YOUTUBE PLAYLIST

Monday, May 3, 2010

Mitindo ya Bendi

Nikisema tuanze kutaja mitindo ya bendi ni mingi sana maana kila bendi imekuwa inakuja na mtindo wake. Majina mengine ya mitindo yana historia na maana na mengine yana kuwa yakutunga na kwa kweli hata waliokuwa wanayatumia hawana maelezo ya maana ya maneno hayo. Mundo,Msondo, sokomoko, dondola, kiweke, segere matata,super mnyanyuo, vangavanga, chikwalachikwala, libeneke na kadhalika ilikuwa mitindo ya bendi mbalimbali, na muziki wa bendi ulikuwa ndiyo unaonyesha utofauti huo. Kwa mfano katika mji wa Tanga ulikuwa na bendi kubwa mbili, Jamuhuri Jazz na Atomic Jazz. Jamhuri ilikuwa na mtindo wa Toyota, na baadae Dondola, hata muziki katika awamu hizi mbili katika bendi hiyohiyo ulikuwa tofauti. Atomic walikuwa na mtindo wa Kiweke. Muziki wao ulikuwa tofauti na ule wa Jamhuri. Na wapenzi wa Jamhuri hata wakizeeka husifu mtindo wa upigaji wa Jamhuri na rythm la Harrison Siwale(Satchmo). Kadhalika wapenzi wa Atomic watakwambia hakuna kama Kiweke, upigaji solo wa John Kijiko, bass la Mwanyiro na kadhalika. Mtu ambae kisha sikia muziki katika mtindo wa Ambianse wa Cuban Marimba, hawezi kuchanganya na Likembe wa Moro Jazz. Nimeanza kwanza kwa kutaja bendi zilizokuwa katika mji mmoja tena huko mikoani ambapo watu walikuwa wachache na wanamuziki wanajuana na kuishi jirani. Hali hiyo ndio iliyokuwa Tabora, ambako pamoja na Tabora Jazz, kulikuweko na Nyanyembe Jazz, Kiko Kids, muziki wa kila bendi ulikuwa tofauti na mwingine. Dar es salaam kulikuwa na bendi nyingi na hivyo mitindo mingi. Hakuna aliyeweza kuchanganya Maquis na OSS, wala Sikinde na msondo, Sokomoko, afrosa, Katakata vumbi nyuma ya Kyauri voice havikuwa na mpka wa kulinganishwa. Kikubwa ninachotaka kueleza ni kuwa bendi kuwa na mtindo ilikuwa si jina tu bali kulikuweko na kazi ilifanyika ili kupata kulinda na kuendeleza mtindo ambao bendi iliamua kuwa nao. Nakumbuka wakati wa mazoezi enzi hizo unaweza ukatunga wimbo ukianza kuimba wenzio watakwambia mbona unafanana na bendi fulani na hapo utakarabatiwa mpaka uwe katika mtindo wa bendi husika.

9 comments:

  1. Anonymous23:01

    Balozi, ni kweli kabisa nakubaliana nawe moja kwa moja. Nakumbuka mwaka 1981 pale Mwananyamala wakati Matimila wanafanya mazoezi ya wimbo wa Almasi. Kasalo aliimba sauti fulani halafu Remmy akamwambia mbele ya mashabiki kuwa ile sauti inafanana sana na Maliki Star wa Orch. Makasy, hivyo asiikaze sana. Kumbuka, kuwa Matimila ilikuwa na karibia ya wanamuziki wote wa Makassy na wakaja na staili yao pekee ya Talakaka eh! Huu ndo muziki wetu wa asili, kweli bendi zilitofautiana na mitindo yao. Sikinde, ukisikia tu wimbo redioni utajuwa hiyo ni Sikinde, Pamba Moto (solo la Kalala), Msondo, Zembwela (solo zito la nguza), Talakaka (solo la bati Osenga), Chakachua (solo la Michael Vincent) yaani utamu kweli kweli!

    Hivi Michael Vincent yupo wapi na bado anaendeleza libeneke la solo lake?

    ReplyDelete
  2. Michael Vincet alikwishafariki zamani. Soloni moja wapo ya vionjo, kulikuwa na vitu vingi aina ya kupiga rythm, drums,besi na kadhalika

    ReplyDelete
  3. Anonymous23:19

    Kweli balozi nakubaliana nawe, kulikuwa na vionjo vingi sana. Sikiliza ule wimbo wa Penzi La Mwisho wa Sikinde. Katika vtyombo (sebene) utasikia Mwanyiro akilia na lile gita lake la bezi, mhhhhh mhhhh mhhhh, yaani ananifurahisha sana na ule utundu wake pale.

    Kingine balozi, hivi ule upigaji solo ama tuseme upigaji wote wa muziki katika bendi, ni kiongozi ndiye anayetaka bendi yake ipigeje ama?

    ReplyDelete
  4. Perez00:02

    UDA Jazz - Bayankata.
    "..Tulizaliwaa woote, kijiji kimoja, lakini ulishindwa kunioa kwa sababu, ulisema sina tabia nzuri eeh! Sasa nimeolewa..."

    Atomic Jazz
    "..Leo nakupasulia ee, mpenzi wangu nikupendae, usione ninateseka, ni we peke nikupendae..."

    ...ndugu ee nihurumiee mwenzio ee niko mashakani,
    nisije nikapoteaa oo oo niko mashakani..."

    ReplyDelete
  5. Anonymous00:53

    Balozi, nimesikia kibao cha Orch. Vijana Jazz 'Bujumbura' kina sound kama new version ktk linki hii http://dalstonoxfamshop.blogspot.com/2009/02/blog-post.html

    Je Vijana Jazz wamefufuka upya maana hii version ya vyombo na sauti na madoido sijapata kuisikia ktk "Buja', kwani wengine tuliondoka kitambo nyumbani.

    Mdau
    BabaJunior

    ReplyDelete
  6. MIaka michache iliyopita Vijana Jazz walitoa album yenye nyimbo za zamani kwa kurekodi upya nyimbo hizo. Ilitegemewa jambo hilo lingeirudisha bendi katika chart lakini haikusaidia.

    ReplyDelete
  7. Anonymous18:12

    Balozi,
    asante kwa kutufahamisha majaribio ya Vijana jazz kurudi ktk chati, ushauri wangu wasikate tamaa kwani version mpya nimeipenda ya Bujumbura, Aza, VIP n.k labda waongeze mbinu za kutawala steji na kuvuta hisia za mashabiki wakati wa live concerts labda itaamsha wimbi jipya la washabiki.

    Mdau
    BabaJunior.

    ReplyDelete
  8. Anonymous00:48

    Kweli Baba Junior, inabidi bendi zetu si Vijana tu iangalie namna ya ushambuliaji wa jukwaa, ni muhimu sana kwa mashabiki.

    ReplyDelete
  9. Mimi nafagilia sana miziki ya zamani kutokana na ujumbe maridhawa na umbuji wa upigaji vyombo. Vijana Jazz ni moja ya bendi zilizokuwa kali sana nikumbuka nyimbo kama vile Masaki,Chaurembo, Na Nani? (..Mimi nilie na nanii..eehh..utu na hasira ni vituuu tofautiiii mamaaa eeh.Lakini mitaani inaaminika kuwa bendi hii imekua mahututi baada ya kuundwa TOT.Inaonekana nguvu imeelekezwa TOT na kuacha Vijana ima makusudi au bahati mbaya.Ni kama ilivyokua kwa Twanga na Chipolopolo nyingine inapewa umuhimu nyingine inasahauliwa, sijui ukweli ukoje

    ReplyDelete

SAFARI ZANGU NA BENDI sehemu ya kwanza.

  TANCUT ALMASI ORCHESTRA  wakiwa Jamhuri Stadium Dodoma   Sikumbuki ni safari ngapi za kimuziki nilizowahi kuzifanya hapa nchini katika m...