Jukwaa la wapenzi wa mambo ya muziki wa Tanzania-

Breaking

Friday, August 20, 2010

Kinguti System


Ramadhan Maulid Kinguti maarufu kama Kinguti System ni mzaliwa Ujiji, Kigoma.
Bendi yake ya kwanza ilikuwa Super Kibissa ya Kigoma.
Super kibissa ni bendi iliyoanziswa 1968 na Kinguti akajiunga nayo mwaka 1977. Wakati huo kiongozi wa bendi alikuwa Mlolwa Mussa Mahango ambaye alikuwa ni binamu yake Kinguti. Bendi ilikuwa mali ya watu watatu, Gollo Saidi, Haruna Mahepe, n Maulidi. Kinguti alitunga nyimbo kadhaa katika bendi hii kwa mfano-Kazi ni uhai, Mapenzi tabu,na Zaina. Mwaka 1979 alichukuliwa na Ahmed Sululu ambae alikua katibu wa Dodoma International na kuhamia Dodoma, ililazimika Dodoma International wamchukue kujaza nafasi ya Shaaban Dede ambaye alikuwa kahama Dodoma International na kuhamia JUWATA. Katika bendi hiyo alikutana kwa mara ya kwanza na mpiga gitaa mahiri Kassim Rashid. Baada ya hapo alihamia Orchestra Makassy ambapo wakati huo walikuweko wanamuziki akina Marehemu Masiya Raddi ambaye alifariki kwa kukanyagwa na daladala, Doctor Remmy, Andy Swebe, Keppy Kiombile, John Kitime, Issa Nundu, Kyanga Songa, Choyo Godjero na wengineo, pia alikuweko Mzee Aimala Mbutu kwenye solo, na Kassim Mganga kwenye rhythm. 1986 alijiunga Afrisso ngoma chini ya Lovy Longomba, hapa alitunga nyimbo sita, Pesa ni maua, Amana mpenzi, Estah Usituchonganishe, waimbaji wakati huo walikuwa Kinguti, Lovy na Anania Ngoliga,kwenye solo alikuweko mzee Kassim Mponda, na rhythm Maneno Uvuruge, Kwa muda mfupi alikuwa DDC Mlimani Park, na hapa akatunga kile kibao maarufu Visa vya mwenye nyumba, ambapo aliimba na Hassan Bitchuka, Francis Lubua,Hussein Jumbe na Benno Villa. Mwaka 1989 alikuwa moja ya wanamuziki waanzilishi wa Bicco Sound, wakiwa na Mafumu Bilali, Asia Darwesh, Andy Swebe, Mzee Aimala Mbutu, walitikisa na vibao kama Muuza chips, Leyla, Magreth maggie, Kitambaa cha kichwa, Nyumba ya kifahari, na nyingine nyingi tu. 1999 alijiunga na kilimanjaro Connection, alikaa bendi hii na Kanku Kelly kwa miaka miwili kisha kuanzisha bendi na akina Hassan Shaw The Jambo Survivors ambayo yupo mpaka leo

13 comments:

Mzushi said...

Huyu ni Kaka yake NYOTA WAZIRI ALI?

Eti niulisikia naye anaitwa NYOTA KINGUTI

Anonymous said...

Katika picha Kinguti System alishirikiana katika uimbaji na Lovy Longomba na Bwami Fanfan

John Mwakitime said...

Ni nduguye,huyu ni Ramadhan Maulid Kinguti, na yule ni Nyota Abdallah Kinguti

emu-three said...

Wakongwe wa muziki, mimi napenda miziko yao tu, kwani ya kale ni dhahabu

Anonymous said...

Baada ya Kassim Mponda kuondoka Afriso Ngoma kijana mmoja machachari sana katika kucharaza solo alijiunga na bendi hiyo. Huyu si mwingine bali ni Madaraka Uledi aliyejulikana kwa jina la kimuziki 'Bongo Star'. Huyu alicharaza solo vilivyo katika wimbo 'Usinicheke' ambamo Lovy Longomba (RIP) aliongoza uimbaji. Kama sikosei wimbo huu ulirekodiwa RTD mwaka 1990 au 1991. Hivi Bongo Star yuko wapi na anafanya nini? Wadau wenye habari zake wanijulishe kupitia ukumbi huu. Vipaji kama hivi havitakiwi kupotea hivihivi.

Anonymous said...

Ninavyoelewa ni kwamba hiki kibao cha ‘Visa vya Wenye Nyumba’ alikitunga Kinguti alipokuwa Mlimani Park lakini alikirekodi na Bicco Stars muda mfupi baada ya kuihama Sikinde. Kibao hiki kiliteta mkanganyiko mkubwa miongoni mwa wapenzi wa muziki kwa kuwa wengi walikuwa hawaelewi kimetungwa na nani. RTD walichochea mkanganyiko huo kwa kupiga nyimbo zote mbili za Sikinde na Bicco Stars katika kipindi kimoja cha salamu na muziki au burudani.

Anonymous said...

Balozi, katika orodha yako ya wanamuziki wa Bicco Stars waliopiga pamoja na Kinguti umemsahau mtu mmoja muhimu sana, naye ni Fresh Jumbe. Ikumbukwe kuwa Bicco Stars ni bendi ya mwisho aliyopigia Fresh Jumbe nchini Tanzania kabla ya kuhamia Kenya na baadaye Japan.

Anonymous said...

Lovy Longomba ni miongoni mwa wanamuziki kadhaa mashuhuri kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo waliohamia Tanzania mwishoni mwa miaka ya 1980 wakitokea Kenya. Wengine ni watu kama Moni Mambo, Fataki Lokassa na Bibiley Kabakaba. Hata hivyo, Lovy alikuwa akisafiri sana kati ya Tanzania na Kenya, ambako nako alikuwa na makazi. Mkewe Zaina alikuwa ni Mkenya ambaye alizaa naye watoto watatu - Elly (RIP) na mapacha Christian na Lovy.

Anonymous said...

kwa sasa hivi kingutti sestym yupo nchini thailand akifanya shuhguli za muziki huko baada ya kumaliza mkataba nchini singapore kuhusu nyota waziri alikuwa ni dada wa kufikia tu ila sio ndugu. bali alitumia jina la kingutti kwa ajili ya umaarufu.

Anonymous said...

Mke wa Lovy Longomba,Mado Zaina ni Mkongo kutoka Bukavu sio Mkenya kwakuzaliwa pengine by makaratasi.

Anonymous said...

Nyongeza kwa mchango wa mdau hapo juu. Christian na Lovy hivi sasa ni wakiwa baada ya kufiwa na mama yao mzazi Mado Zaina Hulu aliyefariki dunia jijini Nairobi mwaka 2007. Mwaka 2005 walifiwa na dada yao Elly aliyefariki Yaounde nchini Cameroon. Kabla ya hapo, walimpoteza baba yao, Lovy Longomba, mwaka 1996 katika ajali ya gari nchini Tanzania.

mdau - Usa said...

Aksante sana Kitime kwa kazi nzuri unanikumbusha wakongwe .. mimi ni mpenzi wa muziki wa zamani na ninajua historia ya muziki huo

Msela said...

Kitime eti nasikia Waziri na Nyota WAMEMWAGANA eti ni kweli?

Adbox