YOUTUBE PLAYLIST

Friday, March 5, 2010

Patrick Pama Balisidya


Jina Patrick Balisdya halitakuwa geni kabisa kwa wadau wa blog hii,lazima roho zimeanza kuwadunda kama inavyokuwa kwangu kila nikimkumbuka Blai. Patrick Pama Balisidya alizaliwa Mvumi Dodoma tarehe 18 April 1946. Kabila lake alikuwa Mgogo , kabila ambalo lina wanamuziki wengi maarufu kutokana na muziki kuwa sehemu muhimu ya maisha ya kabila hilo. Mama yake alikuwa anapiga kinanda kanisani na hivyo basi kutokana na asili ya kabila lake na pia kutokana na mama yake, hakika huyu angeweza kujisifu kuwa muziki uko katika damu yake.

Mdau mmoja alitutaarifu kuwa Balisidya alikuwa kiongozi wa Bendi ya shuleni kwake Dodoma secondary School. Ambapo kutoka hapo alijiunga na Chuo cha Ufundi , na baada ya kumaliza mafunzo alifanya kazi hiyo kwa muda na 1967 akawa tayari anapiga muziki Dar Es Salaam Jazz B. Kufikia mwaka 1970 Patrick alikuwa ameanzisha kikosi chake mwenyewe Afro70, kikiwa na mtindo wake Afrosa. Alikuwa mbunifu katika muziki wake, na kwa muda mrefu alikwepa sana kuingia katika wimbi la kufuata mapigo ya Kikongo kitu ambacho hata wakati huo bendi nyingi zilikifanya, japokuwa kukutana na Franco wakati alipofanya moja ya ziara zake nchini humu kulimfanya abadili mtindo kwa kipindi kifupi na katika nyimbo moja wapo aliiga kabisa solo la Franco alilolipiga kwenye wimbo wake Georgette.

Afro70 iliwakilisha wanamuziki wa Tanzania katika maonyesho ya mtu mweusi Lagos,Nigeria. (FESTAC festival 1977). Vyombo alivyotumia katika maonyesho haya vilimsumbua akili mpaka alipofariki, kwani muda mchache kabla ya Festac, wakati huo serikali ikiwa imeshamtaarifu kuwa ndie atakuwa mwakilishi wa Tanzania, vyombo vyake vyote vilihalibika katika ajali ya gari. Serikali ilinunua vyombo vipya ambavyo siku zote Balisdya alisema aliambiwa ni vyake baada ya maonyesho. Aliporudi kutoka Nigeria Kiongozi mwingine wa serikali aliamuru vyombo virudishwe serikalini na kwa kitendo kile kutangaza kifo cha Afro70. Vyombo hivyo vilitumika kuanzisha bendi ya Asilia Jazz ambayo ilikuwa Bendi ya Wizara ya Utamaduni na Vijana. Balisdya alitumia muda mwingi kujaribu kudai haki yake hiyo ambayo ilimkwepa mpaka mwisho wa maisha.

Mwaka 1979, Balisidya alikwenda Sweden na kushirikiana na kikundi cha Archimedes akatoa album nzuri sana iliyoitwa Bado Kidogo. Kuna wakati Patrick alijiunga na Orchestre Safari Sound, (masantula) na kupiga piano katika ule wimbo maarufu, ‘Unambie siri’, Patrick pia alikuwa mpigaji mahiri wa keyboards. Kwa kweli nyimbo za Patrick zilizokuwa juu katika chati ni nyingi. Harusi, Dirishani, Weekend, Tausi, Pesa, Nakupenda kama Lulu, Ni masahaka na mahangaiko, Afrika.

Patrick alifariki tarehe 7, Agosti 2004.

Daima tutakukumbuka Patrick Pama Balisidya,

Mungu akulaze pema peponi

23 comments:

  1. Anonymous00:10

    John
    kabla sijaingia kitandani kila siku huwa ni lazima nilog in kwenye blog yako nikiwa na matumaini ya kukuta kitu kizuuuri kama hiki ambacho kina kiwango cha juu. Hua ninakuwa mnyonge sana ninapokosa " maandiko" yako ya ukweli na yenye mpangilio.
    Kwa hili la paty balisidya Blai limekamilisha usiku wangu hasa kwa yaliyonisibu leo. Kuna wimbo wake unaitwa " msijali enyi wapenzi wangu mambo yote yatakuwa sawa" Ni wimbo wenye faraja sana kwangu kila ninapopata tatizo naukumbuka. hapa alikuwa akiwasihi wapenzi wake kwamba ipo siku angerudi kwenye game na hayo yaliyomkuta ni mafunzo kwake ili apate ya kuhadithia. Its a good song and very touching.
    Nipo zanzibar leo na ksho nitakuwa dar kucheza mduara. nasikitika sitakuona . lakini nitakuwa na wewe katika maandiko kama haya. Uwe na ziara njema

    ReplyDelete
  2. Anonymous00:17

    Kitime
    hivi Partick alipata kuwa na familia? maana sijapata kusikia kama kuna hata kijana wake aliyefuata nyendo zake.
    Je Group lao kwa maana Afro70 ukimuacha yeye ambaye ninahakika ni marehemu, Je kunawalio hai? na wanaishi wapi na je bado kwenye ulimwengu wa muziki?
    Je endapo kama mtu atajaaliwa kufanya kumbukumbu ya kumuenzi mwanamuziki huyu nguli je wanaweza kupatikana hata wachache wakatupigia muziki? najua mtu kama Sheby Mbotoni ambaye alikuwa mpiga sax enzi hizo na sasa yuko dodoma bila shaka anaweza kuwa mmoja wapo japo alikuwa akilalamika kwamba Patrick alipata kuwazulumu ujira wao? Sheby yuko sub trasure dodoma na alikuwa mheshimiwa diwani wakati fulani.
    Keep it uo Mwakitime

    ReplyDelete
  3. Hakika alikuwa ni mwimbaji mahiri.....Nina nyimbo zake za "Harusi", "pesa", "Dirishani", "Pesa" na "Ni Mashaka".
    Nyimbo hizi zinakumbusha mbali sana. Shukrani Mdau kwa historia ya mwanamuziki huyu.
    Mdau
    drfaustine.blogspot.com

    ReplyDelete
  4. Nafarijika japo naona nabeba mzigo mzito, ila nitajitahidi.

    ReplyDelete
  5. R.I.P Balisidya !
    Kazi zako bado zatugusa!

    ReplyDelete
  6. Anonymous00:33

    Mkuu,

    Blai! Blai wangu! Blai wangu! Wee acha tu.

    Kabla sijazaliwa Baba yangu alikuwa mwalimu huko Dodoma. Kati ya wanafunzi wake alikuwepo mmoja aliyeitwa Patrick Pama Balisdya. Baba yangu aliniambia Marehemu Patrick alikuwa mwanamuziki tangu alipokuwa mwanafunzi.

    Nilipokuwa mtoto niliskiliza miziki ya Marehemu Patrick. Baadaye huyu kaka akaja kuwa rafiki yangu.

    Ninaweza kusema nina miziki karibu yote ya Afro 70 na mingineyo aliyopiga baadaye na Archimedes na alizorekodi na Global Music Centre, Finland na zile alizorekodi kwenye Music from Tanzania and Zanzibar series.

    Hakuna ubishi Marehemu Patrick alivutiwa na muziki wa Marehemu Franco. Ukisikiliza nyimbo ya Pesa utaafikiana na wenye hoja hii.

    ReplyDelete
  7. Anonymous11:38

    John
    Nimependa sana hii story ya huyu mtu Balisidya, lakini jinsi alivyo na mchango wake wa muziki katika nchi hii na hata mimi binafsi ninavyomfahamu kile ulichotupa ni kidogo sana (kiduchu) lakini sina budi kushukuru kwa kutupa hicho kidogo ni matumaini yangu huko mbele tutashiba.
    Sasa nilikuwa na suala moja naomba unijulishe kwani wewe ni mwanamuziki mkongwe inawezekana kabisa ulikuwa na ukaribu fulani na Marehemu Balisidya, tungo zake nyingi zilikuwa ni kuumizwa katika mapenzi, hii inawezekana ilikuwa inagusa sehemu katika maisha yake?

    Naomba niishie hapo kwa kukupongeza na tunarajia vingi vya wakati uleeee..!

    ReplyDelete
  8. Kuna watunzi ambao tungo zao huelemea upande fulani sasa kila moja kwa sababu yake, wengine aliumia kweli, wengine ni tungo tu. Marehem Kalala Mbwebwe tungo zake nyingi ilikuwa kuachwa na wanawake lakini katika kuishi nae sikusikia akilalamika kuachwa kikweli.

    ReplyDelete
  9. Najua Patrick aliacha binti, na kuna mdogo wake ambae anashughulika na muziki

    ReplyDelete
  10. Anonymous09:01

    Anony wa March 5, 2010 1:10PM. Group la Afro70 wengine wapo kama Stephen Balysidia (Mwimbaji) huwa namuona mitaa ya Masaki, hata Paul Mdashasi (mpiga drums) wa pale Kinondoni. Majority wa band hii walikuwa na shule... Stephen alikuwa bima, Paul ni Mhasibu nadhani bado yupo NBC. Sijui akina Owen Liganga, Montegomery Makanjila, Norman Pingalami sijui wako wapi? kuna mdau anayeweza kujui? atupe kidogo! asante John kwa kutupa forum hii nzuri hasa sisi wenye kuupenda mziki halisi wa Tanzania.

    ReplyDelete
  11. Rafiki yangu Salim Willis anaishi Chang'ombe yeye ni dreva wa magari ya mizigo

    ReplyDelete
  12. Anonymous11:01

    Gema yupo Muscat, Oman.

    ReplyDelete
  13. Anonymous16:13

    Monte Makangila amefariki na amezikwa makaburi ya Wailes jirani na ofisi za Manispaa Temeke kaburi lake lipo karibu na kinjia unapotokea ofisi za Manispaa kupandishia mtaa wa Mombo kuna msalaba na jina lake juu ya kaburi.

    apumzike kwa amani

    ReplyDelete
  14. Nakumbuka adhuhuri moja; jua linawaka, watu na shughuli zao, pale mtaa wa Makunganya, Dar es Salaam; magari si mengi kama leo. Nadhani mwaka 1981-83. Patrick Balisidya karudi toka Sweden. Ndo' katoa "Bado Kidogo" na Waswidi (Archimedes); alikuwa kakonda, macho yamemtoka, midomo mikavu; akinieleza habari zake. Enzi hizo bado nikiandikia magazeti kadhaa ya Uhuru, Mfanyakazi na kolam ya Sunday News. Kila nilipoongea naye miaka hiyo nilihisi kama ana hasira fulani. Si kama Kassim Magati kwa mfano au Marijani ambao ukiongea nao unawaona wana ari ya kuendelea na hawakati tamaa. Kila nilipoongea na marehem Balisidja baadaye nilihisi ni mtu aliyekuwa na njozi iliyokatwa katikati; kwamba hakumalizia safari yake, kwamba dhamira yake maishani haijakamilika. Miaka hiyo uchumi ulikuwa mgumu kishenzi. Nadhani Patrick akaanza sasa kuwa "freelance musician" akipiga piano hapa na pale. Ndipo akarekodi kile kibao bab kubwa cha "blues" na King Kiki. Kitime lazima utakijua. Siku hizi King Kiki ndiyo hufungulia dimba lake. Alipofariki kuna mzungu mmoja, hapa London, mwandishi wa habari (aliyeandika makala gazeti la Independent nadhani) akanifuata kutaka habari zake zaidi. Hazikuwa nyingi; na haikuwa rahisi kuupata (sembuse kuununua) muziki wake maana enzi Patrick akiwa "staa" hakukuwa na haya mablogu wala You Tube kama leo. Yeye na wanamuziki wengine bab kubwa kama James Mpungo (sijui Mpungo mwana Kitoto wa "Sunburst" yuko wapi s'ku hizi; Kitime unafahamu alipo?) walikuwa na vipaji na ufundi lakini vyombo vya kujitangaza na kujulikana vilikuwa redio na magazeti tu. Adimu. Si kama leo. Inasikitisha na pia ni fundisho fulani kubwa...kwa baadhi ya wasanii wa leo tusiochimba mambo kama hawa kaka zetu waliokuwa wazito kwa kina.
    Nimalizie kwa kusema hii blogu yako Kitime ni hazina kubwa kwetu Watanzania. Inahitajika sana sana sana...

    ReplyDelete
  15. Nina nia ya kufukua historia kwa wingi kadri iwezekanavyo ili iwe jukwaa la watu wengine kufanya utafiti zaidi kuna mambo makubwa ya kihistoria yamefukiwa katika historia ya muziki nchi hii. Nahitaji ushirikiano wa kila mzalendo maana ni zaidi ya upenzi wa muziki tu.

    ReplyDelete
  16. Anonymous14:38

    Freddy,

    Hukuwahi kumuona Marehemu Marijani siku za mwisho na yeye alikuwa kama Marehemu Patrick. Alihangaika kutafuta vyombo, wafadhili na waajiri vibaya mno tena sana. Kuna kipindi aliingia Mwenge jazz huko alikutana na majungu, fitina naroho mbaya mpaka akaondoka kama kuna mwanamuziki wa Mwenge jazz anayesoma blog hii hatabisha na ataniunga mkono.Marehemu marijani aliishia kuuza kanda zake mkononi kwenye mabaa na mitaani kama wamachinga.

    Kuna siku nilipita nyumbani kwake pale Mtaa wa Somali nikataka kuingia kwenda kuongea na mkewe lakini nilishindwa sikujua nataka kwenda kuzungumza nini.

    Mwenyezi Mungu awarehemu marehemu hawa kwa amani. Amen.

    ReplyDelete
  17. Ni kweli hali ya Marijani katika siku zake za mwisho haikuwa nzuri, alikuwa akifanya biashara ya kuuza kanda alizorudufu mwenyewe akawa na kama kiduka cha kanda pale nyumbani kwake. Mwaka 1995/96 mamake alijaribu kufuatilia haki za mwanawe katika redio za binafsi zilizokuwa zimeanza wakati huo, akiwa na msimamo kuwa mwanae alirekodi na RTD hivyo redio nyingine zozote zitakazopiga nyimbo za mwanawe zinastahili kulipa. Hawakutaka kumlipa mama huyu na jibu lilikuwa wao wamenunua kanda mtaani na hazijakatazwa kupigwa. Ilisikitisha

    ReplyDelete
  18. Yani inasikitisha!

    Twasubiria ulete shule ya HAKI MILIKI hapa MKUU!

    ReplyDelete
  19. Anonymous19:19

    Mkuu,

    Hapa ndipo kilipo kiini na mzizi wa mgogoro wangu na nchi yangu. Nchi yangu imewaharibu wananchi wake wengi sana. Na inaendelea kufanya hivyo hata sasa tena kwa makusudi, ufahamu na ustadi wa hali ya juu wa udhalili huu.

    Marehemu Patrick, Marijani, Mbaraka, Kulwa Salum na wengineo wangekuwa Waingereza wangekuwa wametambuliwa mchango wao na wangejulikana na vizazi vilivyozaliwa miaka hamsini hata mia baada ya kufariki kwao.

    Niliongea na Marehemu Patrick katika ziara yake moja ughaibuni na baadaye tukakutana tena Dar. He was disillusioned, disenchanted, allienated, frustrated, and confused beyond confusion. It was lamost the same na Marehemu Dozza (Marijani)siku za mwisho alikuwa anatuliza mambo kwa konyagi kama maji. Hakuwa yeye tena he was somebody else we never knew!

    Damn I am angry. Sorry wadau!

    ReplyDelete
  20. Si kwamba nchi yetu haina mashujaa, bali haitaki kuwatambua kama ni mashujaa labda wawe wanasiasa. Kama hakuna kujenga utaratibu wa kuwa na mashujaa katika kumbukumbu, vizazi vipya vinatafuta mashujaa wao, na ndio maana vijana wa leo hata wengine wakiwa wanamuziki wanangalia wasanii wa nje kama kioo chao cha mafanikio. Historia ni muhimu kuchimbuliwa na kuwekwa wazi. Vijana wangapi wanajua Hukwe Zawose alifikia mpaka mahala pa kushiriki kutengeneza computer programe ya upigaji wa kalimba? umahiri wa Nyunyusa katika kupiga ngoma nyingi,usanii wa Tingatinga,ambaye mpaka sasa hakimiliki ya uchoraji wake imechukuliwa na Disneyland, aliyeiuza hajulikani. Dozer, David Musa, Daudi Makwaiya, Balisdya, Hanzuruni, Wema Abdallah, Mike Enoch, the list is endless. Tulio na kumbukumbu tuzianike hapa. Tafadhali mwenye uwezo awaambie Ubalozi wetu Washington waondoe ile website ya ubalozi maana humo zimewekwa ngoma za kihindi eti ngoma za Tanzania,spergheti ndo chakula cha Kitanzania, imeelezwa kuwa Ndombolo na Zouk ni muziki wa kiasili wa Tanzania, baadhi ya wasanii waliotajwa kuwa kioo cha utamaduni wetu wengine si Watanzania kukasirika ni lazima aghhhhhhhhh

    ReplyDelete
  21. Anonymous01:47

    Mkuu,

    Sitaki na wala sipendi kuwa negavite lakini nchi yangu imeumiza sana wanamuziki na wasanii.

    Wanamuziki kama isingekuwa kulazimika kushabikia sera za TANU na CCM za Ujamaa na Kujitegemea pasingekuwepo na NUTA Jazz Band, Vijana, Urafiki,Biashara, Bima, UDA, au bendi za manjagu Polisi, Kimulimuli, Kimbunga, Magereza, Uhamiaji, Mlimani nk.

    Zile zilizokuwa bendi za wadau au binafsi, wafadhili, au kujitegemea kama Barkeys, Sunburst, Barlocks, Les Strokers, Trippers, Afrosa, Benebene,Dar International zilibinuliwa na kusabambaratika kama hazijui zilikuwa zinafanya nini lakini ndizo zilizokuwa zinapiga muziki wa kweli.

    Hapa tulipofika tushukuru serikali (pamoja na mapungufu mengi tena mno. You could have done better than use us. Anyway it is better to be used because when you are used you are useful. If you are not used then you are useless or worse you can be misused or abused). Shukrani zaidi kwa wanamuziki, wadau au wafadhili binafsi kama kina Mbaraka Mwishehe Mwaruka, Salum Abdallah Yazide, King Enock, Rev Father Canute Mzuanda, Rev Father Silvano na Stephano, David Musa mwana wa Gordon( You stand tall, ooh no, sorry tallest of all, I admire and respect you Bro. Niliambiwa unaumwa na mdogo wako Peter alitaka nije kukuona lakini nilishindwa. Bro David, Usisahau pale tunaposali na kusema "Utusamehe makosa yetu kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea.. Yes, he screwd up but forgive him and love him for what he was. You were like Ceasar and Brutus. The difference between you and him you did not stab him but you let him go"), Gema (come out now! History is in the making. You are needed to connect the dots), Mhutos (Wakuu, you are sweet peeper/ pilipili tamu: Meck, Alice, George, Paul, Charles, Teddy, Gerry you know who you really are! Come out as you are and it will shake than ever before). Kapingas George, Abraham,and Amato it is time to talk the talk). Lukindos (Freddy and Athanas you are heroes. No biography needed we need autobiography and here is the space jot it down!), Galinomas (particulaly Innocent. Bro, you were and still something specials: unapiga muziki na unachora picha halafu unacheka na kuchekesha, come on man give the world what you have been given to it to!.) Mendes, Tshaka, Ndabagoye, Marehemu Mwendapole, Hugo Kisima, Korean Cultural Centre, Mzee Makala, Mama Kimesera, Butimba TTC na walimu wengine wote mliofundisha wanamuziki njooni mseme.

    ReplyDelete
  22. Anonymous02:14

    Mkuu,

    Marehemu Mike Enoch na Joseph Mulenga walikuwa Watanzania? Mzee Kiki naye ni Mtanzania? Wamechangia kiasi gani kwenye muziki wa Tanzania?

    ReplyDelete
  23. G.Mlundwa18:54

    Nico zengekala? pia alikuwa mtanzania au?? Ni katika wasanii waliokuwa wananifanya nisikilize Radio Tanzania!!! RIP

    ReplyDelete

SAFARI ZANGU NA BENDI sehemu ya kwanza.

  TANCUT ALMASI ORCHESTRA  wakiwa Jamhuri Stadium Dodoma   Sikumbuki ni safari ngapi za kimuziki nilizowahi kuzifanya hapa nchini katika m...