YOUTUBE PLAYLIST

Friday, February 12, 2010


Mwaka 1982/83 Tchimanga Kalala Assossa alianzisha na kuongoza bendi iliyoweza kutia changa moto katika ulimwengu wa muziki wakati huo. Bendi hiyo iliitwa Orchestra Mambo Bado na mtindo wake wa Bomoa Tutajenga Kesho. Wanamuziki katika bendi hiyo walikuwa Tchimanga Assossa, Kiongozi na muimbaji, Kazembe wa Kazembe mpiga solo (pamoja na jina hilo alikuwa Msukuma), William Maselenge, rythm guitar, Huluka Uvuruge second solo guitar, Sadi Mnala drums, Mzee Albert Milonge second solo, Lucas Faustin muimbaji, John Kitime muimbaji na rythm guitar, George Mzee muimbaji, Athuman Cholilo muimbaji, Likisi Matola Bass na keyboards, Jenipher Ndesile muimbaji, selemani Nyanga Drums. Album ya kwanza ya bendi hii ilikuwa na nyimbo zilizotamba kama vile Kutokuelewana, Bomoa Tutajenga Kesho , hii ilipigwa marufuku. Picha ya Assossa iliyotoka kwenye tangazo la kwanza la bendi, hapa akiwa amevaa shati la ndege ambalo kwa siku hizo walikuwa wanavaa wajanja tu.

11 comments:

  1. Hakika blog hii ni hazina tosha ya historia ya muziki wa Kitanzania. Nimeipenda sana. Hongera sana kwa kazi nzuri. Nimefurahi kufika katika blog ya mwanamuziki kweli. Ndashene!
    Nitakuwa mgeni hapa siku zote.
    Upatapo nafasi tafadhali karibu pale fadhilimshairi.blogspot.com uweze kujisomea mashairi katika lugha adhimu ya Kiswahili.

    ReplyDelete
  2. Dah!! Hii listing imenikumbusha kipindi cha Klabu Raha Leoooooooo....Shooooooow!!!!
    Tshimanga Assosa nilibahatika kumuona akitumbuiza na naamini ilikuwa ni mwaka 1991 alipokuja Nachingwea, Lindi na bendi yake ya Bana Marquiz (kama sijakosea jina).
    Nilikuwa nakubali kazi zake na japo sitaweza kukumbusha nyimbo alizowika nazo, lakini nakumbuka nilikuwa msikilizaji mkubwa saana wa Redio Tanzania na kati ya vitu ambavyo ningefahamu wakati wote ni mwanamuziki gani (mashuhuri) kaenda ama kahamia wapi.
    Nilikwa na upinzani na Mjomba wangu na ilikuwa ni kama usajili vile. Msondo wakimchukua huyu, basi ni kusikilizia Sikinde wangemnyakua nani. Iwe ni Washirika Tz Stars ama MCA International (wana Munisandesa). Iwe ni Bima Lee ama nyingine.
    Ninapokumbuka nyakati hizo, nausikitikia muziki wetu ulipo sasa.
    TUNAJIPOTEZA KATIKA HARAKATI ZA KUJITAFUTA.
    Baraka kwako Uncle na ntazidi kusoma na kurevuka kuhusu Muziki wa Tanzania, kutoka kwa mwanamuziki halisi wa kiTanzania

    ReplyDelete
  3. Tanzania hatuna utamaduni wa kuenzi mashujaa labda wawe wanasiasa, tuna watu ambao ni aibu kutowaweka katika historia ya nchi, Mzee Nyunyusa ambae ngoma zake husikika kila siku kwa vizazi karibu vitatu amefariki na hakuna cha kumuenzi, Marijana ambae shahiri lake la Mwanameka lilitumika katika mtihani wa Kiswahili wa Form 4, Maneti, Mbaraka, Kilaza, Balisdya, listi ni ndefu, kwa kuwa hatuwaenzi vijana wanakuta wanaoenziwa ni kina Tupac, Bob Marley, Michael Jackson, ndiyo ni wanamuziki mahili wa hali ya juu lakini na sisi tunao. Hebu fungua website ya Ubalozi wetu Marekani umeandika kabisa kuwa zouk na Ndombolo ni Tradiotional music yetu.!!!!!!!!!!!!!!!!!

    ReplyDelete
  4. Uncle hiyo nimeiona na hilo limenifanya kujiuliza swali (katika kipengele cha blogu yangu cha WALIWAZA NINI?)(http://changamotoyetu.blogspot.com/2010/02/kweli-twatofautiana-kuwaza.html)
    Nimenukuu kama ulivyoagiza kwenye FB na kisha kuweka link. Nimepata emails nyiingi nikiulizwa IMEKUWAJE WAHUSIKA HAWAONI?
    Jibu ni moja tuuuu.
    WHO CARES.
    Hiyo list yako ni sehemu ya ambayo inatufanya tuwaze. WANAWAZA NINI?
    Niliwahi kuandika kuhusu "wasanii kama chombo cha starehe nchini mwetu" ambapo wanatumiwa kwenye kampeni kama GEZAULOLE, KUKARIBISHA VIONGOZI NA SHEREHE NYINGINE LAKINI BAADA YA HAPO....

    ReplyDelete
  5. Kitime mimi ni mmoja wa watu ambao walikuwa wanahudhuria katika show ya mambo bado pale Stereo Kinondoni, mambo yalikuwa mazuri sana chini ya uongozi wa Assosa. Pia nakumbuka mbali na kuimba nyimbo za kwao, walikuwa wanapenda kuiga nyimbo za wanamuziki waliotamba enzi hizo kama Lionel Richie. Mwisho napenda unieleze nini sababu ya kupigwa marufuku wimbo wa BOMOA TUTAJENGA KESHO.

    ReplyDelete
  6. Ni kweli Orchestra Mambo Bado walikuwa pia wakichanganya nyimbo za kuiga. George Mzee ndie alikuwa mwimbaji mkuu wa nyimbo hizo, Likisi Matola kwenye keyboards, Mzee Andre Bass, Huluka Uvuruge solo gitaa, Sadi Mnala Drums, wakti huo nyimbo zilizopigwa zilikuwa kama Holiday, Anjelina,Wanna be starting something na kadhalika. Kuna kitabu nilishiriki kuandika na mwanazuoni Kelly Askew Popular Music censorship in Africa,ambacho ndani yake kulikuwa na taarifa ya matukio ya kupiga marufuku au censorship katika muziki barani Africa, hata humo nilisema na mpaka leo nasema sijui kwa nini nyimbo ile ilipigwa marufuku. Ila najua kwanini ilitungwa. Orchestra Mambo Bado walianza kufanya mazoezi Mabibo Maziwa, katika bar iliyoitwa Lango la Chuma. Ilikuwa wakati huo imekarabatiwa naikawa imepangwa kuwa Bar na bendi zizinduliwe siku moja. Wakati mazoezi yanaendelea, nyufa zikaanza kutokea upande moja wa lango kuu, wanamuziki wakawa wanamtania mwenye bar kuwa siku ya uzinduzi geti litabomoka, mwenyewe akajibu bomoa tutajenga kesho, wimbo ukazaliwa, hao waliopiga marufuku sijui walikuwa na sababu gani

    ReplyDelete
  7. Anonymous01:49

    Assossa alikuja Tanzania na Les Kamale mwaka '77 kama sikosei. Nakumbuka katika nyimbo zake na Les kamale kulikuwa na ule wa Masua. Pia nakumbuka picha waliyotokea gazeti la Uhuru wakati wanashuka toka kwenye ndege.

    Kuna rafiki yangu halafu kuna jirani yetu walikuwa wanunuzi wazuri sana wa rekodi na walikuwa nazo rekodi za Les Kamale, Lipua Lipua, Orchestra Veve, Sososliso (Mwaka 2007 nilinunua CD ya Sosoliso -TrioMadjesi) na zinginezo. Wakati huo huo ndipo Simba Wanyika walipoipua Sina makosa.

    Kipindi hicho (katikati ya miaka ya 70) kulikuwa kuna Record Label ilikuwa inaitwa Sindimba ambayo ilikuwa nakshi na picha ya ngoma ya mapambo ya kusuka. Wadau, Record Label ile ilikuwa inamilikiwa na nani?

    Miziki mipya ya bendi zetu ulikuwa unasubiri RTD kipindi cha Misakato Ijumaa usiku. Kipindi cha Misakato ilikuwa akiingia fundi mkuu mwenyewe Ngariba, Mwana wa Manyema, Jabali la Muziki, Dosser, Marijani Rajabu. Vitu alivyokuwa anaipua na maelezo yake utake usitake, awike jogoo, bata au mbuni mkuu wa ndege wote utakubali kwa shingo upande au nyoofu kwamba bingwa kashinda.

    Babake! RTD ilikuwa ya kina Elly Mboto, Chris George, Gothalum Kamalamo, Tido Mhando, Abdul Masudi Jawewa, Batholomeo Kombwa, Abdul Ngalawa, Mikidadi Mahmoud, Abdallah Mlawa, Mshindo Mkeyenge, David Wakati, Paul Sozigwa, Salim Mbonde. Aaarrghhh!!! Gone are the days but any/someway they can be reversed! Can't thay?

    ReplyDelete
  8. Hapa naona umetuchanganya mambo mengi, Assossa alikuja kwanza hapa Tanzania na Fuka fuka, baadae akajiunga na Mlimani Park Orchestra, ndie mtunzi wa kibao cha Gama cha Mlimani Park. Sijawahi kusikia Marijan Rajabu kuwa mtangazaji wa RTD. Na listi ya watangazaji wa RTD wametokana na awamu tofauti kiasi inachanganya

    ReplyDelete
  9. Anonymous14:08

    Mkuu,

    Ninukuu tena
    "..Assossa alikuja Tanzania na Les Kamale mwaka '77 kama sikosei. Nakumbuka katika nyimbo zake na Les kamale kulikuwa na ule wa Masua. Pia nakumbuka picha waliyotokea gazeti la Uhuru wakati wanashuka toka kwenye ndege.." Nashukuru kwa kunikumbusha kwamba Assossa alikuja na Fuka Fuka. Asante sana.

    Sikumaanisha Marijani alikuwa mtangazaji kumuita Fundi Mkuu nimemremba kama bingwa.

    Ninamfahamu Marijani tangu Olympio mpaka Tambaza hadi Urafiki Textile Mills. Toka Mtaa wa Somali, Kariakoo hadi Chang'ombe kwa David Mussa. Pale yalipokuwa makao makuu ya Dar International wanaSuper Bomboka aliishi Marehemu rafiki yangu mpenzi alikuwa hotelier na paparazi Mwenyezi Mungu Amrehemu na Ampe Amani. Amen.

    Miaka imepita na si rahisi kuwakumbuka watangazaji wote. Hao watangazaji niliowataja ni wale ambao nawakumbuka kati ya 1970 na 1980. Katika listi hiyo nilikuwa sikumtaja human encyclopedia Mzee Khalid Ponela. Wanne au watano kati ya hao niliowataja kwa nyakati tofauti walikuja kuwa Wakurugenzi wa RTD Elly Mboto, Paul Sozigwa, David Wakati, Abdul Ngalawa kama sikosei na sasa Tido Mhando.

    PS/
    Swali la kizushi: Tanzania hatuna shule za muziki na hatuna madarasa ya muziki mashuleni lakini tumeweza kuwa wanamuziki kuanzia waimbaji hadi wapiga ala. Wamamuziki wetu hujifunzia wapi muziki?

    ReplyDelete
  10. Thanx kwa kuchangamsha blog. Shule za muziki zipo kadhaa japokuwa wanamuziki wengi hawapitii kwenye shule rasmi, wengine hujifunza kwa wanamuziki waliopo,wengine wamezaliwa na kipaji cha nafasi mbalimbali katika muziki, wengine hujiunga na muziki na hata kujulikana na kuwa kaarufu na kujifunzia kazini, wengine huwa maarufu wakati hawajui lolote lakini wamepata promo kubwa

    ReplyDelete
  11. Anonymous16:42

    Mkuu,

    Hawa wanaojulikana kwa promo kubwa wamekuja siku hizi. Kibaya zaidi hata hao wanaowapromot hawajui athari za wanachokifanya katika mapana yake. Kwanza wanaua vipaji. Pili wanavuruga soko. Tatu wanaua music identity ya nchi.

    Nimetembelea bendi za siku hizi nikakuta wamejaza watu kibao lakini kimziki hamna kitu kabisa. Yaani performance na audience yao inafanana zaidi na graduation ya secondary school. Wanamuziki na mashabiki wao kama social cult fulani iliyopagawapagawa.

    ReplyDelete

SAFARI ZANGU NA BENDI sehemu ya kwanza.

  TANCUT ALMASI ORCHESTRA  wakiwa Jamhuri Stadium Dodoma   Sikumbuki ni safari ngapi za kimuziki nilizowahi kuzifanya hapa nchini katika m...