YOUTUBE PLAYLIST

Tuesday, April 20, 2010

Shaaban Yohana Wanted


Nilikutana na Shaaban Yohana kwa mara ya kwanza katika bendi ya Tancut, ambapo gitaa lake la solo husikika katika nyimbo zote zilizokuwemo katika album za kwanza za bendi ile. Alipiga gitaa katika nyimbo zifuatazo:-
Nimemkaribisha nyoka
Kashasha
Tutasele
Mtaulage
Masafa Marefu
Butinini. Lakini aliniacha Tancut na kwenda Vijana Jazz huko tukakutana tena ambako solo lake linakumbukwa katika nyimbo nyingi kama vile Aza, Ogopa Tapeli,Thereza, Shoga, Malaine nk. Aliacha bendi ya Vijana na kujiunga na Ngorongoro Heroes akatesa sana huko, kisha akatimkia Botswana ambako yuko mpaka leo, muda mwingi akiutumia kama mwanamuziki wa studio.

35 comments:

  1. Anonymous05:53

    Sijawahi kuona talent kama ya Wanted katika mpiga solo yeyote bongo...Much respect to Mulenga, Baltazar, Mkanyia, Kalala, Kassim Rashid, Pangamawe, Michael Bilal, Dekula and kina Uvuruge, but Shaaban ana kipaji cha namna yake kabisa katika mpini wa solo!

    ReplyDelete
  2. Anonymous10:35

    Nakubaliana asilimia mia moja na mtoa mada hapo juu. Wanted ni habari nyingine. Mwanamuziki huyu ana kipaji cha pekee cha kucharaza solo ambacho Watanzania hatuna budi kujivunia.Mirindimo yake ya solo katika muziki wa Tancut Almasi na Vijana Jazz wa miaka ya themanini na mwanzoni mwa miaka ya tisini haina mfano. Wanted anaweza kabisa kuwatoa nishai watu kama Diblo Dibala, Dally Kimoko na Alain Makaba wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo. Ni bahati mbaya tu kwamba alivuma enzi ambapo muziki wa Tanzania ulikuwa hausikiki sana nje.

    ReplyDelete
  3. Nakubali kabisa kuwa Shaaba Wanted alikuwa mpigaji mzuri sana. Lakini si vizuri kulinganisha kwa harakaharaka na kumwona bingwa kuliko wengine. Magitaa hupigwa kwa staili tofauti. gitaa la Michael Enoch ni tofauti na la Michael Vicent, na tofauti na la Juma Ubao, utalinganishaje? Ila nakubali kumlinganisha Shaaban na akina Dally Kimoko kwani hao ndo alikuwa akipiga staili yao.

    ReplyDelete
  4. Anonymous12:45

    Hivi kwa mtindo huu wa muziki wa kizazi kipya unaopigwa na kompyuta tutawapata akina Shaaban Yohana Wanted wengine kweli?

    ReplyDelete
  5. hivi alikuwa akikukimbia wewe au ? (joke)

    anon wa 2:45 A.M. sahau kuwapata wakina shaban wanted wengine na hili wimbi la bongo fleva. bongo fleva inatengenezwa na waimbaji sio wanamuziki.

    mkuu mwakitime chonde chonde wasiliana na huyu jamaa aje kwenye tamasha la raizoni. this guy got talent. tunam-miss sana mwambie.

    ReplyDelete
  6. Danstan15:26

    Ndugu wachangiaji hapo juu,

    Napenda kukubaliana nanyi kuwa, kwa style yake Shaaban Wanted, alikuwa analeta burudani sana ya muziki. Na nyimbo alizopiga, solo lake, ama hakika, lilizifanya zinoge sana. Sikiliza Aza ya Vijana Jazz....ni habari nzito!!!.

    Lakini nakubaliana sana na Bwana Kitime kwamba, sio rahisi kusema fulani ni mkali sana wa kupiga solo gitaa kuliko fulani. Kila mmoja kwa style anayopiga na hisia anazoweka, anawateka watu kwa namna yake.

    Ukiwatazama wapigaji kwa macho, utaona wengine wanatembeze vidole katika mpini mzima wa gitaa, kama Diblo na Alain Makaba, Miraji Shakashia, n.k. Hii haimaanishi kuwa wao ni wakali sana kuliko Dally Kimoko ambae huchezea nyuzi sehemu ndogo ya gitaa lakini kwa ustadi mkubwa. Kila mmoja ni mpigaji wa style yake na kila mmoja analeta burudani ya aina yake.

    Hata ukileta shindano la mpigaji bora wa gitaa lolote leo, sio rahisi kuamua nani mshindi unless kigezo kiwe nani kashangiliwa sana. Na huyu atakuwa ni yule aliyeweka mbwembwe akaonekana na mashabiki.

    Kwa hiyo mie binafsi nawaheshimu wapigaji wote kwa style zao.

    ReplyDelete
  7. Anonymous16:26

    Kitime pole pole kwa mwendo huu unazidi kututia uchungu. Dozi bin Dozi!

    ReplyDelete
  8. Anonymous20:54

    Kitu kilichomfanya Wanted aonekane tofauti na wapiga solo wengine ni staili yake ya upigaji wa kasi wa gitaa ambayo ilikuwa haijazoeleka masikioni mwa wapenzi wa muziki wa Tanzania enzi hizo. Wapiga solo wengi wakati huo walikuwa wamejikita katika staili ya Luambo iliyoletwa hapa nchini na Mose se Sengo ‘Fan Fan’ mwishoni mwa miaka ya 70. Hii ndio staili aliokuwa akipiga Hamza Kalala alipoondoka Vijana Jazz mwaka 1987. Wengine waliokuwa wakipiga mtindo huu ni watu kama Nguza Viking na Batii Osenga. Kama si staili ya Luambo basi ilikuwa ni mirindimo ya magitaa ya nyuzi 12 kwa kufuata nyayo ya Freddy Ndala Kasheba. Wanted alikuja na staili tofauti kabisa akiwa na Tancut Almasi ambayo aliiendeleza Vijana Jazz na hatimaye Ngorongoro Heroes.

    ReplyDelete
  9. Anonymous22:34

    Balozi Kitime, wewe ni mwanamuziki mkongwe ila napingana na wewe katika kutetea wapiga solo wengine ambao hawana jipya. Kumbuka, solo ni lile lile linalopigwa na hawa wote waliotajwa humu, ila tatizo linakuja katika utundu wa kubuni mtindo wa kupiga ili wimbo ule unaopigwa unoge. Mfano, Angalia ule wimbo wa Asha Mwana Seif wa Msondo. Ule wimbo ni mzuri ila solo lake la miaka ya 70 siyo 80's. Na wimbo ule ule angepiga Shube solo wote humu ndani tungelia kwa utundu wa Shube. Hawa wote uliowataja humu ndani ni wazuri ila walipitwa na wakati. Huku Kinshasa ni nadra sana kuona mpiga solo anakaa bendi moja kwa miaka 10, nakuambia lazima tu atatemwa ili aje mwingine na utundu tofauti. Ebu tumuangaliae Shakashia kwanza. Yeye alipokuwa Vijana pale mwanzoni kweli alistahili kuitwa C.I.D. kwa umahiri wake hasa katika nyimbo za 'Kapu la Mjanja,' Mshenga,' 'Mzinga,' 'Chivalavala.' pamoja na nyinginezo nyingi tu zilizomfanya watu wamgombanie, jamaa akaishiwa akaondoka, aliporudi hakuwa tena yule yule. kaenda Twanga kidogo anajitahidi lakini si kama yule wa zamani. balozi, upigaji ni utundu na ubunifu wa hali ya juu. katika miaka yote ninayosikiliza msondo, sijawahi kusikia solo zuri la mabera ama hata Pangamawe. mabera alitamba miaka ya 70 na solo zuri alilopiga miaka ile ni katika ule wimbo wa 'Nasikitika Kijana' sikilizeni ule wimbo na ulinganishe na mapigo mingine ya mabera muone kama nadanganya.

    ReplyDelete
  10. Anonymous22:41

    Bw. balozi ni kweli Wanted hana mpinzani TZ. Kuna mdau hapo juu ametaja baadhi ya wakali wa solo lakini hakuna anayemfikia Wanted, no ONE. Mimi kama Mtanzania na mpenzi wa muziki nakubaliana na huyu jamaa wa Kinshasa kuwa upigaji ni utundu na ubunifu wa hali ya juu. Sikiliza hizo nyimbo alizozitaja huyo mdau ambazo C.I.D. Shakashia alipiga akiwa Vijana na hizi za sasa apigazo Twanga, kweli hana jipya. Shaban alikuwa mtundu sana kwa ukung'utaji wake, yaani tuseme alikuwa na kichwa cha computer, kwa TZ ni Shaaban na Michael Vincent tu, hakuna mwingine. japo Michael Vincent alikuwa anatumia staili yake lakini ukisikiliza Chakachua, ndipo utajiju...jamani sikilizeni 'mtoto wa mjomba' na lile solo lilivyolia yaani hakuna mfano. balozi, nadanganya hapa?

    ReplyDelete
  11. Anonymous22:44

    Balozi Kitime, kama kungekuwa na uwezo wa kukutumia kuku wa plastiki (wa huku Ulaya) kwa njia ya fax, aisee ningefanya hivyo kwako. haki ya Mungu wewe si mtu bali ni mtume wetu, yaani unatufurahisha basi tu. Hivi hawa waandishi wa habari wanafanya nini huko TZ? Yaani wanashindwa kuenzi miziki yetu kweli? Kweli kwenye miti mingi hakuna wajenzi.

    ReplyDelete
  12. Anonymous22:48

    Ombi: Hivi kuna uwezekano wa wewe Balozi Kitime, Wanted, Shaweji, Professor Pembe, Ndula, Mawazo Hunja, na wasanii wengine waliopitia sagha Rhumba kukutana na kuunda bendi yenu?

    ReplyDelete
  13. Anonymous22:52

    Mimi nashangazwa sana na watanzania wenzangu mpaka leo hii. Ninabishana nao kwa sababu nawaambia kuwa kasheba (Ndala Kasheba) hakuwa mpigaji solo mzuri. nakubali alikuwa na staili yake, lakini katika staili hiyo hiyo lazima wewe mpigaji uwe na mbinu za ubunifu kitu ambacho Kasheba alikuwa hana. Nani anaweza kunitajia wimbo wowote wa kasheba ambao utaweza kucheza kama ukipigwa disco, jibu hakuna. Yeye alipata ujiko tu kwa kuwa na lile solo lakini alikuwa hana jipya. Alizidiwa na Kina Mulenga, Kamaley, Mfalme Nguza, Bati Osenga, Fan Fan, Mze Abel, na Mabera lakini watu umuita supreme, for what?

    ReplyDelete
  14. Anonymous23:02

    Wanted ni Tishio la Afrika, siyo TZ pekee!

    ReplyDelete
  15. Anonymous23:02

    Balozi, hapa umechemsha kidogo. Upigaji bwana ni utundu na ubunifu wa mtu na ni kitu ambacho Wanted alibarikiwa nacho. Sisemi kama hao uliowataja ni wabovu, lahasha.....ila hawana jipya. Nisikilizie hizi nyimbo 'Mke Mkubwa', 'Lumbesa,' 'Mtatumaliza', na 'Mama Kidude' katika ile albam ya Lumbesa. Bwana, wanted ni kitu kingine aisee....msipimeeeee ni dhambi, yule apimiki.

    ReplyDelete
  16. HII NDO RAHA YA MUZIKI. MTU ANAWEZA KUPENDA AINA FULANI YA MUZIKI NA KUTOTAKA KUSIKIA JINGINE LOLOTE. HASARA YA UPENZIWA AINA HII NI KUWA HUIPI NAFSI YAKO NAFASI YA KUTAFAKARI MUZIKI MWINGINE WOWOTE. BADO NAJIULIZA HUU UTUNDU AMBAYO WANTED ALIKUWA NAO LAKINI WAPIGAJI WENGINE HAWANA NI UPI HUO? AU NIULIZE KATI YA FRANCO, DR NICO, KINZUNGA, MPIGA SOLO WA KIAM, WA BELABELA, WA LIPUALIPUA , JOHNNY BOKELO NANI ALIKUWA NA HUO 'UTUNDU' UNAOTAJWA HAPA?

    ReplyDelete
  17. Anonymous02:09

    Ama kwa hakika hii inatia raha sana hasa ukisikiliza debate za muziki uliokonga mioyo enzi zetu kwa maana enzi hizo hakukuwa na forum za namna hii! Nakubaliana na John kwamba magita hupigwa kwa staili tofauti kutokana na ama mirindimo iliyotokana na watunzi wa nyimbo au 'touching' ya mpiga gita mwenyewe, na vilevile mtindo wa bendi yenyewe.
    Kaya yetu imepata kuwa na wapigaji wengi wa gita la solo tangu enzi za akina Michael Vicent na Juma Ubao kama John alivyoainisha hata kufikia kina Wanted, Shaaban Dogodogo(RIP), Pangamawe, Kassim Rashid "Kinzunga" na Shakashia.
    Nilibahatika kuwa karibu na wapiga magita wengi wa kuanzia miaka ya 80 kuanzia Mulenga, Mabela, Hamza kalala, Dekula, wanted, Kibambe, Robert Tumaini, Khalfan Uvuruge(RIP) pamoja na ndugu zake ambao mara nyingi walikuwa wanapiga rythm katika bendi walizopitia "Sikinde, OSS, Afriso na Msondo" ukiacha kaka yao Jumannne (RIP). Naweza kutaja wengi tu kwani hata Shakashia wakati anaingia vijana toka MK Group tulikuwa tunashinda nyumbani kwangu tukijaribu 'kukopi' Jazz za George Benson na Earl Klugh kuboresha skills zetu.
    Kitime you made a very good point kwamba "Magitaa hupigwa kwa staili tofauti. gitaa la Michael Enoch ni tofauti na la Michael Vicent, na tofauti na la Juma Ubao, utalinganishaje?" Hiyo ita apply kwa mipambanisho mingi ya ma soliste, Lakini Shaaban Yohana ni mpiga gita ambaye alibobea kufunika staili nyingi...alipiga style ya Lwambo maarufu kama 'Kent' ambayo unashika nyuzi mbili ya kwanza na ya nne yake na kuleta sauti tamu mno! Sikiliza kipande cha katikati cha wimbo wa 'Theresa' au solo la Kalala kwenye 'Tambiko la Pambamoto". Hata Madilu alipotembelea Bongo mwanzoni mwa miaka ya tisini alimfananisha Shaaban na wacongo pale nyumbani kwa Kanku kelly baada ya Wanted kupiga kwa ufasaha wimbo wa 'Ya Jean'.
    Vile Wanted alipiga staili za kina Dally na Diblo ukiachilia skills zake katika Jazz kwani alipopiga wimbo wa Samba pati wa Santana utafiri ni orijino, ama extra ball ya Diblo pale Ngorongoro Heroes ungedhani ni Diblo mwenyewe.
    Nimetoa maelezo meeengi lakini ninachojaribu kusema kwa Bw. Kitime ni kwamba Shaaban yuko kwenye category ya kupambanishwa na wapigaji magita wa styles tofauti bongo.
    Kwa manitiki hiyo nakubaliana na waliotangulia kusema kwamba ndiye mpiga solo bora katika historia ya wapiga solo wa ka nchi ketu kadogo!

    ReplyDelete
  18. Anonymous13:47

    Kwa maoni yangu mpiga solo aliyekuwa anaelekea kumkaribia Wanted, japo kwa mbali, ni marehemu Shaaban Athumani 'Dogo Dogo', ambaye pia alijulikana kama 'Luxury'. Huyu alikuwa ni moto wa kuotea mbali katika muda mfupi aliyokaa na Kurugenzi Jazz ya Arusha mwanzoni mwa miaka ya tisini. Ukisikiliza solo lake katika vibao vya Kurugenzi kama 'Emmy' utakubaliana nami. Baadae alijiunga na Vijana Jazz ambako hakukaa sana kabla ya kutimkia Nairobi alikofariki dunia miaka michache iliyopita. Sikumbiki vizuri ni nyimbo gani za Vijana ambamo solo lake linasikika, labda Balozi Kitime atukumbushe.

    ReplyDelete
  19. Shabaan Dogodogo alishiriki album nzima ya VIP, ambayo kama nilivyotoa maelezo humu ndani kabla arrangement yake ilikuwa kulipigwa solo gitaa mbili katika wimbo mmoja. Hivyo Wanted na Dogodogo walipiga sana, ila katika wimbo niliotunga Mfitini ndio Dogodogo alipiga solo linaliosikika humo. Agreed alikuwa mkali amekufa mapema mno

    ReplyDelete
  20. Anonymous15:34

    haiwezekani kulinganisha wasanii mahiri ukampata mshindi hivi nikakuuliza kati ya Bob Marley na Michael Jackson yupi anayeimba vizuri zaidi ya mwingine utapata jawabu gani?

    ReplyDelete
  21. Anonymous20:04

    balozi, utundu wa wanted ni kubuni mbinu ama njia ya mirindimo tofauti ya kulinyanyasa solo lake. katika hao wapiga solo uliowataja wewe hapo juu ni djuke pekeeyule wa kiam ndiye solo lake linafanana sana na la wanted. balozi, narudia tena....hapa kini (kinshasa) Franco hatambi ama alikuwa hatambi kama nyie mnavyofikiria huko TZ, yeye alikuwa tu mtu wa kawaida na muziki wake ulipendwa sana afrika ya mashariki na sio huku, why I dont know. Franco yeye anatambuliwa kuwa ndiye mmoja wa ma-pioneers wa muziki wa zaire pamoja na kina Ya Papa wendo, Bowane, Edou Elenga, na dk. Nico bila kumsahau Pascal (tabu ley). watu waliopenda sana muziki wa franco wengi walikuwa ni viongozi wa serikali na watu wenye matabaka ya juu kwani mara nyingi alikuwa (franco) anamsema mobutu na nyimbo nyingi za kumsema ama kumsakama mobutu au kiongozi wa serikali alikuwa anapewa na baadhi ya viongozi ili awaseme hao walengwa. na ndiyo maana nyimbo za franco alikuwa anapiga kwa staili ya jazz ama blues ili mtu ukae kwenye baa na kutafakari. Baadaye ama tuseme katika miaka yake ya mwishoni alihamua kutumia mapigo ya haraka ili kwenda na wakati, na alianza kutumia mtindo huu pale mwaka 1986 katika ile albam ya Boma ngai na boma yo, tobomana (Nipige nikupige, tupigane). pale franco alimuachia kijana Jerry Dialungana (RIP) katika solo huku yeye akipiga second solo.

    hao kina dr. nico, bokelo, na wengin uliowataja walitamba miaka ya zamani ile 1960's na hawakubadilika jinsi miaka ilivyoenda, hivyo naweza kusema kuwa hawakuwa na lolote jipya na ndiyo maana waliishia tu.

    ReplyDelete
  22. Anonymous20:31

    Ndimi mwana Kini (Kinshasa). Nataka nikuambie kitu kimoja balozi pamoja na wachangiaji wote humu, nimegundua kitu kimoja huko TZ. Mnajuwa wanamuziki wengi wa huku Kini(ondoa hawa lika la kina Mpiana na wenge) huku hawana sifa, na utakuta wakiishiwa ndipo wanakuja ama kuhamia nchi za afrika mashariki kutafuta ajira. nakumbuka siku moja nilikwenda kwenye concert ya zaiko pale kipwanza bar baada ya zaiko kugawanyika. watu wengi walidhania kuwa ndiyo mwisho wa zaiko maana wapiga solo wao hatari beniko popolipo, jimmy yaba, na petit poisson waliondoka pamoja na waimbaji na watunzi wa kutegemewa kama kina lengos, ya ombale, na ya jp buse. basi bwana pale zaiko ilikuja upya kwa kuchukua vijana wa hajabu. waliwapata wapiga solo wengine kama shiro mvuemba, baroza, na wengineo wengi tu ambao ilifanya zaiko kuwa moto wa mbali na kuwa bendi bora mwaka ule. sasa basi ile siku bwana, vilipopigwa vigongo ama nyimbo za zamani zilizopigwa na wale wapiga solo walio ondoka, baroza ambaye ndiye alikuwa mpiga solo mpya alibadilisha ile mitindo na kupiga kipeke kabisa mpaka kufanya watu waseme bora wale waliondoka, hawa ndio wapigaji tunaowataka zaiko (maneno ya mashabiki hayo). Nono atalaku (yule repa wao) kwa jinsi alivyokolezwa na lile gitaa la baroza alisikika akisema 'barozaaaaaa, tika kolela mwana ya Mama! bakoki pe kokende na nairobi...ah mawa trop!'

    Maana yake: baroza mtoto wa mama acha kuliza hilo gitaa, wameishiwa hao na ndiyo maana wameenda nairobi, ah shida tupu!

    kwa hiyo bwana balozi utundu na ubunifu wa mpiga solo ni muhimu sana. na ndiyo maaana baroza alipokuja zaiko alibadilisha ile mirindimo ya zamani na kuja na kitu kipya mpaka mashabiki wakamtukuza na kumuita 'le roi lion.' yaani ni lion king (mfalme simba), kaja watu wametimka na kwenda kenya. vituko hivyo.

    ReplyDelete
  23. Anonymous21:56

    Kwa kweli John yoote yamesemwa na wachangiaji wengi wenye mtazamo na ladha tofauti. Ninakubaliana sana na maoni na mitazamo yao. Lakini nitofautiane nao kwa jambo moja. Ni kweli Shaaban Yohana alikuwa ni mpiga solo mahiri kwa wakati wake na nyakati zile. Itakuwa sii sawa sana kuweza kumlinganisha na wapiga solo wengine mahiri ambao nao walifanya vizuri sana katika nyakati hizo. Ninahakika kama tungeweka mizani wapo wengi ambao kwa kutojitokeza ama kutokuwa maatufu katika nyanja za mitandao nao walifanya kazi nyingi nzuri tena kwa utundu na mirindimo makini kama ya wanted. hebu waeleza wachangaji jinsi unavyopata raha kupiga slo la wimbo wa Ngoma iko huku!!! pana vitu vingi sana ndani ya gita lile. kwa wanaoujua muziki watakubaliana nami ama waje Kilimanjaro band wasikilize na wafananishe

    ReplyDelete
  24. Kuna kambi mbili za upenzi wa muziki, moja hupenda kwa ushabiki na ndio maana kuna kitu kinaitwa popular music, kambi nyingine huangalia umahiri zaidi, technics za upigaji au uimbaji, na hawa wanaweza wakatofautiana na sana, chukua mfano wa Franco, sikiliza upigaji wake katika miaka tofauti, amekuwa na staili tofauti mpaka kifo chake. Na kuna wanamuziki huibuka na kuwa na staili moja tu lakini wakapendwa sana katika kipindi chao. Hivyo kuwepo kwa uchangiaji humu pia kunaonyesha sura hizo mbili za mtizamo wa muziki.

    ReplyDelete
  25. Anonymous12:34

    Huyu bwana namkumbuka sana kwa nyimbo za wana sukuma push..mitwango (ngorongoro heros). pale Ilala Max bar ilikuwa every friday night...nilikuwa silali mpaka niende pale......hasa nyimbo zao kama naachia ngazi, pokea ujumbe, kambwembwe n.k. palikuwa hapatoshi. Yohana (lead guitar), Huruka (rythm), Challenger (bass). sijui John kama ulibahatika kuwaona walikuwa na mziki mzuri sana....ilikuwa miaka 1996-99

    ReplyDelete
  26. Niliwaona ii was a great team, Huruka nilipiga nae Orchestra Mambo Bado, yeye ndo alipiga solo la wimbo ule uliopigwa marufuku, wa Bomoa Tutajenga Kesho. Shaaban nilianza nae Tancut na kisha Vijana na hivyo ilikuwa muhimu kwenda kuona mambo gani wametayarisha. Bendi ile ilikuwa doomed kufa. Mwanasiasa mmoja ndie alietumia juhudi kuianzisha na kuifadhili. Ilianza kwa lengo la kwenda kupiga nje ya nchi, hiyo ndo ahadi waliopewa akina Wanted, baadae wakaambiwa wanaenda kusaidia kampeni za mwana siasa huyo huko mkoa wa Mwanza 1995 wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu. Nilipokutana na Wanted Mwanza nilimueleza kampeni ikiisha mwanasiasa hana haja nanyi atawatosa, kwani akishinda hana haja na nyinyi, akishindwa hana haja na nyinyi, na ndio kilichotokea , hawa kwenda nje wala hawakuendelea muda mrefu

    ReplyDelete
  27. Maabadi17:13

    Well said John, siku za Ngorongoro Heroes zilikuwa zimehesabiwa coz ilianzishwa kwa msisimko lakini kwa mission ya muda mfupi sana.
    Siku moja nilimsikia marehemu Aggrey Ndumbalo akisema hivyo pia pale kinondoni sikuweza kupambanua haraka, lakini baada ya muda si mrefu sana nikatambua kwa nini alisema vile.
    Ufa mkubwa ulionekana baada ya ahadi kutotimilika...Wanted(Solo), Abdallah Dogodogo(Bass), Thadeo Mkama(kinanda), Muharami Seseme(drums) waliungana na Kinguti kwenda Botswana na kuiacha Ngorongoro kubaki na ukiwa.
    Kama si umahiri wa mpiga solo Lovelace Maradufu (Omary Seseme) ambaye aliweza kuikamata vizuri program yote ya Wanted, Ingekuwa ndio mwisho wa bendi. Lakini kuwepo kwa safu ileile ya waimbaji na Omary Seseme kulisaidia ku stabilize bendi japo kwa muda mfupi.
    Huruka Uvuruge alitumia busara sana kurudi Sikinde kabla yote haya hayajatokea maana alishaona mbele...Omary Seseme akajaza nafasi yake ambapo baadaye ndiye akawa mpiga solo baada ya kundi lilioondoka. Aliniita Ngorongoro kipindi hicho tukawa na Jumanne Zumba kwenye rythm, John Mwalyanga kwenye bass, Andrew Sekedia kwenye kinanda huku safu ya waimbaji ikiwa ileile (Kasaloo Kyanga, Kyanga Songa, Kalondji Matutu na Skassy Kassambula).
    Ntakudondoshea taswira za wakati huo kaka....

    ReplyDelete
  28. Anonymous20:46

    sasa wewe anon wa April 21, 2010 5:34 AM, hivi hata wewe mwenyewe ukikaa chini na kutafakari haya uyasemayo unapata jibu kweli? Swali unaloulizia hapa ni sawa tu na kumchukua Mze Yusuf kumlinganisha na Bitchuka, inakuja kweli kichwani mwako? Bob mi mpigaji reggae na ni muimbaji reggae, na lil solo lake inabidi ipigwe mitindo ya reggae, siyo? Marehemu michael ni muimnaji wa pop music na hapigi chombo chochote kile katika music labda manyanga tu amabayo alikuwa anatumia enzi zile za jackson 5. Bob marley anafananishwa na kina peter tosh na jimmy cliff na wengineo. michael anafananishwa na kina lionel ritchie, cool and the gang, na wengineo. nakubaliana moja kwa moja na huyo mdau wa kinshasa na wengineo kuwa upigaji wa solo unahitaji utundu sana na ni kitu ambacho wanted alikuwa nacho. jamani sikilizeni sukuma push....mtajiju!

    ReplyDelete
  29. Anonymous01:57

    Katika solo au lead guitar tusimsahau Rashidi Hanzuruni aliyekuwa Western Jazz miaka ya 60. Ukiweza hebu sikiza wimbo wa Western Jazz "unionapo nikiandamana, sio kama nafuata bendera, naipenda kweli nchi yangu, shika moyo utakueleza, twende haya twende..." Rashidi Hanzuruni pia alikuwa anapigaa hawaiian guitar. Pamoja na kuwa na sauti nzuri, Mbaraka Mwinshehe alikuwa ni "guitar master". Mwenyezi Mungu awalaze wote katika amani. Amin.

    ReplyDelete
  30. Anonymous02:07

    sukama eh sukuma, yeee mitwangwo!

    ReplyDelete
  31. Perez14:52

    Nyie wote mnaobishana hapo hebu kasikilizeni KASHEBA na NGUZA wanavyoongea kwa masolo gitaa katika wimbo wa "Mama Mariaa twakutakia kila la kheri mamaa..."

    ReplyDelete
  32. Balantanda21:03

    John,hivi yuko wapi huyu mheshimiwa?,jamaa alikuwa anatisha hasa...Nakumbuka alivyoondoka Vijana pengo lake likazibwa na Miraji Shakashia(Shaka Zulu wa Twanga Pepeta) kipindi hicho kijana mdogo,Shakashia akapewa jina la CID(kwamba anamtafuta Yohana ambaye ni Wanted...hahaaaaaaaaaaa)

    Mara ya mwisho nilimsikia akiwa katika bendi ya Ngorongoro Heroes wana Sukuma Push,alikuwa na Skassy Kasambula,sijazisikia tena habari zake baada ya bendi ya Ngorongoro kufa

    Yuko wapi sasa huyu bwana?

    Balantanda

    ReplyDelete
  33. Anonymous04:57

    Hivi we Perez kichwani zimetulia kweli? Sasa kasheba ana solo gani? Yeye alipata tu ujiko kupiga lile gitaa la nyuzi kumi na mbili lakini huwezi kucheza solo lake, yaani aliishiwa. hakuna solo lolote alilopiga Safari Sound wala Zaita ambalo mtu unaweza kucheza. labda kidogo ule wimbo wa Kesi Ya Khanga. Ila Big sound 'Nguza' yeye simpingi. Kweli Nguza anastahili sifa pamoja na fan Fan na bati Osenga kwa kipindi kile. Kwa Wanted....ahhhhhh, yule apimiki, ni dhambi kumpima!

    ReplyDelete
  34. Anonymous00:27

    Ngorongoro Heroes walipiga kambi Bahama Mama chini ya Juma Mbizo.
    Mitwango sukuma, wanted alikuwa ni mtundu sana kwenye solo.

    ReplyDelete
  35. Anonymous02:31

    tusitake kukwepesha ukweli! wanted ni hatari sana si tz hata afrika..mfananisheni na diblo. ila kitime kwasasahivi sijaona mpiga solo anaeweza mfikia pangamawe wa msondo. yule jamaa ni hatari..sidhan ka yupo wakumfilia kwa sasa

    ReplyDelete

SAFARI ZANGU NA BENDI sehemu ya kwanza.

  TANCUT ALMASI ORCHESTRA  wakiwa Jamhuri Stadium Dodoma   Sikumbuki ni safari ngapi za kimuziki nilizowahi kuzifanya hapa nchini katika m...