YOUTUBE PLAYLIST

Sunday, August 1, 2010

Harison Siwale-Satchmo


Kwa mara ya kwanza niliwaona 'Live', Jamhuri Jazz Band wakipiga katika ukumbi wa Community Centre Iringa, ukumbi maarufu kwa wenyeji wakati huo kwa jina la Olofea senta (Welfare Centre). Ni vigumu kuelezea jinsi nilivyokuwa najisikia kwani nilikuwa sidhani kama kutakuja kuweko na wanamuziki wanapiga vizuri namna ile. Lakini katika wote mpiga rythm guitar Harison Siwale, aliyejulikana kwa jina la Satchmo, alikuwa na anabakia kuwa mpiga gitaa aliyenifurahisha kuliko wote. Kwanza alikuwa na staili ya peke yake, na mpaka leo nikisikiliza nyimbo zake kama vile Blandina, Mganga no 1, Maria bembeleza mwana au Ewe ndege, nabaki kusifia kuwa huyu bwana alikuwa na kipaji cha pekee. Kuna rafiki yangu aliwahi kumuuliza wakati ule huwa anapataje mawazo ya kupiga gitaa lake kwa staili ile? alijibu kuwa huwa anajaribu kupiga sauti za viumbe mbalimbali wa porini katika gitaa lake.
Wanamuziki waliokuwa katika bendi ya Mkwawa High School, watakumbuka jinsi walivyoweza kupata nafasi ya kupiga pamoja na bendi hii kila ilipokuja Iringa mjini, maana hizo ndiyo zilikuwa taratibu wakati huo. Bendi ikifika katika mji, kama mji ule una bendi basi nao watapata nafasi ya kushirikiana na wageni. Wakati huo Mkwawa ilikuwa na wanamuziki kama vile Sewando, Manji, Mpumilwa,Kakobe waliweza pia kubadili hata muziki wao kutokana na kupiga na bendi hizi zilizokuwa kubwa wakati huo. (Pichani toka kushoto- Harison Siwale, Mbaraka Mwinyshehe na Abdul Mketema)

7 comments:

  1. Anonymous11:35

    Kumbe Huyu ndie aliyepiga ile rythm......John nilipokwa mdogo naukumbuka sana huu wimbo wa mganga kwa sababu ulikuwa ukigwa na RTD kila jioni kufungua na kufunga kipindi cha kusoma salama, kile kipindi kiliitwa 'Jioni njema'

    Waambie wanamuziki wako wa kizazi kipya wana kazi nzito ya kuacha vitu vya kukumbukwa siku zote kama hivi.

    -Muarubaini

    ReplyDelete
  2. Anonymous17:37

    Nakumbuka miaka ya 70 na 80 nilipokuwa nikiishi Kenya, Wakenya walikuwa hawasiti kuitaja Tanzania kama nchi ya pili kwa muziki barani Afrika baada ya Congo. Hii haishangazi kwani miaka hiyo wanamuziki wa Tanzania walikuwa wakitamba kwelikweli katika stesheni ya redio ya VOK (siku hizi KBC). Nakumbuka muziki wa Tanzania ulikuwa ukipigwa mfululizo kiasi kwamba msomaji mmoja aliandika barua ya malalamiko katika gazeti la 'Daily Nation' yenye kichwa cha habari 'Dar music is overplayed' (muziki wa Tanzania unapigwa kupita kiasi). Nakumbuka hiyo ilikuwa ni 1981. Miaka hiyo ilikuwa ni 'Golden Age' ya muziki wa Tanzania. Kila nikisikiliza muziki wetu wa enzi hizo ndipo ninapogundua kwa wanamuziki wetu wa miaka ya nyuma walikuwa na vipaji vikubwa mno ambavyo ni nadra sana kuonekana miaka hii.

    ReplyDelete
  3. Anonymous17:50

    Kitime,

    Huyo Kakobe ndiyo Askofu sasa?

    ReplyDelete
  4. Anonymous17:57

    Napendekeza TBC Taifa iwe na kipindi cha salamu kila siku ambacho kitakuwa kikipiga muziki wa Tanzania wa miaka ya 60,70 na 80. Salamu zitumwe kwa ujumbe mfupi wa simu kuepuka watu kuropoka ovyo katika simu. Napendekeza kipindi hicho kianze saa 12 jioni hadi saa 1 jioni. TBC ina hazina kubwa sana ya muziki wa Tanzania ambayo haifikiwi na kituo kingine chochote cha redio, si tu nchini Tanzania, bali dunia nzima. Kipindi hiki kitatupa faraja kubwa wale tunaouenzi muziki wa kweli wa Tanzania na kuweka hai kumbukumbu ya muziki huo.

    ReplyDelete
  5. Anonymous18:23

    Namuunga mkono mdau hapo juu aliyependekeza kuanzishwa kwa kipindi cha salamu chenye muziki unaoweza kuitwa muziki, sio makelele. Kuna nyimbo nyingi sana ambazo mara ya mwisho nilizisikia Redio Tanzania miaka ya 80. Kwa mfano, ningependa sana kusikia tena wimbo wa 'Chukulubu' uliopigwa na CTU Orchestra Les Mwenge katikati ya miaka ya 80. Sauti za akina Ahmed Manyema na lile solo la nyuzi 12 katika kibao hicho si mchezo. Balozi fikisha ujumbe huu kwa Masoud Masoud wa TBC.

    ReplyDelete
  6. Anonymous19:22

    Kwa maoni yangu, Harrison Siwale ndiye aliyekuwa mchawi wa rhythm Afrika Mashariki na Kati enzi zake. Ikumbukwe kuwa Siwale alitamba miaka ambayo watu kama Vata Mombassa, Lele Nsundi na Lokassa ya Mbongo wa Congo walikuwa bado wanajifunza kupiga chombo hicho.

    ReplyDelete

SAFARI ZANGU NA BENDI sehemu ya kwanza.

  TANCUT ALMASI ORCHESTRA  wakiwa Jamhuri Stadium Dodoma   Sikumbuki ni safari ngapi za kimuziki nilizowahi kuzifanya hapa nchini katika m...