minazini Community Centre iliyokuwa eneo linaloitwa siku hizi Mchikichini na pia walikuwa wakipiga muziki katika ukumbi wa Arnatougro.

Kutokana na miji kuwa ndio ilikuwa inaanza, watu wengi kutoka maeneo mbalimbali walihamia mijini na kujaribu kutafuta wenzao waliotoka sehemu moja na kuwa na vikundi vya kusaidiana au kuwaunganisha, watu wa sehemu mbalimbali walianzisha bendi wakazipa majina ya wanakotoka, hivyo waanzilishi wa Rufiji Jazz walitoka Rufiji, na ndivyo ilivyokuwa kwa Kilwa Jazz, Ulanga jazz na kadhalika. Hivyo Iddi Nhende aliyekuwa ametoka Nzega akaamua kuanzisha bendi ya watu kutoka Magharibi, kwa kuwa nchi ilikuwa imegawanywa katika majimbo, yakiweko majimbo kama Northern Province, Southern Highlands Province, Western Province na kwa vile Nhende alitoka Western province akaanzisha Western Jazz Band 1959. Akanunua vyombo aina ya Grampian toka duka la Souza Junior duka la vyombo vya muziki lililokuwepo mtaa wa Mkwepu. Aliweza kupata fedha baada ya kuuza ng’ombe kadhaa wa mamake. Wakati huo katika bendi za aina yake ni Dar es Salaam Jazz Band peke yake waliokuwa na magitaa ya umeme, hivyo Nhende akawa na kazi ya kuwatafuta wapigaji ambapo alimfuata mpiga gitaa la umeme wa kwanza Haus Dibonde(Msukuma), aliyekuwa anapigia Dar es Salaam Jazz Band(hii ilikuwa chini ya Mzee Muba), baada ya hapo akawapata wanamuziki wengine kutoka Ulanga Jazz Band, wakati huo chombo cha banjo kilikuwa muhimu hivyo akamtafuta mpiga banjo toka Cuban Marimba tawi la Dar es Salaam. Cuban Marimba wakati huo ilikuwa na tawi Dar Es Salaam lililokuwa chini ya Mzee Mwaipungu. Mwaka mmoja baadae alipata transfer ya kwenda Morogoro, hivyo huku nyuma alilazimika kuongeza wasanii ili kuimarisha bendi wakati hayupo. Akampata David Makwaya mwimbaji, na Ally Rashid(huyu ameacha muziki karibuni akiwa Msondo), mpiga Saxaphone toka Zanzibar. Bahati mbaya yule mpiga gitaa Haus akapata kichaa katika mazingira yaliyohusishwa na ushirikina kutokana na ushindani wa bendi uliokuwepo. Hivyo basi walifuatwa wanamuziki watatu toka Tabora Jazz, wanamuziki hao walikuwa wametoka pamoja katika bendi iliyokuwa na makazi Mwanza ikiitwa Kimbo Twist Band na wakahamia Tabora Jazz, na kutoka hapo wakachukuliwa na Western Jazz. Wanamuziki hao walikuwa

Rashid Hanzuruni, Kassim Mponda na Omary Kayanda. Baada ya kazi nzuri sana, Hanzuruni Nae akarukwa na akili katika mazingira yale ya yule mpiga solo wa kwanza akalazimika kurudishwa Tabora ambako alikaa mpaka mauti yake. Wema Abdallah akachukua nafasi ya mpiga solo katika bendi ya Western. Tatizo la kinidhamu lilifanya Wema aondolewe Western, na mpigaji mwingine mzuri sana Shamba Abbdallah akachukua nafasi, solo la huyu bwana linasikika kwenye nyimbo ka Rosa na kadhalika.

Hall la nyumbani la Western Jazz lilikuwa Alexander Hall, ambalo lilikuja kuwa hall la DDC Kariakoo. Western walinunua drums baada ya Kilwa Jazz kununua drums na kuzipitisha kwao kuwaringia. Walinunua toka kwa bendi moja ya Wagoa iliyoitwa De Mello Brothers. Western walirekodi santuri kadhaa chini ya mkataba waliyousaini na lebo ya Phillips ya Kenya. Hatimae Western na mtindo wao wa Saboso walitoweka katika anga za muziki miaka ya mwisho ya sabini. Kati ya nyimbo zao nyingi ni hizi hapa; Rosa, Vigelegele, Jela ya Mapenzi, Helena no 1 na 2.

19 comments:

Anonymous said...

John!
Uchangiaji wa hapa utawahusu watu makini wenye historia na kumbukumbu za ukweli sana, sii za kubabaisha. Mimi langu ni swali. Je huyu Omar Kayanda aliyetajwa humu ni yule mpuliza sax aliyepata kushiriki katika band mbali mbali?
Na kama ni yeye je yuko wapi kwa sasa?

Anonymous said...

Bwana Kitime nifahamishe ni nani alipiga solo katika Jela ya Mapenzi na Vigelegele. Hivi vibao si mchezo na si vigumu kuelewa ni kwanini akina Lokassa ya Mbongo na Dally Kimoko waliviiga.

kitime said...

Ndiye haswa, alianza kama mwimbaji na baadae kuwa mpuliza saxophone mahiri. Hatunae tena duniani miaka mingi

Anonymous said...

John!
Kutokuingia kwenye blog hii makini kwa siku moja tu, ninakuwa ninapitwa na mambo mengi na pia kukutana na watu wenye kumbukumbu zenye thamani na makini. Asante kwa up date ya kayanda. Mungu amrehemu.
Nilipata kukuuliza habari za mpuliza sax mwengine Kalamazoo nyembo. Sijui yuko wapi na ana endelea na muziki?
Hivi huko nyumbani wanamuziki kama wakina Hamza kalala huwa hawajajiunga ama kujua mambo ya blogs! kama kuna uwezekano tupostie mahojiano nao mara mojamoja. Asante

Anonymous said...

Hivi ni malipo kiasi gani walipatiwa wanamuziki ama waridhi wao katika kibao cha vigelegele ulio igwa na wakina lokasa ya mbongo?

kitime said...

Kalamazoo amepumzika kupiga muziki siku hizi yupo Magomeni, nitamtafuta atupe machache kwa ajili ya blog hii

Anonymous said...

Japo sii forum yake lakini vipi blog ya njenje ? tunahamu ya kujua mambo yanayoendelea ktk bendi yetu makini hapo TZ

kitime said...

Anon 00:00
Hawajapata hata senti tano. Tatizo ni kuwa wakati wanaenda kurekodi enzi hizo wasanii waliuza kabisa nyimbo zao mara nyingine hata kwa kupokea vyombo vipya vya muziki, na bendi nyingi zilitumia mtindo huu. Na pia kusambaratika kwa bendi na kutokuweko kwa mtu yoyote kufuatilia haki. Nilimuuliza Mzee Nhende kuhusu hili alinambia walijaribu kufuatilia wakakwama kwa kuwa hata zile kampuni walizoingia nazo mkataba hazipo, na kilikuwa kimepita kipindi kirefu bila mawasiliano. Karibuni CD ya nyimbo za western zitatoka najaribu kujua wamepata wapi haki za kutoa nyimbo hizo.

Anonymous said...

Day light robbery! nahisi kama wanataka kubeep waone wahusika wako makini kiasi gani. Je zinaweza kuwa na ubora ule ule? na kama ndio hudhani kama watu wa TBC ambao walikuwa RTD enzi hizo wanaweza kuwa na mkono wao hapo? maana huko nchi za watu na hivi makampuni yalisha kufa huenda ikawa shida kuzipata. Ni mawazo yangu tu

kitime said...

Hapana si daylight robbery, RTD hawahusiki listi ya nyimbo ni zile zilizorekodiwa Kenya.

Mlevi said...

Nyie mnaotaka Bendi za Tanzania ziwafuatilie hao wakongomani walioiga nyimbo zao, na wao wakiamua kufuatilia kuna atakaebaki hapa?

Bendi ngapi za kitanzania zimeiga nyimbo/mapigo ya nyimbo za Zaire?

Toka enzi za zamani tukianzia na "NAPENDA NIPATE LAU NAFASI?"

"...mokolo mosusu na makanisi,
nayebi lokola ngaa kozonga aa mamaaa,
Mokolo nakokufa..."

"...napenda nipate lau nafasi,
nipate kusemna nawe kidogo aa mama,
Mwenzio naumia..."

Kuna atakaebaki?

Anonymous said...

Mlevi! kweli waujua muziki na dhana yake!

kitime said...

Anachosema Mlevi kina ukweli mkubwa, hali ya kuchakachua nyimbo za Kikongo ilikithiri mpaka bendi zikaanza kutungiana nyimbo. Kuna bendi ilitunga wimbo wenye maneno yafuatayo, KOMA KOMA KOMA KAKA WEWE TUNGA ZAKO. Ilifikia mpaka waziri mmoja aliwaita wanamuziki na kufanya nao kikao kuwaambia waache kuchukua nyimbo za Kongo na kuweka maneno ya Kiswahili. Lakini katika kesi ya nyimbo za Vigelegele, Rosa wa kudaiwa ni kampuni iliyowaruhusu Soukus kuzipiga tena, lakini hili linategemea na mkataba uliokuweko kati ya Western Jazz na kampuni ya rekodi. Taarifa nilizonazo ni kuwa AIT ilinunua nyimbo hizo na kuna wanamuziki waliotia sahihi makubaliano hayo. Majina ninayo natafuta taarifa zaidi kwa walio hai.

Anonymous said...

Kama sikosei, Rashid Hanzuruni (RIP) alikuwa M-TZ wa kwanza kupiga Hawaian guitar katika wimbo uliorekodiwa "usione nikiandamana, ukadhani nafuata bendera, napenda sana nchi yangu, shika moyo utakueleza, twende haya twende, tufurahi tukiandamana..." Kama nimekosea lyrics naomba nisahihishwe wazee...

Anonymous said...

John!
Niko bukoba leo hii tarehe 25/9/2010 kwenye msafara wa kampeni za mgombea mwenza wa ccm. Band ya vijana jazz wapo hapa. Habari ya kusikitisha ni kwamba mmoja kati ya wanamuziki wake muimbaji wanamuita Mazabe wa kizunguzungu ambaye alipata kuwa na bend ya mchinga sound, amepata ugonjwa wa kiharusi ghafla leo asubuhi. Amelazwa katika hospitali ya mkoa hapa kagera. Jana alikuwa mzima na alifanya show. Mipango ya kumrudisha Dar inafanyika. Tumuombee mwenyezi mungu ampe nafuu na uponyaji wa haraka.
Mdau Hamis.

kitime said...

MUNGU AMSAIDIE

Anonymous said...

Mkuu,

Kila nikitaka kuiburudisha nafsi yangu moja ya kisuuza nafsi yangu ni kibao cha Roza cha Western Jazz Band wana Saboso. Mama watoto wangu huwa akinikuta nasilikiza Roza huwa anajua leo Mzee kafurahi.

Zamani nilikuwa na kanda yake. Baadye nikaja kukipata katika CD ya The Most Beautiful Songs Of Africa.

Kibao cha Roza hata kama nina mambo gani yanayoniudhi nikikisikia huwa nafarijika sana. Huwa kinanikumbusha Dar ya miaka ya mwanzoni mwa sabini. Hunikumbusha mitaa ya Ndovu na Twiga, Jangwani. Hunikumbusha marafiki zangu wanandugu watatu mabaharia maarufu sana waliotokea mitaa ya Jangwani. Mmoja wa wanandugu hao nilikutane naye mara ya mwisho asubuhi moja mwaka 1997 karibu na mitaa ya Odeon Cinema akanizoa mpaka Mtaa wa Lumumba karibu na makao Makuu ya CCM akanilazimisha kunywa naye bia asubuhi subuhi ambayo si tabia yangu lakini kwa sababu ya urafiki wetu wa miaka mingi tangu shule ilinibidi ninywe naye.

Halafu nikikisiliza kibao cha Vigeregere kinanikumbusha sana The Tanzanites Band na yule mwimbaji wa Kisouth Africa, Thami The Dynamite enzi za Simba Grill, Kilimanjaro Hotel. Thami alikuwa akiimba ile nyimbo vizuri sana na The Tanzanites walikuwa wanaipigia backup nzuri mno. Nilikutana na Thami mara ya mwisho mjini Adelaide, Australia mwaka 2004 kwenye tamasha la Fringes WOMADELAIDE nikamuimbia Vigeregere akanidaka juu kwa juu akaanza kuuimba.

Asante sana.
__________________________________


Mkuu,

Unasemaje kama utatoa fursa ya wachangiaji kutoa maoni yao ya nyimbo kumi bora za muziki wa dansi wa Tanzania of all time?

Unadhani Roza haitakuwemo?

Anonymous said...

LEO NILIKUWA NIMECHOKA NA MAMBO YA KAMPENI ZA UCHAGUZI KWA MICHUZI NIKATUPIA MACHO BLOG YAKO BAADA YA MUDA MREFU SANA.NIMEJIKUTA NIME STACK FOR TWO HOURS.KUNA WAKALI SI VIBAYA KUULIZA WAKO WAPI.SUDI SULTANI,YAHAYA BUHETI(WESTERN)JAMES MKUMBO(SUN BURST)BENNY PETY,VULLY END SAX NA MUSIBA ABDALA DAVID MUSA,MOHAMEDI KASIM YULE KWENYE WIMBO WA LILA UNANIACHA NITAKWENDA WAPI ALIE TIA YEEE NAKUFAEEE!(TRIPERS)MONTE(AFRO 70)USHABIKI WA ZAMANI BWANA MIMI NILIKUWA MTU WA SOKOMOKO PRINCESS BAR,SASA SIKU MOJA MPIGA BASS MAREHEMU CHRISTIAN KAZINDUKI ALIPATA AJALI YA PIKIPIKI PALE JACTION YA CENTROL POLICE NA RAILWAY STATION DANSI LIKWAPWAYA TUKAJIFANYA WATU WA UHAMIAJI KWENDA KUMU AREST JOSEPH MULENGA ALIKWANA TP SANTAFEE PALE MAGOROFANI GETAWAYS TUKALA NAE KONA MPAKA KWA SALEHE AKAKABIDHIWA MPINI NA MAMBO YA KAWA MSWANO.BIG UP JK HONGERA SANA,

Anonymous said...


Nd Kitine waziri aliyewapiga marufuku wanamuziki wa enzi hizo Tanzania wasiige nyimbo za Congo alikuwa ni waziri MGONJA. Na alifaulu kwa kiasi kikubwa

Adbox