YOUTUBE PLAYLIST

Thursday, September 9, 2010

Kassim Mponda

Kassim Mponda alikuwa mmoja ya wapiga gitaa mahiri hapa Tanzania. Kama unakumbuka wimbo utunzi wa Kakere, wa Sogea Karibu uliopigwa na JUWATA ambao pia ulipambwa na kinanda cha Waziri Ally aka Kissinger, basi lile ndio solo la Kassim Mponda. Kwa kifupi alianzia Nyanyembe Jazz, akahamia Tabora Jazz,na kupitia Police Jazz Band Wana Vangavanga, Safari Trippers ,mbapo alihama na wenzie na kuanzisha Dar International, kisha akahamia Msondo, akapitia Shikamoo Jazz, hatimae mwanae akamnunulia vyombo akanzisha bendi yake mwenyewe Afriswezi. Mpaka mauti yake mwezi June 2002. Wanaoikumbuka Police Jazz, imekuwa nayo ni Band ya miaka mingi ambayo wanamuziki wengi maarufu walipitia huko,ni muhimu kuja kuongelea bendi za majeshi na mchango wake katika muziki wa Tanzania.

22 comments:

  1. Anonymous01:15

    mwishoni mwa miaka ya tisini siyo huyu Mponda ambaye alipitia pia Mlimani Park, na kupiga solo katika wimbo wa kiu ya jibu?

    ReplyDelete
  2. Anonymous15:12

    Kassim Mponda au maarufu kama "De la Chance" alikuwa akipenda kuvaa kapelo na kukung'uta uzi (mpini) akifuata miserebuko ya mashabaki utadhani anawaona rohoni. Ukimkuta enzi zile Msondo wanapiga pale Kigongo Bar Buguruni ilikuwa si mchezo na pale ukumbi wa Manzese Argentina wakipelekwa na Landrover la mzee mmoja. Haki ya Mungu ardhi imemeza vingi. RIP De la Chance.

    Maselepa " Kama Zamani"

    ReplyDelete
  3. Anonymous09:25

    Kwa kukusahihisha Anony wa 15:15 Kassim Mponda alijiunga na Sikinde akitokea Msondo katikati ya miaka ya 80 kabla ya kwenda African Sound Orchestra (Afriso Ngoma). Kuondoka kwa Mponda Msondo ndiko kulikompatia Abdi Ridhiwani nafasi ya kuendeleza kipaji chake cha kupiga solo baada ya kuanza kama mpiga kinanda. Kuhusu aliyepiga solo katika wimbo wa Kiu ya Jibu nadhani alikuwa ni Michael Bilali (RIP). Kama nimekosea Balozi atanisahihisha.

    ReplyDelete
  4. Anonymous09:44

    Bwana Kitime machozi yananitoka. Nimekaa miaka yote hii nikijua Mponda yu hai kumbe katutoka tangu 2002, miaka minane iliyopita! Mponda alikuwa ni mchawi wa solo. Hili halina mjadala. Alionyesha kipaji chake cha hali ya juu katika vibao kama Ashibai, Sogea Karibu na vingine vingi. Nakumbuka nikiwa Nairobi mwanzoni mwa miaka ya 80, Lovy Longomba (RIP) alinieleza kuwa Mponda ni mmoja wa wapiga solo wa Kitanzania anaowaheshimu sana pamoja na kwamba alikuwa hajawahi kukutana nae. Hii ilikuwa ni sifa kubwa sana kwa Mponda kwani wakati huo Lovy alikuwa ni mwimbaji na mtunzi katika bendi ya Super Mazembe ambayo wakati huo mpiga solo wake alikuwa ni Bukalos Bukasa (RIP). Kwa maoni yangu, Bukalos ndiye aliyekuwa mcharaza solo anayeongoza miongozi mwa wapiga magitaa kutoka Congo walioweka makazi nchini Kenya. Nimeanza kutafuta nyimbo zote ambamo Mponda amepiga solo ikiwa ni kumuenzi mmoja kati ya wanamuziki hodari kuwahi kutokea nchini Tanzania.

    ReplyDelete
  5. Anonymous21:28

    Mponda alikuwa ni miongoni mwa wapiga solo hodari nchini Tanzania, lakini nyota yake ilianza kufifia alipoondoka Msondo na kujiunga na Sikinde kabla ya kwenda Bima Lee na hatimaye Afriso Ngoma. Kwa maoni yangu, ni Msondo tu ambapo Mponda aliweza kudhihirisha kipaji chake. Hii inadhirisha ukweli kwamba ili kipaji chako cha muziki kionekane inategemea timu unayofanya nayo kazi na mazingira.

    ReplyDelete
  6. Anonymous22:27

    John!
    Kwakuwa wewe ni mwanamuziki wa siku nyingi na ninaamini umeusoma muziki, je kwa kipinde kile ambacho teknologia ilikuwa bado sana ninaamini baadhi ya madoido kama ya sound effects yalikuwa adimu sana.Sasa nikisikiliza gitaa alilopiga marehemu Mponda linamirindimo fulani ya effects ambazo huenda ninaamini yaliwekwa kwa kiasi fulani na mafundi mitambo wazowefu kama wakina Chris Lugongo na wengine. Sasa! walipokuwa wanatwanga live je waliweza kutengeneza ladha hizo toka wapi? maana dunia ya leo imejaa madoido kibao. Kama njenje ukiangalia jukwaani mpaka mpiga tumba huenda akawa na katray ka tuvutu twa kukanyaga kanyanyaga wachulia mbali keppy na wewe kwenye solo. Inakuwaje ama ilikuwaje??

    ReplyDelete
  7. Bendi zilikuwa na effects nyingi tu, kati ya zilizokuwa za kawaida, ni Rpeater, echoo, reverb, tremolo,wah wah. Nadhani mzee Mponda alipiga solo kali katika nyimbo kadhaa Dar International na hata Safari Trippers, hebu sikiliza utunzi wake na solo katika nyimbo Salama

    ReplyDelete
  8. Mzee John Kitime, ahante kwa kuthibitisha kutoweka duniani kwa Mzee Kassim Mponda "De la Chance", ajabu ni kwamba miaka 8 sasa database yangu inasoma tofauti; I will update myself.

    Mzee Kitime pamoja na anonymous wali-comments juu ya topic hii ni kuwa Kassim Mponda (R.I.P) pia alipitia Sikinde (gita lake linasikika vizuri katika wimbo wa Dawa ya Pendo ni Pendo), pia alikwenda Bima (ambapo pamoja na kwamba kipindi hicho alikuwa soloist one, akipiga asilimia kubwa ya nyimbo, gita lake nalikumbuka katika wimbo wa busu pande tatu - Hii ilikuwa bima ya akina Maximilian Bushoke,Jerry Nashon "Dudumizi",)

    ReplyDelete
  9. Anonymous10:01

    Solo la Mponda katika wimbo 'Salama' linanikumbusha solo lililopigwa na Roxy Tshimpaka katika wimbo 'Belinda' wa Bana Ngenge, utunzi wake Fataki Lokassa (RIP). Mirindomo ya solo katika nyimbo hizi inashabihiana sana. RIP Kassim Mponda.

    ReplyDelete
  10. Anonymous14:15

    Asante mdau kwa kunisahihisha kuhusu Mponda, kwa kweli madhumuni yangu ilikuwa kusema mwisho wa miaka ya 80, lakini nikachemsha.Pili, namshukuru sana Kitime kwa kazi yake nzuri,kwani humuhumu tunajulishana mengi au kukumbushana nini hasa kilitokea kwa bendi na wanamuziki wetu wa kizazi cha zamani ambao hawakuchoka kutupa burudani za nguvu.

    ReplyDelete
  11. MCHANGO WA BENDI ZA MAJESHI - TANZANIA

    Mzee Kitime ulipokuwa tunamzungumia na kumjadili Kassim Mponda "De la Chance". Mwishoni mwa post ulichomeka sentensi "...ni muhimu kuja kuongelea bendi za majeshi na mchango wake katika muziki wa Tanzania".

    Nafikiri labda kwa kuanza ni vyema tukazijua hizo bendi ni zipi, mimi ninazozifahamu ni hizi, kama nimesahau nyingine wadau waongezee: -
    Mwenge Jazz Band - JWTZ Dar
    Kimulimuli Jazz Band - JKT Mafinga Iringa
    Police Jazz Band - Police Dar
    Ruvu Jazz Band - JKT Ruvu
    Magereza Jazz Band - Ukonga Dar

    Kisondella - from Mafinga (Iringa)

    ReplyDelete
  12. Anonymous17:15

    Anonymous wa 00:01 umenikumbusha mbali sana kwa kuzitaja nyimbo za Belinda ya Bana Ngenge na Salama ya Safari Trippers. Ni kweli kuwa solo limepigwa kwa ufundi wa hali ya juu katika vibao vyote viwili. Sikiliza Salama katika link http://www.youtube.com/watch?v=fZn2hRY8628 na Belinda katika http://www.youtube.com/watch?v=BdzQdF5tndg

    ReplyDelete
  13. Les Mwenge (Monduli), Tembo Jazz(Songea), Nyuki Jazz(Zanzibar), Uhamiaji(Dar es Salaam),Magereza (Musoma),Air Jazz(Dar es Salaam),JKT(Dar es Salaam),Mzinga Troupe

    ReplyDelete
  14. Anonymous22:48

    Tusisahau Polis jazz ya CCP moshi ambayo ambayo ilimtoa mwanamuziki mmoja wapo nguli hapa nchini mwenye uwezo mkubwa sana wa kutumia karibu vyombo vyote awapo jukwaani. Huyu ni Mgoro Mohamed Mgoro kijana wa majan mapana tanga. Alikuwa polis CCP na baadae akajiunga na JW. Kwa sasa natumaini anapigia AIR jazz kama hajastaafu na kazi zake za nje anafanya na bana mwambe. Huitwa FULL POWER anapocheza sax

    ReplyDelete
  15. Aksante kwa kumbukumbu hiyo, japo ni vizuri kufahamu kuwa historia ya kimuziki ya Mgoro ilianza kabla ya hapo. Yeye tayari alikuwepo enzi za Jamhuri Jazz.

    ReplyDelete
  16. Aksante kwa kumbukumbu hiyo, japo ni vizuri kufahamu kuwa historia ya kimuziki ya Mgoro ilianza kabla ya hapo. Yeye tayari alikuwepo enzi za Jamhuri Jazz.

    ReplyDelete
  17. Anonymous11:18

    Asante sana John
    kwakweli umenifungua akili. Mimi nilimfahamu mgoro wakati nikiwa pale CCP japo sikupata kujua alitokea wapi. Asante sana kwa kuni up date

    ReplyDelete
  18. Anonymous20:45

    Kitime picha ya hapo juu inamuonyesha Mohammed Shaweji na Maneno Uvuruge. Hivi Shaweji aliwahi kupigia Msondo? Nimeuliza kwa kuwa hii picha inaonyesha ilipigwa katika onyesho la Msondo. Naamini hivyo kwa kuwa nyuma ya Uvuruge kuna spika kenye stika ya JJB, yaani Juwata Jazz Band.

    ReplyDelete
  19. Shaweji hajawahi kupigia Msondo inawezekana picha hii ilipigwa alipowatembelea, nitajaribu kupeleleza hii picha ilikuwaje. Du aksante kwa uchunguzi makini, tunaweza kupata mengine mengi kutokana na picha hii

    ReplyDelete
  20. Mzee Kitime ndani ya blog yake hakitajificha kitu, nafikiri hii michango ya mawazo ya hapa na pale itaelelimisha wengi, imenichukua muda sana kuiona JJB ipo wapi; nilipoiona nimecheka saaaaana!. Ningefurahi sana iwapo wanamuziki wangekuwa sehemu ya hii jumuia wa wachangia au watoa maada ndani ya blog yako; vinginevyo naomba uonapoonana nao wape hamasa

    Kisondella

    ReplyDelete
  21. Anonymous20:21

    Kitime!
    Blog ya njenje itakuwa tayari lini? tungependa kufuatilia maendeleo ya bendi yetu makini huko nyumban

    ReplyDelete
  22. Anonymous15:23

    Naomba nitofautiane kiduchu na Anonymous 11:28. Mponda alifanya maajabu mengine alipokuwa "Sikinde". Unaikumbuka KONJESTA? Mwimbaji alikuwa Benno Villa Anthony.

    ReplyDelete

SAFARI ZANGU NA BENDI sehemu ya kwanza.

  TANCUT ALMASI ORCHESTRA  wakiwa Jamhuri Stadium Dodoma   Sikumbuki ni safari ngapi za kimuziki nilizowahi kuzifanya hapa nchini katika m...