Jukwaa la wapenzi wa mambo ya muziki wa Tanzania-

Breaking

Thursday, January 21, 2010


Hebu jaribu kupata picha, umelima shamba lamba lako na kupanda mahindi ambayo umeyatunza vizuri na yako tayari kuvuna….. unaamka siku moja na kukuta kuna mtu kayavuna na ameanzisha biashara anapata fedha nzuri wewe huna hata fedha ya kula.

Au umenunua suti nzuri akaja mtu akaivaa harusini, kesho yake anakuja kukutaarifu jinsi walivyomsifia harusini.

Hiyo ndio picha ilivyo katika shughuli za sanaa Tanzania. Na haswa katika mambo ya muziki na filamu.

Wasanii hufanya kazi ngumu ya kutunga na kufanya mazoezi kisha kurekodi kazi zao, kabala hawajafaidi kazi zao hukuta shamba lao likiwa linavunwa kwa njia mbalimbali. Wengine hurudufu kazi zao, wengine huzitumia kutangaza biashara zao. Wengine huzitumia kuhamasisha mikutano yao, wengine huziuza kwa kuwarekodia watu katika simu, katika yote haya mwenye shamba haoni mafao yoyote.

Kutokana na matumizi mengi ambayo yanaweza kutokana na kazi zilizotungwa, na kutokana na ugumu wa kudhibiti kazi hizi sheria zinazitwa za Hakimiliki hutumika katika kulinda maslahi ya mtunzi kwa upande mmoja na mtumiaji kwa upande mwingine.

Ulinzi wa hakimiliki umekuwa mgumu sana hapa nchini kwetu hasa kutokana na kuweko kwa utamaduni wa kutokuheshimu ubunifu wala sheria zinazolinda haki za ubunifu. Labda nitoe mfano, leo ukianzisha kibanda cha chips chenye mapambo tofauti na vingine, muda mfupi baadae mtaa mzima utajaa vibanda vinavyofanana na chako. Watu hawaoni shida kunakili ubunifu. Fundi seremala akibuni staili fulani ya makochi baada ya muda mfupi maseremala kila mahali wataiga staili hiyo ya makochi bila hata kuwaza kuwa wanaiba ubunifu.

Katika maeneo yote ya karibu ya vyuo na sehemu za elimu ya juu utakuta biashara kubwa ya mashine za fotokopi, kazi ya mashine hizi ni kurudufu maandiko na vitabu mbalimbali vya watu bila kujali kuwa waliotunga vitabu hivyo wanahitaji viuzwe ili wapate mafao yao.

Kwa masaa ishirini na nne kila siku redio na baadhi ya Tv hurusha hewani nyimbo za watu, tena kwa vipindi ambavyo hutangazwa wazi kuwa vimedhaminiwa na kampuni kubwa mbalimbali zenye kuheshimika. Vituo hivi vinamilikiwa na kuendeshwa na watu wanaoheshimika katika jamii kwa kuhamasisha vijana wajiajiri, lakini ikishafika kwenye eneo la kulipia matumizi ya kazi za wasanii kigugumizi kikubwa kinatokea.

Watetezi wa haki mbalimbali za wananchi wa Tanzania, watatetea kila haki lakini wakati wa kampeni zao watatumia kazi za wasanii na kuwa wagumu kulipia matumizi hayo. Wanasiasa wakiwa katika kampeni za kuwaeleza wananchi ni jinsi gani wakipata madaraka watatetea haki zao hutumia kazi nyingi za sanaa bila kuzilipia na wala hawaoni kuwa tayari kuna wananchi wanawanyanyasa kwa kutumia kazi zao bila kulipia.

Sheria za hakimiliki humpa mtunzi haki zifuatazo katika tungo zake;

(a) Kurudufu kazi

(b) Kusambaza kazi

(c) Kukodisha kazi

(d) Kutafsiri kazi

(e) Kubadili matum izi ya kazi

(f) Kuonyesha kazi hadharani-exhibition

(g) Kuifanya kazi hadharani-public performance

(h) Kutangaza kazi katika vyombo vya habari-broadcasting

(i) Kuwasilisha kazi kwa umma kwa njia yoyote

(j) Kuingiza kazi nchini

Mtunzi anaweza akaingia katika makubalianao na mtu mwingine ili kutumia moja au zaidi ya haki hizo ili kupata mafao yake.

Nadhani ukiangalia haki hizo hapo juu utaweza kuona jinsi haki za watunzi zinavyovyunjwa masaa ishirini na nne.

Ununuapo CD au DVD elewa kuwa umeipata kwa ajili ya matumizi yako binafsi, ukianza kuitumia kwa shughuli yoyote ile nyingine unaanza kuingilia haki zilizotajwa hapo juu. Hivyo basi kununua CD hakukupi haki ya kuanza kutoa nakala za CD hiyo, wala kuanza kuirusha redioni au kuipiga hadharani kwenye baa au hoteli, hapana, utahitaji kupata ruksa kuanza kutumia kwa kazi hizo za ziada. Ruksa hizi hupatikana kwenye Chama kinachoshughulika na mambo ya Hakimiliki Tanzania yaani COSOTA.

COSOTA hutoa leseni ambazo watumiaji wa kazi za muziki huzilipia na fedha zinazopatikana hugawiwa watunzi. Katika nchi ambazo taratibu hizi zinafanya kazi wanamuziki na wadau wengine wa muziki hupata fedha nyingi kutokana na matumizi ya kazi zao. Bado kuna tatizo kubwa la hili kwani kama nilivyosema utamaduni wa kudharau haki za watunzi bado ni mkubwa katika jamii ya Tanzania.

Jambo la kufurahisha ni kuwa tayari kuna wafanya biashara kutoka sehemu mbalimbali nnchini ambao wamekuwa wanalipia kwa matumizi ya kazi za muziki na COSOTA wamekwisha gawa fedha kwa mara ya saba kwa watunzi wa kazi mbalimbali.

Ili kupata watunzi bora na kazi bora za muziki ni muhimu kuhakikisha watunzi wanalindiwa haki zao na kila mpenda sanaa.

No comments:

Adbox