YOUTUBE PLAYLIST

Saturday, April 3, 2010

Teknolojia na ubora wa muziki

Nadhani kuna haja ya kuongelea swala la teknolojia katika muziki na hapa nitazungumzia teknoljia ya kurekodi. Nyimbo karibu zote ambazo husifika kama zilipendwa zilirekodiwa wakati wa kutumia kanda(tape), kwa teknolojia iliyoitwa 'two track recording' (pichani juu). Kwa teknolojia hii ilihitaji wanamuziki kuwa wazuri sana na fundi nae kuwa mzuri, kwani kama unarekodi wimbo bendi nzima lazima ipige kwa pamoja na akikosea mtu lazima kurudia wimbo wote tena kwa pamoja. Kwa bendi zilizorekodi RTD miaka hiyo zilipewa siku mbili za kurekodi kinachoitwa album siku hizi, yaani nyimbo sita au zaidi kwa kipindi cha siku mbili. Siku ya kwanza Bendi ilitakiwa kufika asubuhi kwenye studio za RTD, ambapo ilifanyika kazi ya kufunga vyombo vyote na kuvijaribu hapo fundi mitambo ndipo alipokuwa na kazi kubalance vyombo vyote viwe vinasikika inavyostahili. Mchana wa siku hiyo ililazimika bendi kurekodi nyimbo zote bila kukosea hata kama ni kumi. Siku ya pili ilitumika kurekodi kipindi cha klab raha leo show. Mwanamuziki yoyote wa siku hizi atakwambia haiwezekani kurekodi nyimbo sita kwa siku moja. Teknolojia ya sasa hutumia njia inayoitwa 'multi track recording', ilianza kwa kurekodi kwenye kanda maalumu tack 4,kisha zikawezekana 8,16,32 na kuendelea. Siku hizi kwa kutumia program za kompyuta ktu una uwezo wa kuwa na mamia ya tracks, hivyo basi hata bendi ya watu mia kila mtu akaweza kuja siku yake na kurekodi kipande chake , akakakirudia mpaka kikawa sawa, na ndio maana siku hizi kurekodi wimbo mmoja inaweza ikachukua hata mwezi na zaidi , kwa kurudia sehemu zenye makosa, kuzibadili kabisa na kadhalika, na siku hizi kuna hata teknolojia inayoweza kurekobisha sauti iliyoimbwa vibaya kwa maana hata kama hujui kuimba unaweza ukatengezwa mpaka uonekane unajua kuimba. Kama kawaida teknolojia mpya ina faida nyingi sana lakini mwisho wa yote faida hizi huonekana pale akiwepo fundi mitambo mzuri na msanii mzuri. Waliorekodi enzi za two track duniani kote husifia ule utamu ambao hupatikana wakipiga pamoja, ambao hupotea kama kazi itarekodiwa kila msanii akija kwa wakati wake.

12 comments:

  1. tamba00:02

    Kaka nimefurahia sana blogu yako. Wewe ni mwalimu. Hujui tu.

    ReplyDelete
  2. Patrick Tsere15:32

    Muziki wa zamani kwa kweli ulipigwa na wataalamu. Siyo sasa ninaweza nikatoka zangu hadi Kigoma maeneo ya Ilagala nikiwa na CD yangu kibindoni na nikajidai mimi ndiye Mwanafalsafa. Nikapozi na Mike na kutembeza midomo watu wakafurahi wakanilipa mie huyo. Siyo siri John I hate playback. It kills talents na mazingira yake ya kifekifeki sana. Fine the technology is good but the reality is not the truth my friend. Unless sielewi ninachochangia humu ndani.

    ReplyDelete
  3. ..Umeongea la msingi...Hapo zamani wanamuziki walikuwa ni makini katika kazi zao....Siku hizi wanamuziki wengi hawajui kutumia ala za muziki na pia wanategemea sana kompyuta....

    ReplyDelete
  4. Anonymous06:14

    Mze Kitime wewe ni mwanamuziki ambaye nakuzimia sana katika upigaji wako gitaa. Ulinifurahisha sana na ile albamu yenu ya malaine (penzi halina shule). Nina mengi sana ya kuandika lakini ngoja nikuulize swali moja tu ambalo bado linanikuna sana kichwani. Hivi ni mpiga solo gani TZ ukichukulia hawa wacongo na wazalendo kama kina marehemu Mulenga, Mze Baltazar, Kalala, Bati Osenga, Fan Fan, Nguza, Kasheba, Elombe Kichinja (F.M. Academia), Pitchou (Vijana wa masauti), Shube wanted, pamoja na Mze Mabela na wengineo mastadi. Hivi kwa kweli kuna anayemzidi Shuibe wated hapa? Tuache ubishi usio na sababu, naona shube wanted kiboko. Tafadhali naomba ulete hoja hii ya wapigaji wa ala kisha ulete pia hoja ya waimbaji. katika uimbaji mi naona ngoja nianze na Gotagota (electronic voice).

    ReplyDelete
  5. Kuna ugumu sana kuanza kupima ubora wa msanii maana lazima uweke vigezo.Bila vigezo inakuwa taabu, na tena vigezo ananweka nani? unajua kuna wapiga solo wanajua vizuri staili nyingi, lakini hawapendi kupiga stail flani ambayo wewe unapenda. Hivyo unaweza kudhani hafai kumbe wewe ndo umepanga vigezo ambavyo havimhusu. Wote uliowataja nawaheshimu sana katika upigaji wao. Hebu nambie utampimaje Gotagota na Mzee Gurumo, wanaimba sauti tofauti, hakuna kigezo hapo

    ReplyDelete
  6. Anonymous08:48

    Asante John kwa maelezo yako juu recording ya nyimbo. kwa jinsi ulivyofafanua nachelea kusema kwamba vipaji na uwezo wa wanamuziki wapya upo hatari.....tutakuwa na watu wengi wanaojiita wanamuziki lakini kimsingi sio wanamuziki ila ni 'WASANII'. Ninyi manguli wa zamani mlilazimika kujisahihisha ninyi wenyewe kabla hamjaingia studio...sasa ikiwa watu wanaingia studio halafu wanasaidiwa na mitambo nadhani hapo hakuna vipaji ila kuna vifaa vizuri.

    Pia inapokuja suala la live performance hapo ndio utajua mbichi na mbivu. Music uliyonunua kwenye CD ya mwanamuziki hafanani kabisa na kile unachokisikia jukwaani.....na zaidi je wimbo wenye track say 60 unaweza kupingwa live na wanmuziki jukwaani?

    Nashukuru sana kwa mada zako nzuri, zinatufurahisha na kutuliwaza sana hasa sisi walevi wa muziki.

    By Petro

    ReplyDelete
  7. Ni kweli live shows huwa kipimo kikubwa kwa wasanii wetu, unakuta nyimbo imeimbwa vizuri kwenye CD lakini msanii huyohuyo akiimba live ni disaster ndo maana wengine wanajijua hivyo wakati wa playback hata mic haiwashi, anachezesha midomo, anaigiza kuimba.

    ReplyDelete
  8. Anonymous00:37

    Mze Kitime, nakubaliana na uyasemayo hapa. Je, wewe unavutiwa na nani katika upigaji ala na uimbaji?

    ReplyDelete
  9. Kwanza nikushukuru Uncle Kitime kwa chambuzi makini juu ya Muziki na Wanamuziki wa Tanzania.
    Suala zima la "maendeleo" katika muziki huu wa kizazi kipya ni PARADOX.
    Yaani yanaangaliwa kwa URAHISI WA KAZI YA KUREKODI (japo urahisi huo waendana na upungufu wa ubora wa muziki, wanamuziki na hata uwajibikaji). Kama ulivyosema, zamani kurekodi ilikuwa ni sawa na kutumbuiza jikwaani. Mlirekodi kama vile mnafanya "show" na ndio maana uwezekano wa kupata muziki uliokaribiana kiwango jukwaani na kwenye rekodi ulikuwa mkubwa.
    Lakini ukiangalia kwa undani kuna kazi kuubwa saana ambayo yastahili kufanywa ili wasanii waweze kufanya maonesho yatakayosikika kama ilivyo kwenye rekodi.
    Nilipoenda kwenye onesho la Burning Spear, nilishngazwa na mshabihiano wa muziki wake jukwaani ukilinganisha na kwenye CD, nilipokuja kununua CD yake ilikuwa ni "dual" ambayo ni video na audio na video yake ilionesha namna anavyohimiza kutengeneza wimbo kwa vyombo asili, anavyohangaika kupata sauti iliyo mwanana toka katika kila zana na anavyojitahidi kurekodi kama anayefanya tamasha.
    Anasema licha ya teknolojia kuwa msaada, lakini kwa unaloweza kufanya kutoukimbia ubora wa muziki ni vema kufanya hivyo.
    Wasanii wa sasa (hasa wa muziki wa kizazi kipya) wanabweteka na hii iitwayo teknolojia. Wanakuwa wavivu, wazembe na sasa twaona msanii hawezi kufanya onesho la nonstop kwa masaa mawili (licha ya kuwa ana-lip sing)
    Tunaweza kusema ni maendeleo ya vifaa vya kurekodi lakini ni UUAJI wa ubunifu na ujuzi kwa wasanii wavivu.
    Leo hii hata ngoma (ambazo zimejaa mitaani) wanataka kutumia za kwenye kinanda (kwa kuwa tu kipo na kinazo).
    Kwa ufupi niseme TUNAJIPOTEZA KATIKA HARAKATI ZA KUJITAFUTA

    ReplyDelete
  10. Anonymous19:14

    Nakumbuka kuna siku Muhidin Gurumo alisema muziki huu wa kisasa umekosa uhalisia, kwa Kiingereza tunaweza kuuita 'artificial'. Nakubaliana naye kwa asilimia mia moja. Kompyuta zimewapa watu mteremko kiasi kwamba kila mtu sasa anaweza kuwa mwanamuziki au msanii. Vijana wa sasa hawataki kujifunza kupiga ala na kwa staili hii sidhani kama Tanzania kutatokea akina Mbaraka Mwinshehe, Marijani Rajab, Michael Enock, Wema Abdallah, Shaaban Yohana, Harrison Siwale, Duncan Njilima, Said Mabera na John Kitime wengine. Kila ninaposikiliza muziki wa zamani huwa najiuliza kama itatokea tena Watanzania kupiga muziki kwa ufundi wa hali ya juu kiasi hicho.

    ReplyDelete
  11. Mi nadhani pia kuna jambo jingine ambalo lazima kuliongelea, nalo ni vyombo vya habari vya utangazaji, si kwamba hakuna vijana ambao wanajifunza na wanapiga muziki wa ala , ila kwa makusudi kazi zao hazipati nafasi kusikika na kufahamika katika vyombo vyetu ambavyo navyo ugonjwa wa rushwa umevikumba kwa kiasi kikubwa.

    ReplyDelete
  12. Anonymous00:22

    Mze Kitime nakubaliana nawe juu ya ulaji rushwa hapa. Najua fika vijana wengi wa bongo flava hutoa rushwa ili nyimbo zao zisikike redioni, cha kushangaza basi hizo nyimbo zenyewe hazina ubora wowote. Kingine, naona ma-dj wengi wa TZ nao hawana uwezo, na hii yote inatokana na kutokuwa na ujuzi kwani kazi zao zote wanazinunua kutoka nje ya nchi na kuzichuja hapo Bongo na ndiyo maana utakuta beats zote za flava ni zile zile, yaani hakuna hata radha. Kwa kweli inasikitisha kama hatutobadilika haraka. Ebu angalia hapo Bongo yaani kila baada ya nyumba mbili utakuta kuna msaniii wa flava. Mtu hana uwezo wowote wa kimuziki lakini anajiita msanii kisa kapikiwa beats na computer kisha yeye anatia sauti tu. Hawa ma-dj wetu bongo wanaua sana kazi za wanamuziki wetu wa asili. TZ tuna wanamuziki wengi wazuri, tena wengi mno ila ma-dj wa redio na rushwa zinawaua. Nilisikitika sana kuona video ya Mze Zahir Ally ile ya flava akiwa na dj-choka. Yaani Mze wa watu alichemsha ile mbaya. Zahir Ally ni msanii mzuri na namzimia sana ila pale alipotea njia kuimba flava, alikuwa out of tune na zile beats cha kushangaza bongo watu haswa ma-dj wanaushupalia ule wimbo, si ujinga huu au wanataka kufananisha TZ na marekani? Katika usikilizaji wangu wa bongo flava, hakuna msanii yeyote mzuri wote wababaishaji tu, ebu angalieni kijana wa Zahir Ally yule Banana, ana ujuzi gani? Kuimba hajuwi, mashairi hadimu, yaani tuseme ni mashairi ya ngumbalu halafu anaitwa bongo super star. Hivi mastaa wa bongo hawajulikani kweli jamani? Mze Kitime, kwa nini msiitishe vikao na wenye maredio nchini mzungumzie ili suala la ukandamizaji wa ma-dj dhidi ya muziki wa dansi?

    ReplyDelete

SAFARI ZANGU NA BENDI sehemu ya kwanza.

  TANCUT ALMASI ORCHESTRA  wakiwa Jamhuri Stadium Dodoma   Sikumbuki ni safari ngapi za kimuziki nilizowahi kuzifanya hapa nchini katika m...