Jukwaa la wapenzi wa mambo ya muziki wa Tanzania-

Breaking

Wednesday, February 17, 2010

Vijana Jazz Vs Maquis

Katika kipindi cha mwisho cha miaka ya 80, Kinondoni ilkuwa inawaka moto kwa Vijana siku ya Jumapili. Lang'ata ambayo baadae ilikuja kuwa Club ASET na sasa kanisa, palikuwa ndo ukumbi wa Dansi za kuanzia mchana kwa Bendi ya Maquis. Ukija hapa mbele Vijana Jazz Pambamoto awamu ya pili chini ya uongozi wa Hemed Maneti walikuwa nao kila Jumapili mchana wanaporomosha Dansi, na siku hiyo ilipewa jina Vijana Day. Kwa kweli Maquis walikuwa wanajaa watu na Vijana wanajaa watu. Kulikuweko na wapenzi wa kudumu wa Vijana kama ilivyokuwa Maquis. Wakati huo nyimbo kama Ngalula, Makumbele zilikuwa zinalia Lang'ata huku Vijana wanateremsha Shingo feni, Ngapulila, Azda. Ushindani huu ulilazimisha bendi kujitahidi kupiga vizuri na kwa displine au la wapenzi wanahamia bendi jirani. Kuna wakati Vijana Jazz walikuwa wanaanza muziki saa kumi na moja jioni na kupumzika saa tatu na nusu usiku kisha kumaliza dansi saa nne. Maquis wakawa wanaanza saa kumi na kumaliza saa tano usiku. Na wakaanza kuruhusu mtu yeyote atakayekuwa kapigwa muhuri wa kuruhusu kutoka nje ya ukumbi Vijana Jazz,aliruhusiwa kuingia Maquis bure. Vijana wakabadili ratiba na kuanza kupiga saa 9 mchana, kwa mtindo wa bandika bandua, yaani muziki nonstop. Na kufuta kupumzika hadi saa tano. Hiyo ndo ilikuwa raha kwa wapenzi. Vijana haikuwa na show wakati wa Maneti, Lakini show ilikuja baadae katika kukabili show ya Maquis ambayo ilikuwq nzuri sana chini ya mwalimu wao Wabangoi. Majina makubwa yalitawala madansi hayo Maquis kulikuwa na Dekula Vumbi kwenye solo,second solo Mbwana Cox (aliyetoka Vijana Jazz), banza Mchafu Bass, Nguza Viking, Adios, Tshimanga Assossa,Parashi Lukumbule Vijana Jazz kulikwa Shaaban Wanted, Hemed Maneti, Eddy Sheggy, Adam Bakari, Kida Waziri, Abou Semhando, Rashid Pembe na wengine wengi, basi raha kila jumapili ilikuwa kama tamasha

8 comments:

EDWIN NDAKI said...

nivunje kikombe nisivunje..vunja..baadhi ya maneno unayoyakuta kwenye wimbo wa Vijana Jazz chini haya Maneti ...Jina la wimbo Muninde yaani ilikuwa safi sana...

Bado Vijana walikuwa na kitu kingine Maria..nilivyoo muhusudu mtoto mary sijatoka kupenda tangu nizaliwee.eee...

When music was music..

Asante sana mkuu Kitime kwa kutukumbusha hizi..

tupo pamoja

Tutafika tu

John F Kitime said...

Jina la wimbo lilikuwa Mundinde. Alikuwa mama mmoja anaishi nyuma ya eneo lililokuwa linaitwa Jambos kwa Mzee Vulata

Anonymous said...

John Mwakitime,
Kazi nzziri sana kaka wewe ni hazina ya muziki wa miziki ya nyakati hizo ambao kwa sasa hautarudi tena. hebu fikiria kuwa na redio program yako angalau kwa mara moja kwa wiki kuzungumzia haya kwa faida ya wanamuziki wa kizazi kipya. Usijali kuhusu udhamini. Nitakupa detail zangu kwa email. kazi safi sana mzee nyongise!!!!!

John F Kitime said...

Kwa redio gani mkuu? hizi zenye kudharau Utanzania?

Baraka Mfunguo said...

Mkuu nilikuwa naomba ukumbushie historia ya Marquis. Pamoja na ushindani wao baadae dhidi ya bendi nyingine na hapa kulikuwa na wapiga gitaa mahiri kama vile Maestro Ndala Kasheba na Mzee Nguza Viking. Nasikia kuna siku iliwekwa ligi mpaka Kasheba akavunja gitaa. Mambo mengine kama Dukuduku, Paselepa na akina King kiki double O, Mangelesange na wengineo. Kwa kweli historia haiwezi kujirudia lakini ni vizuri kizazi chetu kikajifunza tulipotoka.

John F Kitime said...

Pole pole tutapata yote kwa kusaidiana na wadau wengine wa blog hii. Lakini nakumbuka mkasa wa kuvunja gita Kasheba ulitokea katika maonyesho ya Bendi mbili pale DDC kariakoo, alivunja gitaa lake baada ya midadi kupanda utamu ulipomzidi.

Gad said...

Wadau kumbukumbu ni nzuri sana, na zitaendelea. Muhimu pia kupata mwafaka wa jinsi gani muziki huu utakavyoweza kuenziwa kwa muda mrefu, ili kupunguza kasi hii ya kila radio na tv kucheza na kuonesha muziki wa kisasa tu. Kazi nzuri sana mkuu kwa kujitahidi kurudisha kumbukumbu za muziki huu kwenye mstari.

Anonymous said...

"..USHABIKI MBALI ORCHESTRA MARQUIS DU ZAIRE COMPANY LIMITED (OMACO) LILIKUWA TAIFA KUBWA!.."

Baada ya kusema hivyo naomba nitetee hoja yangu: Kimuziki Marquiz walikuwa wanapiga muziki mzuri sana kwa sababu ulikuwa ni muziki uliokuwa umepangiliwa na kuratibiwa sawasawa. Hii ilitokana na sababu kwamba Marquiz walikuwa muundo madhubuti wa kuwasaili wanamuziki wao kabla ya kuwaajiri. Kwa hali hiyo walikuwa wanaajiri wanamuziki wenye vipaji au uwezo wa hali ya juu wa kupiga muziki. (Kwa maelezo juu uajiri kwenye bendi ya Marquiz unaweza kuwauliza kina Mzee Audax, Mzee Kiki, Vumbi Kahanga au Mzee Nguza kama ikiwezekana). Iliwabidi Marquiz kufanya hivi kutokana na ushindani katika soko la muziki wa dansi wakati ule. Tukumbuke kwamba wakati ule kulikuwa hakuna play back music wala video na madisco hayakuwa na nguvu hivyo na hatukuwa na FM na watayarishaji wa vipindi wachanga au wasio na itikadi inayoeleweka. Utandawazi ulikuwa umedhibitiwa na hivyo mazagazaga toka nje yalikuwa siyo mengi kama yalivyo sasa.

Pili, Marquiz ilijimiliki yenyewe tofauti na bendi nyingi za wakati ule ambazo zilikuwa zinamilikiwa na taasisi za umma kama Majeshi (Kimbunga, JKT, Mwenge na Polisi), na idara mbali mbali za umma kama Bima, Uhamiaji, Usalama wa Taifa na baadaye DDC Mlimani Park, Bodi ya Biashara au jumuiya za chama tawala kama Umoja wa Vijana (Vijana Jazz) na Jumuiya ya Wafanyakazi Tanzania (NUTA-JUWATA-OTTU na sasa MSONDO)nk. Kwa kujimiliki yenyewe Marquiz ilibidi ifanye kazi ya ziada ili kuweza kujiweka kwenye soko ili kuukabili ukiritimba wa vibali vya kuishi na kufanyakazi nchini Tanzania (Work and Residence Permits). Hali hiyo iliwafanya Marquiz siyo tu kujihusisha na muziki bali pia kujihusisha na ujasiriamali (Business entrepreneurship)ambapo walimiliki ukumbi wao wa muziki White House Savannah, majumba, walimiliki mashamba, magari na pia pia dirisha la kuuzia mazao yao Kariakoo sokoni.

Marquiz nadhani ndiyo ilikuwa bendi ya kwanza ya muziki wa dansi kurekodiwa na kuonyeshwa na TVZ hii ilikuwa kama sikosei mwaka '77 au '78. Katika ile recording walikuwa wamevaa Tuxedo suits za nguvu sana ambazo zilikuwa ni moja kati ya maleba (costumes) zao nyingi nzuri za kuvutia sana.

cha ajabu ni kwamba hata muziki wa halaiki ya wanafunzi wa mkoa wa DSM wakati wa sherehe ya kuzaliwa kwa chama kipya cha CCM mwaka 1977 ulipigwa na Orchestra Marquiz Du Zaire na siyo bendi nyingine zozote zilizokuwa zinamilikiwa na idara za serikali au jumuiya za chama.

Nakumbuka rafiki yangu mmoja ambaye ni bassist aliniambia kwamba tukiwa Marquiz tukila nyama na kunywa tuzoe mifupa na visoda tuondoke navyo kwa sababu eti baada ya muziki Marquiz huwa wanakusanya visoda na mabakibaki ya mifupa na ndizi halafu wanapeleka kwa mganga wao. Ndiyo maana wapenzi wa Marquiz wanakuwa kama mateja ya unga bila ya Marquiz hawalali.

Mara ya mwisho nilienda Marquiz Lang'ata Kinondoni. Marquiz ilikuwa bado moto juu kama ilivyokuwa miaka ya '70 na '80.

Nilimuuliza mmoja wa wanamuziki wa mwisho mwisho wa Marquiz sababu ya Marquiz kufa aliniambia kulikuwa na tatizo kwenye uongozi na udhibiti wa mahesabu kwenye kulipa kodi.

PS/
Mkuu,

Vijana Jazz nadhani ndiyo bendi ambayo nilihudhuria maonyesho yao mengi kuliko bendi zote nilizowahi kuhudhuria maonyesho yao. Zilikuwa enzi zile walipokuwa wanapiga Mkirikiti Bar, Msasani. Enzi za Amba, Shoga Kidawa kanipandishia na kanzu zake nk. Halafu na wale mashabiki kina Dada Filomena kama utakumbuka na kunipata nasema nini?

Adbox