YOUTUBE PLAYLIST

Saturday, July 31, 2010

Mbaraka Mwinyshehe Mwaluka 1



Ukikaa na kusikiliza muziki wa Mbaraka kwa makini unajifunza mengi sana, kwa mashahiri ya nyimbo hizo unapata picha ya maisha yalikuwaje enzi hizo. Furaha, machungu, vicheko, vilio na kadhalika. Upigaji wake wa gitaa, ni somo zuri sana kwa mpigaji anaetaka kujiendeleza katika upigaji wa solo. Katika vipindi vyake vya kuanzia Morogoro Jazz hadi Super Volcano alipitia staili nyingi za muziki, baadhi kama Sululu, Likembe, Masika Zolezole na kadhalika. Tofauti na bendi nyingi ambazo hubadili majina ya mitindo bila kubadili muziki wenyewe, staili za Mbaraka zilionyesha mabadiliko. Nyimbo katika staili ya Likembe zilikuwa tofauti na zile za Masika Zolezole. Kipindi hicho wapenzi wa muziki waliweza kuondoka Dar es Salaam na kwenda Morogoro kufaidi wiki endi ya muziki aidha wa Cuban Marimba, au Morogoro Jazz. Picha ya juu Mbaraka Mwinyshehe, ya chini toka kushoto Sulpis Bonzo, Mlinzi Mustafa(huyu baadae alipigia Urafiki Jazz), Shaaban Nyamwela, Abdul Mketema (mwenye Saxaphone),Samson Gumbo,Mbaraka Mwinyshehe.Hapa wakiwa Morogoro Jazz Band

9 comments:

  1. Anonymous15:05

    Mashemeji wangaapi ....mimi nimechokaaa...mama mdogo ananitesa sana sanaana njoo unichukueeee.....ondooka Kleruu kalale pema kiongoooziii wetu shujaa..Sululuuu....ulipokuja mjini mimi nimekuona huwezi kunitishaa...hakuna kitu kibaya saana hapa duniani kama shidaaa....ohh shidaaa@

    Bravo kaka Mwakitime ulikuwa wapi kutuletea uhondo huu, unanikumbusha mbali sana nipo Kihesa wakati huo oh RIP Mbaraka!

    Maselepa
    "Mnazi wa zamani"
    Kimara Suka

    ReplyDelete
  2. Anonymous18:05

    Huyu alikuwa ni musical genius. Namkumbuka pia Mbaraka alikuwa mtu mcheshi. Tunamwomba Mola amweke mahali pema peponi. Amin.

    ReplyDelete
  3. Oh mzee wa Likembe huyu Mbaraka. Likembe na Sululu ilikuwa si mchezo. Nakumbuka Mbaraka alitoa wimbo mmoja wa lugha ya kilingala sijui unaukumbuka Mzee Kitime au kama kuna anayejua kwa nini aliutoa kilingala nitafurahi, huwa nikiusikilza nafurahi sana maana Mbaraka alikamua kilingala ile mbaya utasikia akichombeza kilingala kama vile 'kende malamu" nk

    Bana
    Minessota, USA

    ReplyDelete
  4. Wimbo ambao naufahamu Mbaraka aliingiza maneno ya Kilingala ni ule wimbo ambao uliotungwa kumuaga mwanamuziki wa Morogoro Jazz aliyekuwa na asili ya Kongo aliyeitwa Koko Bilo.....Kweli kwaheri rafiki yangu mpenzi unapoenda Zaire wasalimie....... na ndipo akaongeza maneno ya Kilingala mwisho. Mbaraka alifanya hivyo hata ule wimbo wa Expo 70, baada ya kushiriki maonyesho Japan alitunga wimbo na mwisho akawa na maneno ya Kijapani , kama vile Sayonara Japan, na kuna wimbo aliimba m'aneno ya Kiingereza 'Because of love.

    ReplyDelete
  5. Anonymous21:49

    Ni Jambo la kusikitisha sana kwamba Orchestra Volcano ilikufa pale Mbaraka alipofariki dunia katika ajali ya gari nchini Kenya mwaka 1979. Mpiga rhythm wa bendi hiyo Charles Ray Kasembe aliunda bendi iliyojulikana kama Orchestra Les Volcano iliyokuwa na makao yake jijini Nairobi na ambayo aliiongoza hadi mwishoni mwa miaka ya themanini kabla hajaamua kurejea nyumbani ambako alijiunga na kundi la sanaa la Muungano lililokuwa likiongozwa na Nobert Chenga. Hii inanikumbusha TP OK Jazz ambayo pia ilikufa miaka michache baada ya Luambo Luanzo Makiadi kufariki dunia. Tunachojifunza hapa ni kuwa Mbaraka na Luambo walikuwa ni mihimili mikubwa ya bendi zao, na mapengo yao hayakuweza kuzibika walipofariki.

    ReplyDelete
  6. Anonymous22:17

    Nilikuwa ninasoma Nairobi mwanzoni mwa miaka ya 80 na nilipata kuhudhuria maonyesho kadhaa ya Ochestra Les Volcano iliyoundwa baada ya kifo cha Mbaraka. Charles Ray Kasembe, ambaye alikuwa akiimba na kupiga solo kama alivyokuwa Mbaraka kiasi cha kujiita ‘Soloist National Junior’, alijitahidi kadri ya uwezo wake kufuata nyayo ya gwiji huyo aliyetangulia mbele ya haki. Kasembe, ambaye alikuwa ni mpiga rhythm wa Mbaraka, na wanamuziki wachache wa Orchestra Super Volcano walibaki Kenya kujaribu bahati yao baada ya wenzao kurejea Tanzania kufuatia kifo cha Mbaraka. Hata hivyo, viatu vya Mbaraka vilikuwa ni vikubwa mno kwa Kasembe, ambaye naye ameshafariki dunia. Pamoja na hayo, Kasembe alitoa vibao kadhaa vya kuvutia ambavyo kwa bahati mbaya sijawahi kuvisikia vikipigwa na stesheni zetu za redio za Tanzania. Hii na changamoto kwa stesheni kama TBC kutafuta nyimbo za wanamuziki wa Tanzania waliokuwa wakifanya shughuli zao nje ya nchi miaka ya nyuma ili kizazi cha sasa kiweze kuwa na kumbukumbu.

    ReplyDelete
  7. Shukrani sana mzee Mwakitime kwa ufafanuzi mzuri. Kitu kingine ambacho leo kimepotea ni bendi kuwa na vituo mikoani. Utaona Mbaraka alijikita Moro, Shem Karenga Tabora,Tuncut Iringa lakini leo kila bendi inakimbilia Dar. Ninajaribu ku-imagine watu walikuwa wakitoka Dar weekend kwenda Morogoro kuhudhuria show za Moro Jazz. Leo hii ni jambo adimu sana

    ReplyDelete
  8. Ni kweli hali inaonekana hivyo lakini pia kuna bendi nyingi mikoani, tatizo ni vyombo vya habari ambavyo vimejikita kutoa taarifa na kupiga muziki wa bendi za Dar es salaam tu. Zamani redio RTD ilikuwa haina ubaguzi wa aina hiyo, na ndio maana Mitonga Jazz kutoka Lindi iliweza kutikisa anga kwaa nyimbo zake kama Mariana, kama vile ambavyo Les Mwenge ya Arusha iliweza kutuletea kibao cha Kila Munu Ave na kwao au Tancut ya Iringa, zamani zaid Mara Jazz, Arusha Jazz, Super Kibisa ya Kigoma nk. Ziko bendi nyingi mikoani na zina vitu ambavyo ni tofauti na muziki wa Dar lakini havipati nafasi katika media. Moja ni kuwa kuna uvivu fulani wa utafiti na ubunifu katika media, hivyo kuishia kufanana hata sura za magazeti na vipindi, pili ni swala la rushwa hivyo unaeweza kumwona DJ ndo nyimbo zako zinapigwa, tatu ni radio za mikoani kuwa zinakopi mpaka uongeaji wa watangazaji wa radio za Dar hivyo kutokuwa msaada wowote kwa wasanii wa miji yao. Changamoto nyingine hiyo kwa media

    ReplyDelete
  9. Anonymous10:46

    Naziomba radio stations za Tanzania zitafuke nyimbo za Marehemu nyota Mbaraka (RIP) na wazipige hewani ili watu wengi zaidi waburudike na kipaji chake na wa-appreciate sauti nzuri, uimbaji wa kuvutia, umahiri wa upigaji ala, umakini wa kupanga nyimbo, mashairi mwanana, ubunifu na "sheer talent" yake. Tunamwomba Muumba amlaze Mbaraka Mwinshehe mahali pema peopni. Amin. CHE.

    ReplyDelete

SAFARI ZANGU NA BENDI sehemu ya kwanza.

  TANCUT ALMASI ORCHESTRA  wakiwa Jamhuri Stadium Dodoma   Sikumbuki ni safari ngapi za kimuziki nilizowahi kuzifanya hapa nchini katika m...