YOUTUBE PLAYLIST

Friday, July 16, 2010

Gitaa la rythm




Katika mfumo wa awali bendi zilikuwa zikitumia magitaa matatu, Solo, rythm na Bass. Gitaa la solo lilikuwa na sauti ya juu huku rythm ikiwa na sauti nzito kidogo ya kati, na mwisho Bass likiwa na sauti nzito kuliko magitaa mengine. Kimuundo gitaa la rythm na la solo hakuna tofauti. Yote yana nyuzi 6,lakini katika kutyuni kwenye amplifier, gitaa la rythm hunyimwa treble kiasi na kuongeza bass zaidi kuliko gitaa la solo ambalo huwa na treble zaidi ya magitaa mengine. Inasemekana kaka yake Dr Nico, ndie aliyeanzisha mtindo wa kuongeza gitaa la nne lililoitwa second solo. Hili lilikuwa likipigwa kwa mifumo mbalimbali katika bendi mbali mbali. Bendi nyingine zilitumia second solo kama gitaa lililokuwa linajibizana na solo, na bendi nyingine lilikuwa linajibizana na rythm. Bendi ya Cuban Marimba chini ya Juma Kilaza liliongeza ubunifu na kuongeza gitaa la 5 na kuliita chord guitar. Lakini leo tuzungumzie gitaa la rythm. Chombo hiki bado kinapigwa katika bendi nyingi lakini umaaarufu wake umeshuka sana. Katika kipindi cha miaka ya 60 na 70, gitaa hili lilikuwa na umuhimu mkubwa na wapigaji wake waliweza kubuni staili zao wenyewe. Kati ya wapiga rythm maarufu namkumbuka Satchmo, hilo ndio lilikuwa jina la kisanii la Harrison Siwale mpiga rythm wa Jamhuri Jazz. Yeye alikuwa na staili peke yake ya kupiga rythm, sikumbuki kusikia mtu mwingine akipiga rythm ya aina yake kabla ya hapo. Rythm yake ilitawala nyimbo za Jamhuri wakati huo. Kumbuka wimbo kama Mganga no 1 na 2, au Blandina. Marehemu Mzee Kasim Kaluwona nae alikuwa na staili tofauti ya upigaji uliyoifanya Tabora Jazz kuwa na staili yake peke yake, kumbuka gitaa lake katika wimbo Asha, au Dada Lemmy. Charles Kazembe akiwa na Morogoro Jazz anakumbukwa katika upigaji wa rythm kwenye nyimbo kama Wajomba Wamechacha. Hao ni wachache tu kulikoweko na wengi marufu. Katika kipindi hiki huko Zaire kulikuwa na mipigo mbalimbali ya gitaa la rythm, ila kitu kipya kikaanzishwa ambapo katika ufungaji wa nyuzi ,wapiga rythm wakauondoa uzi namba nne na kuweka uzi namba moja, hivyo kukawa na nyuzi namba moja 2 katika gitaa, hapo ndipo akina Vata Mombasa wakaweza kuleta utamu mpya katika upigaji wa rythm. Wakati huo Orchestra Kiam wakawa wanajivunia kupiga rythm kwa spidi kali sana,vibao kama Kamiki, Bomoto ni ushahidi wa kazi hizo. Utamu wa ufungaji wa nyuzi kwa staili hii uliweza kusikika vizuri katika gitaa lililopigwa mwanzo kabisa wa wimbo Andoya. Leo vionjo vya upigaji huo vinarudi kwa njia ya ajabu sana. Vikundi vya taarab vimeanza 'kuachia rythm' gitaa moja kubaki linapiga peke yake, japo wao hupiga gitaa la solo lakini staili ni ile ya enzi. Siku hizi kelele huwa nyingi kiasi unaweza ukatembelea bendi 3 ukaona mtu anapiga gitaa la rythm lakini husikii anapiga nini.

12 comments:

  1. Anonymous12:08

    Tatizo mkuu Mwakitime ni kutotaka kujifunza. Hawa vijana wa leo (narudia mimi nina miaka 32 nastahili kujiita kijana pia) hawapendi kufundwa. Wapigavyo solo na rythm, kila mtu anataka kusikika zaidi ya mwenzie. Ndio maana miziki kama ya akina Twanga Pepeta ni kelele tupu. Tena wanapotumia na keyboard ndio balaa maana vyote vinawekwa sauti ya juu bila mpangilio mwisho wake ni kelele mtindo mmoja.

    BAdo ninasema ukisikiliza music arrangement kwenye nyimbo kama "Kadiri Kansimba" unajifunza mengi. Nyimbo za namna hii zilipigwa kwa ufundi kiasi ambacho hata kama rythm imetumiwa kama second solo, bado kila chombo kinasikika. Yaani hakukuwa na gita linalovuma kufunika wengine.

    Mzee Mwakitime usisahau pia kurudi kwenye matumizi za sauti za watu. Zamani sauti ziliimbwa kwa mpangilio kiasi kwamba hata walipokuwa wakiimba watu wawili kama Marijani alivyowai kuimba na Fresh Jumbe kwenye Dar International Band au hata huu wimbo wa "Kadiri Kansimba" kuna sauti mbili tu lakini zinatoka kwa ustadi kana kwamba ni wengi na zimepangiliwa. Leo akina Twanga Pepeta wanakuwa na sauti kama 5 kwenye kiitikio na wote wanaume kwa wanawake wanaimba sauti ya kwanza. Hata sie tuliojifunzia muziki makanisani tunaona kabisa kuna walakini katika uimbaji wao. Huko kwenye bongo fleva sifiki kabisa manake wale wanaongea badala ya kuimba halafu bado wanajiita wanamuziki. Utajiitaje mwanamuziki kwa kuongea?

    ReplyDelete
  2. Perez18:55

    Mkuu Kitime yaani mimi hapa umenikumbusha RYTHM liliopigwa kwenye wimbo wa "Photo Album" wa kina Zahir Ali Zoro.

    We acha tu.

    Hivi ni nani amepiga rythm kwenye wimbo ule?

    ReplyDelete
  3. Anonymous00:43

    Nakubaliana na mchangiaji wa kwanza: vijana "wanamuziki" wa leo hawataki kufunzwa. Pia naongeza kuwa hawataki kujifunza!!! Lakini mimi naona hali hii TZ imeenea katika fani na nyanja zote. Utamaduni wa sasa TZ ni wa kutafuta "shortcuts". Mimi naona yale mapenzi ya kazi (labour of love) yamepungua sana. Anyway, tuendelee kuelimishana. TM.

    ReplyDelete
  4. Shukrani saana Uncle kwa elimu hii. Nakumbuka swali la Second solo na Rythim guitar na sasa nimeelewa vema.
    Asante kwa ELIMU hii na naamini utaendelea kutuelimisha mengine mengi.
    Je, ipo siku utaweza kuzungumzia familia ya UVURUGE?
    Hii (kwa kizazi kama changu kama kilianza kusikiliza na kufuatilia miziki ya dansi, Klabu Raha Leo Show nk) watakuwa wamewasikia saana kwenye kuungurumisha gitaa la rythim. Na pia wengine waliofana kwenye tasnia hii ya muziki wa dansi nchini

    ReplyDelete
  5. Anonymous18:29

    Kweli balozi Kitime. Ile sanaa ya ucharazaji wa rhythm imekufa si tu hapa Tanzania ambapo tulikuwa na wakali kama Harisson Siwale, Abdallah Gama ‘String Master’, ‘Profesa’ Omari Shabani na wengine wengi, bali hata DRC ambako miaka ya nyuma kulikuwa na miamba wa chombo hicho kama Vata Mombassa (Lipua Lipua) na Lele Nsundi (Kiam). Wapiga rhythm tuliokuwa nao sasa wapo wapo tu ili mradi kukamilisha idadi ya wanamuziki katika kundi. Inasikitisha.

    ReplyDelete
  6. Anonymous13:11

    Unakumbuka rythm ya mokolo nakuokufa? Rythm hiyo - ukichanganya na sauti ya mwimbaji - ndiyo iliyoipa "sura" wimbo huo.

    ReplyDelete
  7. Tatizo ni hilo alilosema mdau mmoja. Kila mpigaji ala anataka asikike,na tatizo linaanzia katika upangaji mzima wa vyombo. Bendi kama Msondo inajitahidi sana ukisikiliza muziki wake vyombo vinaachiana. Sikiliza wimbo kama Mwana Mkiwa, utaona solo la Pangamawe na Rythim ya Zahoro Bangwe ilivyotulia. Hapo hapo utasikia tumba zikihanikiza kwa nafasi yake.Au wimbo wa Transfer, lakini bendi nyingine ni solo na besi tu tabu tupu.

    ReplyDelete
  8. Hivi sasa mpigaji rythim amebaki mmoja, Zahor Bangwe ambaye ameanza toka album ya "Kitoto chaanza tambaa" akiwa na bwana mkubwa King Kikii. Bangwe ni hazina iliyobaki ingawaje haonekani kujulikana ujuzi wake utakuta anafananishwa na Uvuruge Huruka. Mimi huwa namfananisha na Kazidona wa Kanda Bongo Man ambaye alikuwa akimfukuzia Lokasa kule DRC.

    ReplyDelete
  9. Anonymous00:31

    Bwana John Mwakitime nakupomgeza kwa kuanzisha blog ambayo inaelimisha,kutukumbusha na kutumbuiza.Napenda kutoa maoni na kusahihi hasa kuhusu Marehemu Charles Kazembe alipigia Super Volcano na sio Morogoro Jazz baada ya kutoka T.K Limpopo ambayo Juma Kilaza alianzisha.Napenda kuongeza wapigaji wa Rythm ambao ukienda Youtube utasikia na kuona Umahiri wao Alfred Chivaro,Samson Kazingoma,Issa Bendera na Gerald Nangati Wote wa Morogoro Jazz,Charles Kazembe Super Volcano na Senyagwa Cuban Marimba Band.

    ReplyDelete
  10. Anonymous00:50

    jamani naomba msikilize nyimbo ya sikinde iitwayo nalala kwa taabu. Ule mpangilio wa vyombo si wa kawaida,yaani kwa wakati mmoja unaweza kuburudika na rythm,bass,drums,solo na ile midomo ya bata ambayo inaingia kwa utaalamu wa pekee.Hakuna chombo ambacho kipo juu zaidi ya vingine bila sababu.Wadau sikilizeni kibao hicho, mtakubaliana na mimi.Kazi nzuri John Kitime.

    ReplyDelete
  11. Anonymous01:50

    Mdau nimekupata hiyo nyimbo naifahamu ila sikuwahi kuitegea sikio mpaka niliposoma comment yako,sijuwi nimeirudia mara ngapi? ile ilikuwa ni kama dream team!!! uimbaji,bitchuka,gurumo,chidumule solo..Mulenga, Abel ..bass Mwanyiro,..rythm,kama sikosei Muharami,...midomo ya bata,..Enoch,Lendi, aaah we acha.

    ReplyDelete
  12. NYAWANGE NYANGIRA18:13

    Asanteni sana wadau wa blog hii. Naomba sana aliye na wimbo orijino wa bendi ya jamhuri uitwao simba mwituni. Wimbo huo una sauti halisi ya mnyama simba. Napenda sana sauti hiyo. Namba yangu: 0753121903

    ReplyDelete

SAFARI ZANGU NA BENDI sehemu ya kwanza.

  TANCUT ALMASI ORCHESTRA  wakiwa Jamhuri Stadium Dodoma   Sikumbuki ni safari ngapi za kimuziki nilizowahi kuzifanya hapa nchini katika m...