Jukwaa la wapenzi wa mambo ya muziki wa Tanzania-

Breaking

Tuesday, March 9, 2010

Vijana Jazz Baada ya Maneti

Ushindani uliokuwepo kati ya Maquis Original na Vijana Jazz ulikuwa mkali sana mwanzoni mwa miaka ya tisini hasa kwa ajili ya siku ya Jumapili ambapo Vijana walikuwa Vijana Kinondoni, wakati Maquis wakiwa kwenye ukumbi wao wa Lang’ata Kinondoni. Muda wa maonyesho yote mawili ulikuwa uleule hivyo kila kundi lilikuwa linatafuta kila njia ya kumpiku mwenziwe.

Vijana Jazz iliamua kupata wanamuziki wengine wapya. Hapo akaingia Suleiman Mbwebwe toka Sikinde,Jerry Nashon toka BIMA, Benno Villa kutoka Sikinde lakini wakati huo akitokea Nairobi, Rahma Shally kutoka Sambulumaa, wote hao waimbaji. Shaaban Dogodogo akitokea Nairobi (solo gitaa), Mhando (keyboards), Ally Jamwaka toka Sikinde (tumba).

Hapo ndipo ilipoanza Pambamoto Saga Rhumba.

Ujio wa TP Ok jazz ulibadilisha sana mtizamo wa bendi kimziki. Ok Jazz , wakiwemo wakongwe wote kasoro Franco, maana hii ilikuwa baada ya kifo chake. Ingawaje walikuja na kijana mmoja ambae alikuwa anaimba kama Franco pia alikuwa anapiga gittaa kama Franco , walikuja na mtindo wa kuweko kwa magitaa mawili ya solo, tofauti na kawaida iliyokuweko ya kuweko second solo. Tofauti yake ni kuwa katika mfumo wa OK jazz, wapiga solo wote wawili walikuwa mahiri na magitaa yalipewa uzito sawa. Katika mfumo wa second solo, gitaa hili huwa linasindikiza tu solo gitaa. Kwa kutumia mfumo huu, recording maarufu ya VIP ilirekodiwa katika studio za TFC. Mzee John Ndumbalo fundi mitambo mwenye uwezo mkubwa ambao bahati mbaya kama yalivyo mambo mengi mazuri ya zamani ya Tanzania umetupwa na kusahaulika. Aliirekodi album hiyo. Iliyojaa nyimbo ambazo zina kumbukwa mpaka leo, Thereza (Jerry Nashon), VIP (Jerry Nashon), Bahari imechafuka (Benno Villa), Mfitini (John Kitime). Sauti za waimbaji humo akiwemo Jerry Nashon , Benno Villa Anthony, Said Hamisi, Freddy Benjamin,Abdallah Mgonahazelu, Mohammed Gotagota Suleiman Mbwebwe zilileta burudani kubwa wakati huo.

Wapiga magitaa wa Vijana Jazz chini ya Shaaban Yohana (Wanted), walikuwa Shaaban Dogodogo Solo,Agrey Ndumbalo Rhythm, Bakari Semhando na Manitu Musa Bass, hapo ilikuwa utamu kolea………………Picha ya juu Madiluu System kushoto kwake Baker Semhando mpiga Bass wa Vijana Jazz. Chini kushoto Mohamed Gota gota, chini Agrey Ndumbalo

10 comments:

Anonymous said...

John!
Tumekukosa nasa leo kwenye semina elekezi ua TBL maalum kwaajili ya kilimanjaro music award. Hata bendi yako haikutuma muwakilishi coz najua hizi sii anga zenu.
Nimefurahi pia kujua kwamna wewe ndiye mtunzi wa wimbo wa "mfitini"
Sasa John hivi wimbo huo ni mali ya nani?? uliweza kunufaika vipi na tungo hito pamoja na nyingine kama nyongise na hata zile ulizotunga na wana njenje japo najua kwamba kwa sasa mko makini?
kila la kheri kwenye safari yako na mwenyezi munguakutangulie

John F Kitime said...

Sidhani kama ningekuja hata kama ningekuweko,kuna vitu sivielewi elewi. niulize hivi TBL wakidhamini ligi ya mpira wa miguu nao wanakuwemo katika kamati ? au wanawaachia wataalamu wa mpira waendeshe unavyotakiwa?

John F Kitime said...

Mfitini ni mali yangu na bendi, wakati natunga nilikuwa nalipwa mshahara na umoja wa vijana nikatumia vyombo vyao, wasanii ambao waliwalipa wao na hata studio ililipa bendi.

Anonymous said...

JFK huyu Cosmas Chidumule alishaimbia Vijana Jazz au sauti zafanana, maana naona kama sauti yake haijapata mtu wa kuiga na sidhani.
na hii ndoa kuvumiliana kuna sauti za nani na nani wanoongoza hapo, hii ya kwanza kama yako vile.

John F Kitime said...

Chidumule alishawahi kuimbia Vijana nadhani sauti unayofananisha na yangu ni ya George Mpupua

Anonymous said...

Mwaka 1981, Maneti alitua Nairobi ambapo alishirikiana na Charles Ray Kasembe kutoa kibao kiitwacho Stella. Kasembe wakati huo alikuwa anaongoza bendi ya Les Volcano iliyokuwa na makao yake jijini Nairobi. Kasembe alikuwa ni mpiga rhythm wa Mbaraka Mwinshehe Mwaruka na aliamua kubaki Nairobi na kuunda bendi yake baada ya Mbaraka kufariki. Wanamuziki wote hawa wameshatangulia mbele ya haki.

Anonymous said...

Hivi Shabani dogodogo hakuwa Mpiga bass John?

Anonymous said...

John, Kamwene mnyalukolo, hivi Mohamed Gotagota yupo wapi mkwamisi uyu? Na unaonaje miziki ya wakati wenu na wakati huu?

John Mwakitime said...

Mohamed Gotagota alifariki miaka mingi iliyopita.Mungu amlaze pema peponi

John Mwakitime said...

Shaaban Dogodogo alikuwa mpiga solo rythm na second solo mahiri sana, na aliwahi kupigia Vijana Jazz na alishiriki katika album ya VIP. Abdallah Dogodogo ndiye alikuwa mpiga bass alikuwa Ngorongoro Heroes kabla ya kuondoka na Shaban Wanted kwenda Botswana

Adbox