Jukwaa la wapenzi wa mambo ya muziki wa Tanzania-

Breaking

Wednesday, May 19, 2010

Simba wa Nyika

Tanga ni mji ambao umekuwa chimbuko la mambo mengi katika ulimwengu wa muziki. Hata muziki wa dansi uliingia nchini kupitia Tanga. Kilimo cha katani chini ya mpango wake wa SILABU (Sisal Labourers Beureau) iliwezesha watu kutoka sehemu mbalimbali kukutana Tanga kwa ajili ya ajira ya kukata mkonge, na hivyo mchanganyiko huo wa makabila ulileta uchangamfu wa kimuziki katika jiji la Tanga mapema sana kuliko miji mingine. Kati ya mazao ya Tanga ni bendi maarufu ya Simba wa Nyika ambayo wanamuziki wake walitoka Tanga na kuweka makao yao kwa muda Arusha wakiitwa Arusha Jazz na mtindo wao Wanyika. Vijana hawa walipohamia Kenya wakajiita Simba wa Nyika na waliwasha moto wa nyika kimuziki na nyimbo zao tamu. Hapa ni picha yao mojawapo.

12 comments:

Perez said...

Kitime unaniumbusha mbali sana ninapokumbuka huu wimbo hapa chini.
We acha tu

"...Ohoo oo,
Sikujua kama utabadilika,
Najuta kupotezaa, wakati wangu, nyumbani kwako....,

baki salamaa, kuonana nawe ni majaliwa..

Ohoo oo ulimwengu kweli una mambo mengi..."

Anonymous said...

Wa pili kulia ni 'Profesa' Omari Shaaban na wa nne kulia ni George Peter Kinyonga. Wote kwa sasa ni marehemu. Profesa Omari alijitenga na Simba Wanyika mwaka 1978 na kuunda Les Wanyika. George Peter naye alijiengua mwaka 1980 na kuunda Orchestra Jobiso ambayo hata hivyo haikudumu muda mrefu. Alirejea Simba Wanyika miaka michache baadae. Wilson, George na Profesa Omari, ambao wote walikuwa ni Watanzania, walifariki mwishoni mwa miaka ya 1990 na kuzikwa Nairobi.

Anonymous said...

Wapi John Jambele

Anonymous said...

Profesa Omari aliibuka na kibao Sina Makosa akiwa na Les Wanyika baada ya kujitenga na Simba wa Nyika, lakini bado kuna utata hadi leo hii ni nani hasa aliyetunga kibao hicho. George Peter alisisitiza hadi kifo chake kuwa mtunzi wa kibao hicho ni yeye na kwamba Profesa Omari alimuwahi na kukirekodi baada ya kuondoka Simba wa Nyika. Hii inatukumbusha sakata la kibao cha ‘Wenye Nyumba Msiwaudhi Wapangaji’ ambacho kilirekodiwa na Mlimani Park na Bicco Stars mwanzoni mwa miaka ya 1990.

John Mwakitime said...

Taarifa nilizonazo ni kuwa wimbo ni wa Profesa Omari, na kichekesho kikubwa kilitokea siku ya kurekodi wimbo huu. Mwimbaji hakuja studio hivyo basi Issa Juma ambaye alikuwa mpiga drum akalazimika kuimba, na fundi mitambo alipewa kazi ya kupiga drums, matokeo ni wimbo unaoendelea kupendwa. Na kuanzia siku hiyo Issa Juma akawa ndo mwimbaji rasmi wa bendi.

John Mwakitime said...

John Jambele ni mpenzi mkubwa wa Simba wa Nyika ambaye ana taarifa nyingi sana za bendi hii

Anonymous said...

Wakuu,

Kuna mtafiti anaitwa Doug Paterson ametafiti sana juu ya Wanyika. Pia kuna tovuti hii(http://biochem.chem.nagoya-u.ac.jp/~endo/EAWanyika.html) yenye maelezo mengi ya Wanyika.

Asanteni.

Anonymous said...

John Jambele atafutwe anazo kumbukumbu nyingi sana za watu hawa.

Anonymous said...

Issa Juma alijiengua Les Wanyika mwaka 1981 na kuunda Super Wanyika. Kulikuwa pia na kundi lingine lililotokana na Les Wanyika lililojulikana kama Wanyika Stars. Issa Juma aliachana na muziki kwa muda mwaka 1985 na kujichimbia mjini Eldoret alikojitosa katika biashara. Hiki ni kipindi ambapo utawala wa Daniel arap Moi uliwaandama sana wanamuziki wa kigeni, hasa kutoka Tanzania na Congo, kiasi cha wengi kuikimbia nchi hiyo na kuja Tanzania. Miongoni mwa wanamuziki wa Kitanzania waliorejea nchini kipindi hicho ni marehemu Eddy Sheggy na watu kama Mohamed Tungwa na Freddy Mwalasha. Wanamuziki wa Congo waliokimbilia Tanzania miaka hiyo ni pamoja na Lovy Longomba (RIP), Fumutoto Monimambo Jimmy (RIP), Fataki Lokassa (RIP) na Bibiley Kabakaba. Issa Juma alirejea nchini mwishoni mwa miaka ya 80 na kufariki miaka michache baadaye. Les Wanyika bado ipo katika ulimwengu wa muziki ikiongozwa na mwimbaji Freshley Mwamburi. Hata hivyo, tofauti na miaka iliopita, wanamuziki wengi wa bendi hiyo kwa sasa ni Wakenya.

Anonymous said...

Simba Wanyika na Les Wanyika ni miongoni mwa bendi kadhaa za Kitanzania zilizowika nchini Kenya miaka ya 80 na 90. Bendi nyingine za Kibongo zilizotikisa Kenya ni kama Les Volcano chini ya Charles Ray Kasembe (RIP) na Nairobi Matata iliyokuwa ikiongozwa na James Lugendo kama sijakosea. Huyu Lugendo sijui yu wapi kwa sasa. Wenye taarifa zake watuhabarishe kupitia jukwaa hili.

Anonymous said...

Mara ya mwisho kumuona Profesa Omari ilikuwa ni mwaka 1997 sehemu moja inaitwa Githembe jijini Nairobi. Nilistuka kuona jinsi alivyodhoofu na alivyokuwa akiomba fedha kwa aliokuwa akiwafahamu. Mimi binafsi aliniomba shilingi 10, lakini nakumbuka nilimpa shilingi 50. Kwa hakika huyo hakuwa Profesa Omari wa miaka ya 70 niliyekuwa nikimfahamu. Hakika simulizi ya kuporomoka kwake kimuziki na kimaisha kabla ya kifo chake zinasikitisha.

SENETA WA MSONDO said...

JF naona umeibania comment yangu ya kuhusu mahusiano ya TX MOSHI Na WILSON na GEORGE PETER KINYONGA,Poa nadhani ilikua bahati mbaya au urefu ulikukwaza,poa tuko pamoja,leo naomba wenye data ukiwemo wewe wanisaidie,kuna uvumi kwamba wimbo wa les wanyika wenye maneno "kajituliza kwake kasuku hataki maneno aomba mungu amsaidie" huyo kasuku waliyekuwa wakimzungumzia ni mwalimu nyerere,na waliutunga ili kuipiga dongo serikali ya kenya ambayo wakati huo haikua na mahusiano mema na serikali ya mwalimu.Je uvumi huo una chembechembe za ukweli ndani yake?

Adbox