YOUTUBE PLAYLIST

Friday, March 19, 2010

Cuban Marimba


Kuanzia miaka ya 1920 mpaka 1940 Tanzania, hususani Tanzania bara, wanamuziki na wapenzi wa muziki walifuatilia sana muziki kutoka Cuba kupitia sahani za santuri za wakati huo. Kulikuwa na vikundi kama Trio Matamoros and Sexteto Habanero, ambao walitoa santuri zikiwa na namba zinazoanzia GV1, GV2 na kuendelea na kupata upenzi mkubwa katika ukanda huu wa Afrika. Ni vikundi hivi ambavyo viliingiza mitindo kama rhumba, Bolelo, Chacha na kadhalika. Kwa kweli bendi za muziki wa dansi zingepata mengi ya kimapinduzi kama zingeweza kusikiliza na kuelewa muziki wanaoupiga kiini chake ni nini.

Kutokana na hamu hiyo ya kuujua na kuupiga muziki wa kicuba kisawasawa Marehemu Salum Abdallah aliwahi kutoroka kwao Morogoro akakimbilia Mombasa ili apande meli aende Cuba, bahati mbaya safari yake iliishia Mombasa kwa kuishiwa fedha, ambako alianza kupata shida lakini kwa kuwa baba yake alikuwa mwarabu, Ushirika wa waarabu wa Mombasa walimtaarifu mzee huyo kuhusu alipo mwanae na alimfuata na kumrudisha Morogoro. Salum Abdallah Yazidu aliyefahamika sana kama SAY, mwaka 1948 alianzisha bendi yake akaiita La Paloma, ambalo ni jina la wimbo maarufu ambao uliotoka Cuba ukiwa na maana Njiwa, wimbo huu unaendelea kupigwa hadi leo ukiimbwa na kurekodiwa kwa lugha mbalimbali, hata hapa Tanzania bendi nyingi huzisikia zikipiga wimbo huu na kuweka maneno yake ya papo kwa papo hasa kabla dansi rasmi halijaanza. Bendi ya La Paloma ndio ilikuja kuwa Cuban Marimba Band, Salum Abdallah aliiongoza bendi hiyo mpaka kifo chake 1965. Aliyeichukua na kuiendeleza alikuwa Juma Kilaza. Kilaza aliiendeleza vizuri kwa kutunga mamia ya nyimbo yaliyofurahisha sana watu miaka ya 60 na 70. Morogoro ulikuwa mji uliosifika kwa muziki, huku kukiwa na Mbaraka Mwinshehe na Morogoro Jazz, na huku Juma Kilaza na Cuban Marimba. Kuna watu walikuwa wakihamia Morogoro wikiendi na kurudi Dar siku ya Jumatatu asubuhi. Kati ya nyimbo maarufu za Cuban Marimba zinazodumu kwenye kumbukumbu ni wimbo Ee Mola Wangu, ambao Salum Abdallah awali aliutunga kwa mashahiri marefu lakini akachukua beti chache kutengenezea muziki akilalamika kuwa kuna walimwengu wanamtakia mabaya, lakini siku ya kufa atawashitakia maiti wenzake kuhusu ubaya huo.

Pichani ni Cuban Marimba baada ya Salum Abdallah, wa kwanza kulia Juma Kilaza, mwenye mawani Ufuta mpiga solo. Wadau malizieni majina ya hawa wanamuziki wengine. Mheshmiwa Tsere uliishi sana Morogoro tusaidie

17 comments:

  1. Anonymous12:43

    Mzee Kitine shukurani sana kwa hizi habari za muziki. Zinatukumbusha mbali sana. Ingawa wengine tulikuwa na umri mdogo, tulipata kusikia na kucheza baadhi ya nyimbo za hawa jamaa. Kuna wakati tulisikia Juma Kilaza aliharibu mambo TZ akakimbilia kenya. Ni kitu gani kilitokea mpaka akaondoka TZ.Mdau Haji Hamis

    ReplyDelete
  2. Kwa hakika ni mara ya kwanza kusikia Kilaza aliwahi kukimbilia Kenya, lakini kwa vile nina mtu wa karibu yake sana niliye na mawasiliano nae, ntamwuliza kuhusu hilo.

    ReplyDelete
  3. Anonymous14:26

    Mkuu,

    Nina swali la kizushi: Nani mtunzi na bendi gani iliyopiga ule wimbo unaopigwa RTD wakati wa sikukuu ya Krismasi? Wimbo ule unaoimba "..I hepi krismasi iyoo iyoo, i hepi nyuyaa iyoo iyoo.." Nitafurahi sana kujua kama huu wimbo ni local au imported Christmas charol. Asante.

    Nilikuomba safu ya Sunburst katika ile mada ya Banchikicha. Nimeona Freddy Macha kaanza na Kassim Magati na James Mpungu.

    ReplyDelete
  4. Patrick Tsere14:43

    Aisee John. Ninaowakumbuka ni mpiga bass akiitwa Sekuru na mpiga solo akiitwa Waziri ambaye nahisi ndiye Ufuta. Maana Waziri akivaa miwani.Kwenye picha sidhani kama Sekuru yupo.Hivi Juma Ubao hakuwa Cubano kweli? Au alikuwa Polisi Jazz ndiyo akaja Biashara Jazz ya BIT?

    Pale Morogoro ushindani kati ya Juma Kilaza na Mbaraka ulikuwa mkali na wakati mwingine wa kihasama. Unaukumbuka ule wimbo wa Mbaraka akimsuta Kilaza."Tulikuwa na Salum mpaka alipoenda ahera wala hatukutukanana amekuja huyu mchafuzi jina la Morogoro limeharibiwa naye..."Something like that??

    ReplyDelete
  5. Mzee Kitime vipi bendi ya mzinga. ilianza lini na kumalizika lini. na kibao chao cha mazoena yananikondesha alikiimba nani na ujumbe hasa ulikiwa nini maana wengine wanasema anamuimba mpenzi wengine wanadai analalamika kunyang'anywa wanamuziki na bendi nyingine.

    ReplyDelete
  6. Mzinga Troupe ilikuwa bendi ya jeshi ya kikosi cha mizinga Morogoro. Sina historia kwa sasa lakini bahati nzuri kuwa mpiga besi wa Kilimanjaro Bendi Keppy Kiombile aliwahi kupigia bendi hiyo , na mpiga solo wakati huo alikuwa kaka yake ambae ni marehemu, nitamuuliza maswali yako yote halafu tusikie ilikuwaje mkuu.

    ReplyDelete
  7. Bendiu iliyopiga wimbo wa Happy Krismas ni ya Kitanzania na ilikuwa bendi ya wanawake watupu, nisimalize utamu ngoja nitatoa hadithi yao yote, haijatokea tena kama ile.

    ReplyDelete
  8. Mheshmiwa Tsere nilijua utakuwa na jibu la kutia changa moto. Waziri Nyange ndio jina halisi la mpiga solo huyo, na kuna wakati alikuwa ameaacha shughuli za muziki na kuwa mganga wa tiba asili bango lake lilikuwa pale kwenye taa za trafik Jangwani, mwaka 1995 aliwahi kunipa kanda yake ya nyimbo alizotunga lakini sidhani kama aliziendeleza. Ufuta ni mwingine. Sina uhakika kama Juma Ubao aliwahi kupigia Cuban Marimba lakini yupo tutamuuliza atueleze safari yake ya kimuziki toka upolisi mpaka Kumbakisa

    ReplyDelete
  9. Anonymous19:02

    Mkuu,

    Nimekuuliza makusudi kuhusu Happy krismas kwa sababu kule kwenye ile thread ya wanamuziki wanawake hukuwataja baadhi ya kina Dada waliowahi kung'ara kwenye muziki wa Tanzania.

    ReplyDelete
  10. Mheshimiwa Kitine kwa hakika Salumu Abdalla alikuwa mkali, mimi binafisi kuna nyimbo zake mbili ambazo zinanikosha moja ni ile aliowasifia wanawake wa Tanzania kuwa ni wazuri sana, Pili kuna wimbo mmoja una mameno yanayosema mpenzi wangu njoo tufurahi ngoma iko huku na nyingine ambazo nimesahau majina yake.

    ReplyDelete
  11. Anonymous02:05

    Anonymous 4:36 AM, Safu ya Sunbursts ni : (1)Marehemu Kassim (keyboards), (2) James (vocals), (3) Bashir Idi Farhani (bass), (4) Abdallah aka "Johnny Rock" (drums), (5) Florrie (solo) huyu alikuwa Mkongo (Mzaire enzi hizo). Idarusi.

    ReplyDelete
  12. Anonymous15:12

    Miaka ya 80 kulitokea bendi inaitwa 'less Cuban' au jina linalofanana na hilo. Nafikiri maskani yaliwa morogoro pia. Mwanamuziki marehemu alitokea bendi hiyo kabla ya kujiunga na Msondo. Alitunga wimbo Jacky, wenye maneno kama mtoto jacky mpenzi wangu, najaribu kukusahau lakini nashindwa, hasa kwa ile ndoto inayonisumbua, naota unaniletea ... cha zambarau....
    Mzee Kitine, hii bendi ilikuwa na uhusiano wowote na Cuban Marimba,e.g. ilianzishwa na wanamuziki wa Cuban Marimba etc?

    ReplyDelete
  13. Kwanza naomba nisahihishe jina langu naitwa KITIME si Kitine. Sina uhakika Les Cuban ilianzishwa na nani na kwanini iliitwa Les Cuban, japo kipindi hicho ulikuwa mtindo wa bendi ikijiengua kuongeza Les pale mbele, kama vile Les Wanyika, na ilifikia mpaka kukaweko na Orchestra Les Les. Banza Tax na Shaaban Wanted wote walipigia Les Cuban na kuja kujiunga Tancut na tulikuwa tukiupiga wimbo huo ulioimbwa na Marehemu Nico Zengekal yule muimbaji stadi aliyekuwa kipofu, Banza alisema aliutunga huu wimbo yeye na sikusikia mtu kupinga kwa hiyo mtunzi ni Banza Tax. Ila Juma Kilaza alikuja kujiunga na bendi hii baada ya kurekodiwa hizi nyimbo za Album ya Jacky, hivyo nadhani kuna hadithi hapa

    ReplyDelete
  14. umenikumbusa niko zengekala. sijawahi kumuona na hivyo sura yake siifahamu. hakuna picha yake katika makabrasha yako.

    ReplyDelete
  15. Kwakweli uncle hebu pekuapekua kwenye makabrasha yako, hata mimi nihitaji sana kuona picha ya huyu Jamaa, kwakweli alikua kiboko......Solemba imesimama mpaka kesho nafkiri hata ule msemo wa kumuacha mtu solemba ulianzia hapo......sauti kinanda

    ReplyDelete
  16. Masahihisho kidogo mimi nilikuwa Morogoro kipindi bendi ya Les Cubano inaundwa na kadri ninavyojua Kilaza hajawahi kukimbilia Kenya ila alikwenda huko kujaribu maisha baada ya bendi yake TK Lumpopo kushindwa kuendelea kama ilivyotokea kwa Super Volcano. Akiwa Kenya alianzisha bendi ya Magola International ambayo nayo haikudumu sana alirejea Morogoro ambako kwa msaada wa Mkoa ilianzishwa bendi ya Les Cuban ikiwaunganisha wanamuziki wa zamani wa Cubano Marimba na ikawekwa chini ya Uongozi wa Juma Kilaza, baadae bendi ya Vina Vina iliyokuwa Kenya ikiwa na wanamuziki wengi wa Kitanzania wengi wao wakiwa wa kutoka Morogoro nao walikuja Morogoro ila walikuwa wakichangia vyombao na Les Cuban hatimaye Kilaza alinyang'anywa uongozi na bendi nzima kutawaliwa na wanamuziki waliokuwa wa bendi ya Vina Vina ambao waliendelea kutumia jina la Les Cuban na jina lao la uwali kubaki kama mtindo wao wa dansi.

    ReplyDelete
  17. Naomba historia ya Jabali la Muziki Marijani Rajab

    ReplyDelete

SAFARI ZANGU NA BENDI sehemu ya kwanza.

  TANCUT ALMASI ORCHESTRA  wakiwa Jamhuri Stadium Dodoma   Sikumbuki ni safari ngapi za kimuziki nilizowahi kuzifanya hapa nchini katika m...