YOUTUBE PLAYLIST

Sunday, April 18, 2010

TP OK Jazz Dar es Salaam 1974

Mwaka 1974, TP OK Jazz chini ya Lwambo Lwanzo Makiadi walitembelea Tanzania, na kupiga show tatu. Moja National Stadium, Diamond na Bahari Beach. Onyesho la Bahari Beach walishirikiana na Afro 70. Matokeo ya ushirikiano huo yalijitokeza kwa nyimbo kadhaa zilizopigwa na Afro 70 kuwa na solo lilifuata mipigo ya Franco. Nyimbo kama Dada Rida, Umoja wa wakina Mama, ni baadhi ya nyimbo hizo,tena hii nyimbo ya pili ilikuwa kama kopi ya wimbo Georgette wa Franco. Ujio huo ulianzisha utamaduni uliodumu kwa muda mrefu wa bendi kupenda kutumia vifaa vya aina ya Ranger FBT.
















9 comments:

  1. Patrick Tsere07:29

    Baada ya performance yao Dar na Zbar walikwenda Arusha. Wakati huo mimi nilikuwa field wilaya ya Same mkoa wa Kilimanjaro. Nakumbuka ilikuwa Julai 1974.Waliletwa na Rais Mobutu ili washiriki sherehe za Saba Saba. Walikuja kama wageni wa Serikali ya Tanzania. Kwa hiyo they were VIPs na itifaki zote muhimu zilizingatiwa. Okay Jazz ilikuwa habari ingine bwana. Ndiyo maana mpaka leo muziki wao bado ni nambari one. Kama msondo tu.

    Nakumbuka sikulala vizuri nikisubiri kwa hamu ujio wa TP Ok Jazz. Siku ilipofika mimi nikaondoka Same nikaja Arusha. Pale ARusha walipiga muziki ule uwanja wa Sheikh Amri Abeid. Watu wengi hawakuwa na uwezo wa kulipa kiingilio kwa hiyo walipanda kwenye paa za nyumba zilizokuwa karibu na uwanja ule tokea upande wa Kaloleni wakimtazama na kuburudika na muziki Mzee wa Madevu na Madevu. Franco alipoona hali hiyo akaamuru waruhusiwe kuingia bure. Aisee Stadium ilifurika. The music was nice. Nyimbo kama Cedou na nyinginezo ndiyo wengine tulizisikia kwa mara ya kwanza.

    Usiku akapiga shuleni Arusha School lakini walisitisha baada ya askari mmoja wa FFU alipoamua kuwafukuza watu waliotaka kuingia bure kwa kuwatupia bomu la machozi. Yule askari mpuuzi hakujua kuwa ule moshi ulikuwa haubagui kwa hiyo uliingia mpaka ukumbini ambako sisi wengine tulikuwa tunasakata rumba. Siyo siri yule askari alituudhi wengi. Kwa sababu ule muziki ulikuwa umepigwa kwa nusu saa tu. OK Jazz wakasema hawawezi kuendelea na performance.

    That was 1974. Lakini mwaka 1966 African Fiesta na Dr Nico Kasanda walikuja Dar wakiwa wageni wa Dar Young Africans na Western Jazz. They performed in Dar and Morogoro. Ninakumbuka marehemu baba yangu alikuwa akifanya kazi Morogoro kama Regional Medical Officer. Na mzee Saidi el Maamry alikuwa RPC na mkuu wa Mkoa alikuwa marehemu Clement Kapilima. Kuna vituko na vioja vilitokea kwenye ziara hiyo huko Morogoro ambavyo nilivishuhudia. Anyway siwezi kusimulia hapa unless you insist.

    ReplyDelete
  2. Pat, pamoja na kuinsist utueleze vituko wakati huo, ningependa nigusie moja kuhusu ujio wa Dr Nico. Tulikuwa tunaishi Iringa wakati huo, lakini baba yangu aliwasha Ki VW chake na tulikuja mpaka Dar kwa ajili ya Dr Nico, na kwa kuwa nilikuwa mdogo ililazimu tupaki na kukaa nje, na kusikiliza muziki kutoka kwenye gari. Wimbo ambao huwa unaniijia kichwani kila mara ni ule ulioimbwa kumlilia Lumumba, uliimbwa kiswahili....... Baba Lumumba usisahau nchi yako ya Kongo.......Afrika mzima wanalia Lumumba wa Kongo e, President Nyerere analia Lumumba wa Kongo......
    Dansi hilo liliporomoshwa katika ukumbi wa Arnatougro, ukumbi ambao historia inaonyesha Jiji limewadhulumu wasanii, kwani aliyejenga George Arnatougro alijenga kwa ajili ya shughuli za sanaa. Si viwanja wa michezo tu vilivyodhulumiwa nchi hii.

    ReplyDelete
  3. Anonymous14:04

    Kaka umenikumbusha mbali kukata picha kwa magazeti na kubandika kwa madaftari album za ukweli

    ReplyDelete
  4. Danstan21:54

    Ndugu zangu mnaburudisha mnavyokumbushia mambo hayo ya muziki zamani.

    Mheshimiwa balozi,kwa kweli hebu tumalizie hiyo story ya vituko vilivyotokea. Ndio raha yenyewe.

    ReplyDelete
  5. Anonymous22:58

    Mkuu,

    Siku TP OK Jazz walipopiga Diamond Jubilee ni moja ya siku kubwa sana ambayo picha yake haitatoka kichwani kwangu kirahisi.

    Wakati huo tulikuwa tunaishi Maweni Street, Upanga. Ni mitaa mitatu toka Diamond Jubilee. Nyuma ya nyumba tuliyokuwa tunaishi alikuwa anaishi ofisa mmoja wa Ubalozi wa Zaire/Kongo. Wanawe huyo ofisa na nduguze walikuwa ni marafiki wa karibu sana. Urafiki wetu ulifikia kiwango Dada yangu mkubwa na dada yangu mdogo kuongea Lingala fluent na mimi kujua Lingala kwa kiasi fulani. Bado naongea Lingala lakini ya kubabaisha babaisha.

    Ok, siku hiyo kati ya wageni waalikwa miongoni mwao walikuwa wazazi wangu. Tulienda mpaka Diamond Jubilee jioni ile ili kuona kama tutaweza kupenya. Tulikuwa tuna njia zetu za kuweza kuingia ukumbini kwa sababu pale palikuwa uwanja wa nyumbani. Lakini siku hiyo hata yule Mmakonde mlinzi mrefu tuliyekuwa tunamuita Mapekosi au Machale alikuwa hana namna ya kutupenyeza. Kulikuwa na ulinzi kabambe. Nadhani mgeni wa heshima jioni ile alikuwa Waziri Mkuu Marehemu Rashid Kawawa. Magari yalikuwa mengi sana pale mbele ya Diamond Jubilee na mengine ilibidi yaegeshwe mitaa ya Shule ya Shabaan Robert na maeneo ya karibu karibu.

    Baada ya lile onyesho ilikuwa ni kusikiliza miziki ya Franco tu haswa Azda na Dje Melasi.

    Athari niliyoipata baada ya onyesho lile ni kuwa ardent fan wa Franco. Nimetazama kwenye Ipod yangu na kukuta nina nyimbo 172 za Franco kutoka katika album 26!

    Marehemu Franco si tu alipiga muziki mzuri. Muziki wake pia ulikuwa umejaa ujumbe mzito sana iwe ni katika mapenzi, siasa, mambo ya kijamii au kiuchumi. Miziki yake ilisheheni kila namna ya uzuri. Wadau wengi wamejaribu kutengeza album mbali mbali na kuziita The Best of Franco lakini kila album utakayoisikiliza utakuta imepungua nyimbo nyingi nyingine ambazo zingeweza kuwemo.

    Miaka mingi baadaye nilibahatika kuwaona TP OK Jazz Uwanja wa Taifa Dar es Salaam lakini Franco hakuwemo kundini alikuwa ameshafariki.

    ReplyDelete
  6. Anonymous23:04

    Balozi Kitime, mimi nilikuwa mdogo sana miaka hiyo ya 70, ila naomba unieleze ni bendi gani haswa ambayo ilikuwa inanyanyasa pale dar from 1973 mpaka maybe 78. Yaani ni bendi ipi ikipiga watu ufurika kama dagaa kauzu gengeni, na ambayo ilikuwa ni gumzo zaidi pale jijini Dar wakati huo.

    ReplyDelete
  7. Bendi zilikuwa nyingi na hazikuwa namtindo mmoja kama sasa hivyokila moja ilikuwa inatesa kivyake.

    ReplyDelete
  8. Anonymous23:25

    wimbo dje melasi ndio uliompatia sifa mosesengo fan fan kwani ndie aliyeutunga...wimbo azda ulikuwa ni kusifia magari ya vw(volks wagen)...ndo maana kunasikika maneno ...vewe vewe..azda...kombo ya sika..

    ReplyDelete

  9. ..Dah!hizi kumbukumbu hizi! Jamani mimi nakumbuka kuwa TP OK Jazz walifika Dar kwa mara ya kwanza 1973. Nilikuwa darasa la sita hapo shule ya Msingi Chang'ombe. Nakumbuka jinsi jiji lilivyohamanika kwa ujio ule.
    Usiku wa siku tukapigwa karantini ya kutoka nyumbani wakati wazee wetu wanakwenda Uwanja wa Taifa kushudia live show ya gwiji huyo.
    Ile wanatoka tu sisi huku tukakusanyana watoto wa mtaa mzima wa NGORONGORO Str na kupiga mbio kwenda uwanjani na kufaulu kuingia kupitia mipenyo ya ule upande wa Uwanja wa ndani.
    Tukaingia na kunogewa!
    Muziki ulipokwisha wazazi wakaondoka na magari na kurudi nyumbani na kukuta mtaa mzima upo tupu hauna watotot!! Nakumbuka Fito zilizotembea maungoni mwetu usiku ule hazina mfano!
    Nakumbuka pia Wanenguaji wa OK Jazz ndio ukaleta mtindo wa bendi kuwa na wanenguaji.
    Nakumbuk pia wakubwa zetu walikuwa wnavaa Pekos lakini lakini siku hiyo Lwambo alivaa Booonge la Bugaluu na kuanzia siku hiyo kila Mtu jijini akaanza kuvaa Bugaluuu!!!

    ReplyDelete

SAFARI ZANGU NA BENDI sehemu ya kwanza.

  TANCUT ALMASI ORCHESTRA  wakiwa Jamhuri Stadium Dodoma   Sikumbuki ni safari ngapi za kimuziki nilizowahi kuzifanya hapa nchini katika m...