YOUTUBE PLAYLIST

Friday, April 23, 2010

Bendi za Mkoa wa Morogoro

Kati ya mikoa iliyokuwa na Bendi nyingi, sijui kama ulikuweko ulioushinda mkoa wa Morogoro. Ilikuwa kila wilaya ina bendi. Baadhi ya bendi ninazozikumbuka ni Morogoro Jazz, Super Volcano, Cuban Marimba Band, Les Cuban, TK Limpopo, Kilosa Jazz (alikotokea Abel Balthazar), Ifakara Jazz, Sukari Jazz, Imalinyi Jazz, Mahenge Jazz, Kwiro Jazz., Mzinga Troupe. Na hata wale wakali wa wakati huo na ule wimbo wao enye maneno,

Waache waseme watachoka wao,

Mzee Makelo endeleza libeneke,

Waache waseme watachoka wao,

mtindo libeneke unatia fora

Hapa naongelea Butiama Jazz Band, iliyokuwa inapiga muziki kwa mtindo wao uliotokana na ngoma ya kwao Libeneke,wao ni wa Ifakara hivyo nao ni bendi ya mkoa wa Morogoro japo jina lilitokana na mahala alipozaliwa Baba wa Taifa.(Mzee Mkwega aliyekuwa mwenye bendi alikuwa kada mzuri sana wa CCM, hata kifo chake kilimkuta akiwa mtumishi wa CCM ofisi ndogo Dar es Salaam).

Mpaka leo ukienda Ifakara wakati wa msimu wa mavuno ikiwa kuna sherehe za jumla kama vile kipaimara, ndo utajua wanavyopenda ngoma. Kuna vikundi vingi vya ngoma ya Sangula na kila kikundi kimejipa jina la Bendi, hivyo utakuta mabango yakitangaza Tancut Almasi, Msondo, Super Volcano, na kila nyumba yenye sherehe huandaa kundi lake ni raha tupu hapo

2 comments:

  1. Anonymous11:53

    MAMBO YAENDA YAKIONGEZEKA! HEBU MKUMBUSHE KAKA KEPI MAMBO YA MZINGA TPOUPE NA KALE KA-WIMBO 'UBAHARIA....UTAKUPONZA....'

    ReplyDelete
  2. Nimempigia simu kasema mtunzi alikuwa mpiga solo marehemu Kipanga, pia kumbuka kakake Keppy ,Ndoki Kiombile alikua nae akipiga solo bendi hiyo.

    ReplyDelete

SAFARI ZANGU NA BENDI sehemu ya kwanza.

  TANCUT ALMASI ORCHESTRA  wakiwa Jamhuri Stadium Dodoma   Sikumbuki ni safari ngapi za kimuziki nilizowahi kuzifanya hapa nchini katika m...