YOUTUBE PLAYLIST

Tuesday, May 11, 2010

Zahir Ally Zorro


Muziki una mengi ya kushangaza, unaweza ukafika wakati ambapo mwanamuziki fulani kila akitoa nyimbo inatokea kupendwa. Hali hii inanikumbusha kipindi Zahir Ally Zorro alipokuwa JKT Kimulimuli Jazz , bendi iliyokuwa katika kambi ya Mafinga huko Iringa. Wakati huo ambapo JKT ilikuwa na makundi mawili ya askari kuna wale waliojitolea kwa ridhaa kujiunga na jeshi hilo na kulikuweko na wale waliolazimika kujiunga kwa mujibu wa sheria. JKT ilianzisha bendi mbili ambazo zote zilikuwa na muziki mkali. Dar es Salaam kulikuwa na JKT Kimbunga Stereo, jina lililotokana na staili yao ya Kimbunga, na Iringa kulikuwa na JKT Kimulimuli, hii ilitokana na kuwa na taa za steji zenye kuwakawaka. Bendi ya JKT Kimulimuli ilipata umaarufu sana baada ya mwanamuziki Zahir Ally Zorro kujiunga na bendi hii. Ilikuwa ni kama lazima usikie vibao vya bendi hii kila siku radioni. Kabwe..tungo kuhusu mtoto mtukutu alieanza uhuni toka mdogo na kulazimika kufungwa hata jela ya watoto. Kitu mapenzi kilianza zamani.....maneno ya kibao kingine kilichogusa sana hisia za watu, Tausi...wimbo unaohusu mwanamuziki aliyemtungia wimbo mpenzi wake. Ilikuwa kama vile kila kibao anachotunga Zahir kinakuwa hit.

5 comments:

  1. Anonymous19:29

    Balozi hapa umenena kweli kweli. Mimi bwana huyu bwana namkubali, yaani amekamilika katika kila idara. Utunzi ni mtunzi mzuri sana, na sauti yake iko fiti hasa anapoimba nyimbo zake za hisia. Kitu kinachonisikitisha kuhusu Zorro ni kuel kujiunga na bongo fleva, ama kupiga muziki usio na akili. Huyu Zahir Ally anastahili kuwa na bendi yake pekee kwani ana kipaji cha aina yake. Namkumbuka sana kwa nyimbo zake kama Tikisa, Kisura, pamoja na Tabia ya Mapenzi. Bwana Zorro uko juu, achana na fleva zinakulostisha.

    ReplyDelete
  2. Anonymous13:06

    Huyu Bwana Ana kipaji sana. Mimi nakumbuka sana kwa wimbo wake wa 'kisa cha photo album'.

    Baadae alikuja kuanzisha bendi nyingine ya Jeshi 'JKT Ruvu'. Siku ya kuzindua kundi hili ilikuwa pale hall la JKT mgulani. Nakumbuka Zahir alichelewa kufika na kulikuwa na waalikwa waheshimiwa wengi wakuu wa jeshi. Mkuu wa JKT Ruvu - Lt. Canal Lameck Meena alitoa amri Zahir asipande jukwaani wala kupiga kabisa siku hiyo. Nilimwona akilalamika sana pale mlangoni kwa kuingilia Mgulani JKT hall karibu na geti la kutoka kambini upande wa uwanja wa taifa, ilikuwa mwaka 1986.

    by Marubaini

    ReplyDelete
  3. Anonymous15:12

    Anatisha huyu mzee ...bado yuko kwenye gemu hadi leo

    ReplyDelete
  4. Anonymous12:20

    Mkuu,

    Mdau Marubaini kazungumzia suala la Zahir Ali kuchelewa kwenye onyesho na kuamriwa kutopanda jukwaani na Lt. Colonel Lameck Meena. Tabia ya wanamuziki kuchelewa kwenye maonyesho naomba katika mada zako iwe ni moja kati ya mada za kujadiliwa.

    Asante.

    ReplyDelete
  5. Perez15:34

    Eee bwana Kitime umenikumbusha mbali sana huyu Jamaa namkubali sana.
    Umenikumbusha PHOTO ALBUM Mwanangu.

    "... Wamenambia mambo yako mabaya ehee...,
    Wamenieleza matatizo ya mume wako ee,
    Na kisa cha we Sheri Zinduna ee,
    Kufika kupewaa talakaa,
    Photo album, imeleta manenoo...,
    Katikati ya Daresalama
    Kisa ni picha ilopigwa zamani,
    Katikati ya mji wa Mwanza..."

    Yaani we acha tu.

    ReplyDelete

SAFARI ZANGU NA BENDI sehemu ya kwanza.

  TANCUT ALMASI ORCHESTRA  wakiwa Jamhuri Stadium Dodoma   Sikumbuki ni safari ngapi za kimuziki nilizowahi kuzifanya hapa nchini katika m...