YOUTUBE PLAYLIST

Friday, October 8, 2010

The Upanga Story - The Strokers


The Strokers, hili lilikuwa kundi jingine la wanamuziki wa Upanga. The Strokers lilikuwa na awamu mbili, ya kwanza ilikuwa na wanamuziki akina Donald Max, David Max, Harry Chopeta, Vincet Chopeta, Pino Makame na Ochiwa na Freddy Lukindo. Awamu ya pili ya kundi hili ilikuwa na Sajula Lukindo,Onesmo Kibira,Innocent Galinoma,Ben Galinoma, Denis Pad,Francis Kasambala,Vicent na Harry Chopeta, Ally Mwarabu, Sabri Mmanga na wengineo. Pichani ni awamu ya kwanza ya Strokers. Waliosimama, Pino Makame, Freddie Lukindo, David Max. Waliokaa (?),Harry Chopeta, Vincet Chotepa.

Thursday, October 7, 2010

Upanga Story extra

Picha hii ina maana nyingi kwa wapenzi wa Groove Makers. Hapa ni wakali wawili wa GrooveMakers wakiwa katika mazoezi ya Karate. Hakuna zawadi kwa kuwataja japo itakuwa vizuri kupata taarifa ya kipindi hiki

Thursday, September 30, 2010

Sikujua kama utabadilika - Simba wa Nyika


Wengi tunaufahamu wimbo Sikujua Kama Utabadilika, wenye maneno yafuatayo....
Ohhh Sikujua kama utabadilika
Ohhh Ulimwengu kweli una mambo mengi
Baki salama oo kuonana nawe ni majaliwa
Chorus
Utalia utalia ooo usinione, Mombasa mbali, Kakamega mbaali......................
Wimbo huu ulitungwa na Wilson Peter kama kijembe, baada ya mpiga rythm wa Simba Wa Nyika, Prof. Omar Shaaban kwenye mwaka 1978 kuondoka na karibu kundi zima la Simba wa Nyika na kwenda kuanzisha Les Wanyika ambao nao waliokuja na vibao vikali sana katika album yao ya Sina Makosa.

Tuesday, September 28, 2010

Western Jazz Band 2 (Rashid Hanzuruni)

Rashid Hanzuruni, kama ilivyo watu wote walio mahiri katika vyombo vyao vya muziki alilipenda gitaa lake na alifanya mazoezi kila alipopata muda. Kwa maelezo ya mtu aliyekuwa karibu nae alisema huyu bwana kuna wakati dansi likisha isha watu wanaenda kulala yeye aliwasha tena mashine na kuanza mazoezi ya gitaa. Kuna hadithi ambayo hata mimi niliiamini kwa miaka mingi kuwa Doctor Nico alipokuja Tanzania alimuulizia Hanzuruni, hadithi hii si ya kweli. Kwa malezo ya mtu aliyekuweko kipindi hicho, Western Jazz walialikwa kupiga pamoja na Dr Nico alipokuja Tanzania kati ya mwaka 66 na 67, na katika maonyesho hayo, kwanza Hanzuruni ndipo alipomuona Dr Nico kwa karibu na kupenda staili ya upigaji wake, na pia ndipo alipomuona Dr Nico akipiga Hawaian Guitar, nae akalipenda na Western Jazz wakalinunua na Hanzuruni akawa mpigaji wa kwanza Mtanzania wa gitaa la hawaian,baada ya hapo Hanzuruni alifanya sana mazoezi ili aweze kupiga gitaa kama Dr Nico. Ni vizuri kulisema hapa kuwa Hanzuruni ndie alikuwa mwanamuziki aliyelipwa vizuri kuliko mwanamuziki yoyote wa Dar Es Salaam wa aina yake, katika kipindi hicho.

Monday, September 20, 2010

Western Jazz Band



Mzee Iddi Nhende ndiye aliyepata wazo la kuanzisha bendi maarufu ya Western Jazz. Iddi Nhende alianza muziki akiwa bado mdogo katika bendi ya shule alipokuwa Primary huko Nzega, mwaka 1944 alijiunga na Tabora Boys Secondary na hapa akajiunga na Brass Band ya shule ambapo alikuwa mpigaji wa Cornet. Alimaliza shule na kuja Dar es Salaam kujiunga na Chuo cha Afya, Sewa Haji Medical Training Center. Baada ya kumaliza mafunzo akaajiriwa Bohari ya madawa na kisha mwaka 1957 alihamishiwa Muhimbili. Upenzi wake wa muziki ulimfanya mwaka huohuo ajiunge na Rufiji Jazz Band kama mpiga trumpet, bendi hii wakati huo ilikuwa ikifanya maonyesho yake Minazini Community Centre iliyokuwa eneo linaloitwa siku hizi Mchikichini na pia walikuwa wakipiga muziki katika ukumbi wa Arnatougro.

Kutokana na miji kuwa ndio ilikuwa inaanza, watu wengi kutoka maeneo mbalimbali walihamia mijini na kujaribu kutafuta wenzao waliotoka sehemu moja na kuwa na vikundi vya kusaidiana au kuwaunganisha, watu wa sehemu mbalimbali walianzisha bendi wakazipa majina ya wanakotoka, hivyo waanzilishi wa Rufiji Jazz walitoka Rufiji, na ndivyo ilivyokuwa kwa Kilwa Jazz, Ulanga jazz na kadhalika. Hivyo Iddi Nhende aliyekuwa ametoka Nzega akaamua kuanzisha bendi ya watu kutoka Magharibi, kwa kuwa nchi ilikuwa imegawanywa katika majimbo, yakiweko majimbo kama Northern Province, Southern Highlands Province, Western Province na kwa vile Nhende alitoka Western province akaanzisha Western Jazz Band 1959. Akanunua vyombo aina ya Grampian toka duka la Souza Junior duka la vyombo vya muziki lililokuwepo mtaa wa Mkwepu. Aliweza kupata fedha baada ya kuuza ng’ombe kadhaa wa mamake. Wakati huo katika bendi za aina yake ni Dar es Salaam Jazz Band peke yake waliokuwa na magitaa ya umeme, hivyo Nhende akawa na kazi ya kuwatafuta wapigaji ambapo alimfuata mpiga gitaa la umeme wa kwanza Haus Dibonde(Msukuma), aliyekuwa anapigia Dar es Salaam Jazz Band(hii ilikuwa chini ya Mzee Muba), baada ya hapo akawapata wanamuziki wengine kutoka Ulanga Jazz Band, wakati huo chombo cha banjo kilikuwa muhimu hivyo akamtafuta mpiga banjo toka Cuban Marimba tawi la Dar es Salaam. Cuban Marimba wakati huo ilikuwa na tawi Dar Es Salaam lililokuwa chini ya Mzee Mwaipungu. Mwaka mmoja baadae alipata transfer ya kwenda Morogoro, hivyo huku nyuma alilazimika kuongeza wasanii ili kuimarisha bendi wakati hayupo. Akampata David Makwaya mwimbaji, na Ally Rashid(huyu ameacha muziki karibuni akiwa Msondo), mpiga Saxaphone toka Zanzibar. Bahati mbaya yule mpiga gitaa Haus akapata kichaa katika mazingira yaliyohusishwa na ushirikina kutokana na ushindani wa bendi uliokuwepo. Hivyo basi walifuatwa wanamuziki watatu toka Tabora Jazz, wanamuziki hao walikuwa wametoka pamoja katika bendi iliyokuwa na makazi Mwanza ikiitwa Kimbo Twist Band na wakahamia Tabora Jazz, na kutoka hapo wakachukuliwa na Western Jazz. Wanamuziki hao walikuwa

Rashid Hanzuruni, Kassim Mponda na Omary Kayanda. Baada ya kazi nzuri sana, Hanzuruni Nae akarukwa na akili katika mazingira yale ya yule mpiga solo wa kwanza akalazimika kurudishwa Tabora ambako alikaa mpaka mauti yake. Wema Abdallah akachukua nafasi ya mpiga solo katika bendi ya Western. Tatizo la kinidhamu lilifanya Wema aondolewe Western, na mpigaji mwingine mzuri sana Shamba Abbdallah akachukua nafasi, solo la huyu bwana linasikika kwenye nyimbo ka Rosa na kadhalika.

Hall la nyumbani la Western Jazz lilikuwa Alexander Hall, ambalo lilikuja kuwa hall la DDC Kariakoo. Western walinunua drums baada ya Kilwa Jazz kununua drums na kuzipitisha kwao kuwaringia. Walinunua toka kwa bendi moja ya Wagoa iliyoitwa De Mello Brothers. Western walirekodi santuri kadhaa chini ya mkataba waliyousaini na lebo ya Phillips ya Kenya. Hatimae Western na mtindo wao wa Saboso walitoweka katika anga za muziki miaka ya mwisho ya sabini. Kati ya nyimbo zao nyingi ni hizi hapa; Rosa, Vigelegele, Jela ya Mapenzi, Helena no 1 na 2.

Tuesday, September 14, 2010

Maneno Uvuruge 2


Katika kipindi ambapo Maneno Uvuruge alikuwa akipigia Super Rainbow ndipo Eddy Sheggy na Emma Mkello walipojiunga, hawa hukumbukwa sana kwenye bendi hii kwa ajili ya ule wimbo Milima Ya Kwetu, pia nae Banza Tax akajiunga kipindi hiki. Na kule Mabibo bendi ya Mambo Bado ilipata msukosuko na kuvunjika kwa mara ya kwanza na hivyo wanamuziki wake Juma Choka mpiga drums, Lodji Mselewa na Nana Njige pia wakajiunga na kundi na Super Rainbow, lakini hawakukaa sana Assossa aliweza kuifufua tena Mambo Bado na wote wakarudi wakifuatana na Maneno Uvuruge. Lakini tayari bendi ilikuwa iko katika hali mbaya kwani Assossa aliacha tena akiwa katika harakati ya kuunda bendi mpya na Mambo Bado ikafa rasmi. Juma Choka akamtaarifu Maneno kuwa Urafiki Jazz kuna nafasi ya kazi na hapo akenda na kusailiwa na Ngulimba wa Ngulimba, Marehemu Mzee Juma Mrisho, Urafiki nayo ilikuwa katika siku zake za mwisho lakini bado yule mpiga solo mahiri Michael Vicent alikuweko. Kipindi hiki pia waliingia Mohamed Gota gota na Hussein Jumbe. Maneno Uvuruge sasa alianza kufahamika kwa wanamuziki wengine kuwa ana uwezo mkubwa na bendi zikaanza kumsaka, na kuanzia hapo amekuwa hatafuti kazi bali anatafutwa. Bendi ya kwanza kumchukua ilikuwa ni Maquis, alichukuliwa ili awe mpiga gitaa la rhythm, aliwakuta wapiga rhythm wawili, huko, Mbwana Cox na Makuka. Akawa mwanamuziki wa Maquis wakati huo wapiga solo wa bendi hiyo walikuwa ni Nguza Viking, na Mzee Lubaba.

Mwanamuziki Belly Kankonde akakutana na Marehemu Mzee Mwendapole na kuamua kuipa uhai bendi ya Afrisongoma. Kankonde akawashawishi wanamuziki wenzie wanne wa Maquis, Maneno Uvuruge (guitar),Kiniki Kieto(mwimbaji), Comson Mkomwa(saxophone) na Keppy Kiombile(bass) wakahamia Afrisongoma. Maneno hakukaa muda mrefu kwani Nguza alimfuata yeye na Comson na kuwarudisha Maquis , na kwa kuwa walikuwa wamekwishapokea fedha za Mzee Mwendapole kesi ilifika polisi na ikalazimu Maquis warudishe fedha hiyo. Lovy Longomba alijiunga na Maquis nae hakukaa muda mrefu Mwendapole akamshawishi akaunde upya kundi la Afrisongoma ambalo katika awamu ya kwanza liliishia kurekodi mara moja na kutokuwa na maendeleo. Lovy pia tena akamuondoa Maneno na kuhamia nae Afrisongoma.

Wakati huo Mosesengo Fan Fan yule mpiga gitaa mahiri aliyetoka kwa Franco na kupigia Matimila na Makassy alikuwa amehamia Uingereza na akawa amemtaka Kiniki Kieto awashawishi Maneno Uvuruge, Keppy Kiombile, na Vivi Kapaya wamfuate,lakini mpango huo uliishia kwa Kiniki na Vivi kuendelea na Fanfan wakati Maneno na Keppy wakahamia Afrisongoma wakiwa na Lovy. Wanamuziki kadhaa walihamia Afriso wakati huo wakiwemo Kalamazoo, na Mzee Mponda ambae baada ya kutoka Msondo alikuwa kapita Sikinde na akatua Afrisongoma. Na hapo ndipo msondo wakamchukua Maneno kwa mara ya kwanza. Alikaa kwa muda na rafiki zake akina Benno Vila Anthony wakaweza kumshawishi ahamie Sikinde. Baada ya muda si mrefu Nguza akamfuata ili kumshawishi ajiunge na Orchestra Sambulumaa. Ilikuwa ni ushawishi wa Skassy Kasambula na Emmanuel Mpangala aliyekuwa mkurugenzi wa bendi ndio ulioweza kumfanya Maneno ahamie Sambulumaa (itaendelea………) (Pichani...Keppy Kiombile Bass, Maneno Uvuruge Rythm, Makuka Second solo, Juma Choka Drums, Lubaba Solo....)

Saturday, September 11, 2010

Maneno Uvuruge



Maneno Uvuruge ni moja ya wanamuziki waliotoka katika familia ya wanamuziki ya ukoo wa Uvuruge. Kaka zake Jumanne, Stamili, na Huluka ni kati ya wapiga magitaa walioheshimika sana katika jamii ya wanamuziki wa bendi Tanzania.

Jumanne Uvuruge ambae alikuwa mkubwa wa akina Uvuruge wote, ndie aliyetunga kibao maarufu cha Georgina, kilichopigwa na Safari Trippers na kuimbwa na Marijani Rajabu. Siku zake za mwisho za maisha Jumanne alikuwa anajishughulisha na kupata riziki yake kwa kuzunguka katika mabaa mbalimbali na gitaa na kupiga maombi mbalimbali ya wanywaji, na kisha kuhama na kuelekea baa nyingine. Hayakuwa maisha rahisi.

Maneno Uvuruge hana kumbukumbu ya jinsi gani Jumanne alijifunza gitaa, lakini anajuwa kuwa Stamili alifundishwa na Jumanne. Anakumbuka zaidi jinsi Huluka alivyojifunza kwani ndie alikuwa kaka yake waliefuatana kuzaliwa. Huluka alijifunza gitaa kwa kuanza kuchonga gitaa lake mwenyewe, aliiba mishipi ya kuvulia ya baba yake na ndio zikawa nyuzi za gitaa lake, siku babake alipogundua wizi huo alivunja vunja gitaa na kumkataza asiguse mishipi yake tena, lakini akamwelekeza inakonunuliwa, Huluka alitafuta pesa na kwenda kununua mishipi na kuendelea na gitaa lake la kopo. Wakati huo Huluka alikuwa anasoma, naye Maneno akaanza hamu ya kutaka kujua kupiga gitaa akawa anaiba gitaa la kaka yake kila alipoenda shule, ilikuwa ni ugomvi kila alipokata nyuzi kwani alikuwa bado anajifunza. Jumanne na Stamili wakaanza rasmi kumfundisha gitaa Huluka nae akalijua vizuri sana. Si muda mrefu baadae nae akaanza rasmi kumfundisha mdogo wake. Maneno anasema wimbo wa kwanza kakake kumfundisha ni ile rhythm ya wimbo Novelle Geneation wa Orchestra Lipualipua, wimbo huu ulikuwa ni kipimo muhimu kwa wapiga rythm enzi hizo. Freddy Benjamin ndie aliyemshauri kujiunga na Bendi. Alimkaribisha UDA Jazz ambako alikuwa akiimbia na pamoja na kuweza kupiga gitaa alifanyiwa mizengwe na mpiga rhythm aliyekuweko na ambae pia alikuwa katibu wa bendi. Freddy alimuombea kazi Super Rainbow iliyokuwa na makao yake makuu pale Sunlight Bar Mwananyamala B. Na hapo akakutana na wanamuziki kama Hatibu Iteytey, Nuzi Ndoli, Rocky, Mzee Bebe, Akina Eddy Sheggy walikuwa bado hawajajiunga na bendi hii wakati huo.(Picha ya juu akiwa na Mohamed Shaweji, ya chini akiwa na Mawazo Hunja)

Thursday, September 9, 2010

Kassim Mponda

Kassim Mponda alikuwa mmoja ya wapiga gitaa mahiri hapa Tanzania. Kama unakumbuka wimbo utunzi wa Kakere, wa Sogea Karibu uliopigwa na JUWATA ambao pia ulipambwa na kinanda cha Waziri Ally aka Kissinger, basi lile ndio solo la Kassim Mponda. Kwa kifupi alianzia Nyanyembe Jazz, akahamia Tabora Jazz,na kupitia Police Jazz Band Wana Vangavanga, Safari Trippers ,mbapo alihama na wenzie na kuanzisha Dar International, kisha akahamia Msondo, akapitia Shikamoo Jazz, hatimae mwanae akamnunulia vyombo akanzisha bendi yake mwenyewe Afriswezi. Mpaka mauti yake mwezi June 2002. Wanaoikumbuka Police Jazz, imekuwa nayo ni Band ya miaka mingi ambayo wanamuziki wengi maarufu walipitia huko,ni muhimu kuja kuongelea bendi za majeshi na mchango wake katika muziki wa Tanzania.

Wednesday, September 8, 2010

Kuanzishwa kwa Mlimani Park Orchestra

Sababu ya Mlimani Park kuzaliwa ikiwa imeundwa na kundi kubwa la wanamuziki kutoka Dar International ilitokea kwa bahati sana. Kwa maelezo ya mwanamuziki aliyekuwepo wakati huo, hadithi nzima ilitokana na bendi ya Dar International kukodishwa na Chuo Cha Ardhi katika sherehe yao ya kuwaaga wanachuo wazamani na kukaribisha wapya. Chuo cha Ardhi kilikodi ukumbi wa Mlimani Park kwa ajili ya shughuli hiyo. Wakati huohuo utawala wa Mlimani Park ulikuwa mbioni kutengeneza bendi baada ya kumalizika mkataba wa Orchestra Fukafuka katika ukumbi huo. Tchimanga Assossa ambaye alikuwa amekuja na Bendi ya Fukafuka alibaki nchini na alikuwa katika hatua za mwisho za kwenda kufuata wanamuziki wengine kutoka Kongo kwa ajili ya ukumbi huo. Hivyo basi Dar International wakati huo ndio wakivuma na nyimbo kama Magreti walianza kuporomosha muziki chini ya kiongozi wao Abel Balthazal. Uongozi wa Mlimani Park ulipigwa butwaa na muziki wa hawa jamaa, Abel aliitwa pembeni na kuulizwa bendi iko chini ya mkataba wa nani? Na je, wanamuziki wangeweza kukubali kuajiriwa na na Mlimani Park wakati huo ikiendeshwa na TTTS? Kwa vile Dar International ilikuwa ya mtu binafsi na hawakuwa na ajira yoyote ya kudumu katika bendi hiyo, haraka sana wanamuziki walikubali wazo hilo. Kesho yake viongozi wa Dar International walienda kukutana na viongozi wa ukumbi wa Mlimani Park, na wakakubaliana kuazisha kambi ya bendi mpya palepale katika ukumbi wa Mlimani. Haikuwa taabu maana vyombo vilivyonunuliwa wakati wa mkataba wa Orchestra Fukafuka vilikuwa mali ya Mlimani Park kwa hiyo bendi ilianza kwa Abel kusisitiza kupata wanamuziki kama Muhidin Gurumo,ikumbukwe kuwa ni huyu Abel ndiye aliyeisuka Dar International baada ya kuwachukua wanamuziki wote wa Safari Trippers kundi zima wakati huo, Kassim mponda, Joseph Bernard, Marijan Rajabu, Ben Peti, Zito Mbunda,Bito Elias na wengine kasoro Christian Kazinduki na kutoka Tanzania Stars ya Maggot walitoka Joseph Mulenga, George Kessy , Haruna Lwali na wengineo. Na kwa staili hiyohiyo skwadi nzima ya Dar International ikageuka kuwa Mlimani Park. Muda mfupi kabla la hili ugomvi mkubwa ulikuwa umetokea Dar International kati ya Marijani Rajabu na Abel Balthazar katika ubishi kuhusu tungo aliyoleta Marijani ambayo Balthazar alidai kuwa ni ya Tabu Ley kwa hiyo akatunge tena, jambo lililoleta kushikana mashati, na kusababisha Marijani kusimamishwa kazi. Wakati yuko benchi ndipo mpango mzima wa kuhamia Mlimani ulifanyika hivyo mwenye vyombo alilazimika kumfwata tena Marijani na kumwomba aunde bendi upya, na ndipo Super Bomboka ikaundwa.

Mlimani Park ikaanza ikiwa na Tchimanga Assossa ambaye safari ya kwenda kutafuta wanamuziki Kongo ikawa imekwisha. Na mchango wa kudumu wa Assossa wakati huo ni utunzi wa ule wimbo Gama.

Saturday, September 4, 2010

The Upanga Story-Autographs

Utamaduni wa Autograph ulikuwa maarufu sana kwa vijana wa enzi hizo, kwa bahati tuu niliweza kupata kurasa chache za Autograph za vijana wa Upanga sitayataja majina ya wahusika kwa sababu nyingi sana chini ni maelezo yaliyokuwa kwenye autograph hizo, ukizisoma zina eleza mengi kuhusu hali ya wakati huo;
Drink: Coke
Food: Ugali
Clothes:boo-ga-loo
Singers: James Brown
Showbiz Personalities:Guliano Gemma
Records: The Chicken
Girl: "X"
Boy:Groove Maker
Place: Mchikichi
Best Ambition: Music (Drumer)

Drink: Babycham
Food: Tambi + Rice
Clothes: Pecos(bell-bottom)
Singers: James Brown, Clarence Carter,Otis Redding
Showbiz Personalities:Sidney Poitier,Elvis Presley,Franco Nero
Records: If I ruled the world,Thats how strong my love is, Take time to know her,
Girl: The one who loves me
Boy:Groove Maker
Place: Soulville Upanga
Best Ambition: Secret Agent

Drink: Fanta
Food: Chapati
Clothes:boo-ga-loo
Singers: Percy Sledge,James Brown
Showbiz Personalities:Fernando Sancho, Lee Marvin
Records: Take time to know her, Sex Machine Blue Transistor Radio
Girl: Fikirini
Boy:Groove Maker
Place: Soulville Upanga
Best Ambition: Electrician

Tuesday, August 31, 2010

The Upanga Story


Upanga ni eneo muhimu sana katika historia ya muziki Tanzania. Hata katika miaka ya karibuni kulizuka kilichoitwa East Coast, muungano fulani wa wasanii wa Bongoflava toka maeneo ya Upanga, hii haikuwa mara ya kwanza kwa Upanga kuwa na wanamuziki waliotingisha mji. Enzi hizo za muziki wa soul, vijana wa Upanga walilipa eneo hili la mji jina la Soulville.Kwenye kona ya barabara ya Mindu na United Nations, nyumbani kwa familia ya Jengo, hapo ndipo palikuwa mahala pa mazoezi pa kundi lile la Groove Makers. Baadhi ya wanamuziki wa kundi hili walikuwa Mohamed Maharage, Joseph Jengo, Emmanuel Jengo, Herbert Lukindo, Willy Makame, na mpiga Drums ambae mpaka leo yupo katika anga za muziki Jeff. Kipindi hiki kilikuwa ni wakati wa muziki wa soul na kundi hili lilikuwa kundi la ubora wa juu wakati huo. Upanga ilikuwa na kundi jingine The Strokers, hili lilikuwa na awamu mbili, awamu ya kwanza ilikuwa na wanamuziki akina Donald Max, David Max, Harry Chopeta, Vincet Chopeta, Pino Makame na Ochiwa na Freddy Lukindo. Awamu ya pili ya kundi hili lilkuwa na Sajula Lukindo,Onesmo Kibira,Innocent Galinoma,Ben Galinoma, Denis Pad,Francis Kasambala,Vicent na Harry Chopeta, Ally Mwarabu, Sabri Mmanga na wengineo. Barlocks ni Bendi nyingine iliyochipukia Upanga, jina la Barlocks lilitokana na kuweko kwa kundi la Barkeys ambalo leo linaitwa Tanzanites. Barlocks walikuwa wakitumia vyombo vya Barkeys kwani kwa wakati huo bendi hizi zilikuwa kama mkubwa na mdogo. Barlocks hiyo ya awamu ya kwanza ilikuwa na wanamuziki akina Jimmy Jumba,Pimbi Sokoine, huyu alipewa jina la utani Pimbi kutokana na kuwa mrefu sana, Said Mbonde kaka yake Amina Mbonde mwanamuziki mwingine muimbaji,Sajula Lukindo, Abraham. Kulikuweko na makundi mengine mengi hapo Upanga, kama White Horse, Aquarius hapa walikuweko producer maarufu Hendrico Figueredo, Joe Ball,Joel De Souza, Mark De Souza,Roy Figueredo, Yustus Pereira,Mike De Souza. Baadhi ya wanamuziki wake walienda na kuungana na wengine Arusha na kuvuma sana na kundi la Crimson Rage, baadae wakarudi Dar na kujiita Strange. Baadhi ya kumbi walizokuwa wakipiga zilikuwa DI, Marine,Gymkhana,Maggot, St Joseph na kwenye shule mbalimbali.
(Picha ya juu-Emmanuel 'Emmy' Jengo, Joseph 'Joe' Jengo, Herbert 'Herby' Lukindo. Kati-Jeff 'Funky' nyuma yake ni Willy Makame. Picha ya chini Willy Makame)

Thursday, August 26, 2010

Marijani Rajabu

Marijani Rajabu kwa vyovyote ni mmoja wa wanamuziki ambao wametoa mchango mkubwa katika ulimwengu huu wa muziki. Japo ni miaka mingi toka mauti yake yalipomfika, bado nyimbo zake zinapigwa na wanamuziki mbalimbali majukwaani na hata kurudiwa kurekodiwa tena. Marijani alizaliwa maeneo ya Kariakoo mwaka 1954. Mama yake alikuwa mama wa nyumbani wakati baba yake alikuwa na shughuli za uchapishaji. Maisha yake ya utoto yalikuwa ya kawaida ila alikuwa kipenda sana uimbaji wa Tabu Ley na mwimbaji mmoja wa Guinea Sorry Kandia. Alilelewa vizuri kwa misingi ya dini ya Kiislam kwa hivyo alihudhuria mafunzo ya dini utotoni kama inavyotakiwa. Akiwa na umri wa miaka 18 hivi, alijiunga na STC Jazz, ikiwa chini ya mpiga gitaa maarufu wakati huo Raphael Sabuni, kabla ya hapo bendi hii ilikuwa unajulikana kama The Jets. Katika bendi hii Marijani aliweza kutoka nje ya Tanzania kwa mara ya kwanza ambapo alikwenda Nairobi na kurekodi nyimbo zilizotoka katika label ya Phillips. Mwaka 1972 Marijani alihamia bendi ya Safari Trippers. Hapa ndipo ubora wake ulifunguka haswa na kuweza kuinyanyua Safari Trippers kuwa moja ya bendi maarufu za wakati huo. Waliweza kutoa vibao vilivyopendwa mfululizo na kuweza kuzunguka nchi nzima. Vibao kama Rosa nenda shule, Georgina,Mkuki moyoni, viliweza kuuza zaidi ya nakala 10000 za santuri na hivyo kuwezesha bendi kuwa na vyombo vyake vizuri. Bendi wakati huo ikiwa na wanahisa wanne, ambao kwa bahati mbaya wakati bendi ndio iko juu, wakakosa kuelewana na ukawa ndio mwisho wa bendi hiyo. Miezi michache baadae Marijani na wenzie waliibukia Dar International. Pia huku kulikuwa na wanamuziki wazuri na haraka bendi ilipata umaarufu wa hali ya juu kwa vibao vyake kama Zuena na Mwanameka. kutokana na hali wakati huo bendi ilirekodi vibao hivi RTD na kuambulia sh 2500/- tu. Kilichosikitisha zaidi ni kuwa nyimbo zao tisa ziliuzwa kwa kampuni ya Polygram bila ridhaa yao. Kati ya mwaka 1979 na 1986 bendi ilipiga karibu kila wilaya nchi hii na kufurahisha sana watu na mtindo wao wa Super Bomboka. Uchakavu wa vyombo hatimae mwaka huo 1986, ukamaliza mbio za bendi hii. Kwa miezi michache Marijani akashiriki katika lile kundi kubwa la wanamuziki 57 waliotengeneza Tanzania All Stars, kundi hili lilirekodi vibao vinne ambavyo si rahisi kwa bendi zilizopo sasa kufikia ubora wake kimuziki. Marijani alipitia Mwenge Jazz kw muda mfupi, na kukaa kama mwaka mmoja Kurugenzi Jazz ya Arusha, kisha akajaribu kuanzisha kundi lake la Africulture na mtindo wa Mahepe lakini kwa ukosefu wa vyombo mambo hayakuwa mazuri. Kufiki1992 hali ya Marijani ilikuwa ngumu akiishi kwa kuuza kanda zake ili aweze kuishi.Pamoja na nyimbo nyingi, za kuimbia Chama tawala na serikali, na hata tungo yake Mwanameka kutumiwa katika mtihani wa kidato cha Nne. Rajabu Marijani hajawahi kukumbukwa rasmi kama mmoja wa wasanii bora Afrika ya Mashariki

Wednesday, August 25, 2010

Blog Mpya ya haki za wasanii Tanzania

Nimekuwa napewa changamoto kubwa kuhusu namna ya kusaidia wasanii wenzangu katika mapambano yao ya kupata haki kutokana na kazi zao mbalimbali walizorekodi au kushiriki. Hivyo basi nimeanzisha blog inayoitwa Wasanii wa Tanzania na Haki Zao ambapo patakuwa jukwaa la kutoa elimu kuhusu haki kama vile Hakimiliki, mikataba ya kazi mbalimbali, pia sehemu ya kupeana maoni na taarifa mbalimbali kuhusu biashara nataratibu nzima za shughuli za sanaa hapa nchini Tanzania. Nategemea wadau mtaweza kuchangia maoni na kuitangaza ili iwe kweli chombo muhimu kwa wasanii wa Tanzania

Saturday, August 21, 2010

Kinguti System


Ramadhan Maulid Kinguti maarufu kama Kinguti System ni mzaliwa Ujiji, Kigoma.
Bendi yake ya kwanza ilikuwa Super Kibissa ya Kigoma.
Super kibissa ni bendi iliyoanziswa 1968 na Kinguti akajiunga nayo mwaka 1977. Wakati huo kiongozi wa bendi alikuwa Mlolwa Mussa Mahango ambaye alikuwa ni binamu yake Kinguti. Bendi ilikuwa mali ya watu watatu, Gollo Saidi, Haruna Mahepe, n Maulidi. Kinguti alitunga nyimbo kadhaa katika bendi hii kwa mfano-Kazi ni uhai, Mapenzi tabu,na Zaina. Mwaka 1979 alichukuliwa na Ahmed Sululu ambae alikua katibu wa Dodoma International na kuhamia Dodoma, ililazimika Dodoma International wamchukue kujaza nafasi ya Shaaban Dede ambaye alikuwa kahama Dodoma International na kuhamia JUWATA. Katika bendi hiyo alikutana kwa mara ya kwanza na mpiga gitaa mahiri Kassim Rashid. Baada ya hapo alihamia Orchestra Makassy ambapo wakati huo walikuweko wanamuziki akina Marehemu Masiya Raddi ambaye alifariki kwa kukanyagwa na daladala, Doctor Remmy, Andy Swebe, Keppy Kiombile, John Kitime, Issa Nundu, Kyanga Songa, Choyo Godjero na wengineo, pia alikuweko Mzee Aimala Mbutu kwenye solo, na Kassim Mganga kwenye rhythm. 1986 alijiunga Afrisso ngoma chini ya Lovy Longomba, hapa alitunga nyimbo sita, Pesa ni maua, Amana mpenzi, Estah Usituchonganishe, waimbaji wakati huo walikuwa Kinguti, Lovy na Anania Ngoliga,kwenye solo alikuweko mzee Kassim Mponda, na rhythm Maneno Uvuruge, Kwa muda mfupi alikuwa DDC Mlimani Park, na hapa akatunga kile kibao maarufu Visa vya mwenye nyumba, ambapo aliimba na Hassan Bitchuka, Francis Lubua,Hussein Jumbe na Benno Villa. Mwaka 1989 alikuwa moja ya wanamuziki waanzilishi wa Bicco Sound, wakiwa na Mafumu Bilali, Asia Darwesh, Andy Swebe, Mzee Aimala Mbutu, walitikisa na vibao kama Muuza chips, Leyla, Magreth maggie, Kitambaa cha kichwa, Nyumba ya kifahari, na nyingine nyingi tu. 1999 alijiunga na kilimanjaro Connection, alikaa bendi hii na Kanku Kelly kwa miaka miwili kisha kuanzisha bendi na akina Hassan Shaw The Jambo Survivors ambayo yupo mpaka leo

Vijana Jazz enzi za Ngapulila




Kati ya awamu nyingi za Vijana Jazz Band moja iliyoleta changamoto na furaha ni ile awamu ya nyimbo , Ngapulila, Ogopa Tapeli, Adza. Pichani baadhi wa wanamuziki wa wakati huo. Picha ya kwanz a juu- Mzee Joseph Nyerere akiwa na Kulwa Milonge na Hamis Mnyupe, picha ya pili wapiga trumpet marehemu Chondoma, Hamis Mnyupe, na Kulwa Milonge. Picha ya chini ni kundi zima la Vijana Jazz wakiwa na Mheshmiwa Seif Khatib, hapa wanaonekana akina Shaaban Dogodogo, Hemed Maneti,Shaaban Wanted, Abou Semhando na wengine wengi.Kama unavyoona alama za x wengi hawapo tena nasi duniani.

Wednesday, August 18, 2010

Shaw Hassan Shaw


Kwa wapenzi wa Vijana Jazz wanakumbuka vile vipande vya keyboards vilivyokuwa vikianzisha zile nyimbo mbili alizokuwa akiimba Kida Waziri, Penzi Haligawanyiki na Shingo feni, mpigaji wake alikuwa Shaw Hassan Shaw Rwamboh. Mwanamuziki huyu alizaliwa

tarehe 25/sept/1959, Dar Es Salaam. Alianza kujifunza kupiga gitaa na wenzie kando ya Ziwa Tanganyika huko Kigoma, wakitumia magitaa ya tajiri mmoja aliyekuwa na meli ya uvuvi. Aliporudi Dar es Salaam akakutana na mwanamuziki Zahir Ally Zorro, Zahir ndiye aliyeboresha upigaji wake wa gitaa kiasi cha kukubaliwa na Patrick Balisidya kupiga gitaa la rythm katika bendi yake ya pili PAMA Band, chini ya Afro70.

Ni chini ya malezi ya Patrick alipojifunza kupiga Keybords (Kinanda). Baada ya hapo aliacha muziki na kujiunga na Dar Technical College. Lakini 1980 alijiunga na Vijana Jazz kama mpiga Keyboards, alishirikiana na wanamuziki wengi lakini wengi pia wametangulia mbele ya haki. Waliobaki kati ya aliyokuwa nao wakati huo ni John Kitime, Abuu Semhando, Kida Waziri, Saad Ally Mnara, Hamisi Mirambo, Hassan Dalali, Hamza Kalala na Rashid Pembe. Mwaka 1990 alijiunga na Orchestra Safari Sound, chini ya Maalim Muhidin Gurumo (MJOMBA), na Marehemu Abel Baltazar , hapa alikutana na wanamuziki kama Benno Villa Anthony na Mhina Panduka (Toto Tundu) .Aliacha bendi baada ya miezi sita tu, mwenyewe anasema, ‘….kutokana na muhusika kutozingatia mkataba wangu…’. Alihamia Zanzibar na kujiunga na bendi iliyokuwa ikipiga Mawimbini Hotel, hakukaa sana kwani Washirika Tanzania Stars walimwita. Hapa akakutana na Zahir Ally, Ally Choki Rwambow, Musemba wa Minyugu,Tofi Mvambe, Abdul Salvador na wengine, ilitokea kutoelewana baina ya wanamuziki na yeye kama kiongozi wa bendi ilibidi aachie ngazi kuepusha bendi kuzidi kujichanganya. Baada ya hapo Kanku Kelly ambaye ni mume wa dada wa mke wake alimuita ajiunge na Kilimanjaro Connection Band. Anasema Kanku alimvumilia sana kwa kuwa alikuwa hajawahi kufanya kazi ya kukopi nyimbo za wanamuziki wengine wakubwa duniani, pili hii bendi ilikua inazunguka kwa kupiga muziki hotel mbalimbali Malaysia,Singapore, Indonesia,Thailand na Japan jambo ambalo lilifanya aone kila kitu ni kigeni. Katika bendi hiyo alishirikiana na akina Kanku Kelly, Mafumu Bilal, Maneno Uvuruge, Burhan Adinan, Shomari Fabrice, Bob Sija, Fally Mbutu, Raysure boy,Delphin Mununga na Kinguti System. Baadaye Shaw, Kinguti na Burhan Muba waliamua kuanzisha kundi dogo wakitumia sequencer keyboards na kumuaga Kanku Kelly. Group hiyo ilijiita Jambo Survivors Band, itakumbukwa kwa ule wimbo Maprosoo uliokuwa katika album ya MAPROSOO. Baada ya hapo bendi ikaanza kuzunguka nchi mbalimbali ikipiga katika mahotelini. Wameshapita Oman , Fujairah, U.A.E, Singapore, Malaysia na sasa wapo Thailand. Shaw anasema wanamuziki ambao hatawasahau kwa kuwa wamemfikisha alipo ni Zahir Ally Zorro, Marehem Patrick Balisdya, Waziri Ally, Kinguti System, Burhan Muba na Kanku Kelly. Kituko ambacho hawezi kusahau ni nchini Malasyia akiwa na Kanku Kelly kwa mara ya kwanza kupiga muziki akiwa amezungukwa na watu weupe Anasema nyimbo zote zilipotea kichwani akawa hakumbuki hata nyimbo moja.

(Picha ya juu Burhan Muba, Kinguti System ,Hassan Shaw, ya chini ni Vijana Jazz, Hassan Shaw wa mwisho kulia)



Tuesday, August 3, 2010

Lister Elia














Huyu ni mwanamuziki mpiga keyboards, zao la Dodoma, kule alikotoka Patrick Balisdya, Anania Ngoliga, Rahma Shally na wengi wengine. Lister mtoto wa mchungaji atakumbukwa sana kwa kazi yake katika bendi ya Sambulumaa lakini baada ya hapo alipitia Afriso Ngoma ya Lovy Longomba na Orchestra Safari Sound wale vijana wa Kimara, na hatimae akatua MK Sound(Ngoma za Magorofani). Hiyo ilikuwa baada ya wanamuziki akina Andy Swebe, Mafumu Bilali, na Asia Darwesh kuhamia Bicco Sound, alitua huko wakati mmoja na Ally Makunguru, Rahma Shally na hivyo kujiunga na Joseph Mulenga , Makuka, Matei Joseph na wengineo. Lister pia ni mtunzi wa vitabu na mwanamuziki ambae amesoma vizuri muziki kwa sasa yuko Japan habari zake za sasa zinapatikana kwenye website yake http://www.listerelia.com/

(Pichani Sambulumaa katika picha kabla tu ya uzinduzi wa bendi hiyo, picha ya pili Lista akiwa OSS)

Sunday, August 1, 2010

Harison Siwale-Satchmo


Kwa mara ya kwanza niliwaona 'Live', Jamhuri Jazz Band wakipiga katika ukumbi wa Community Centre Iringa, ukumbi maarufu kwa wenyeji wakati huo kwa jina la Olofea senta (Welfare Centre). Ni vigumu kuelezea jinsi nilivyokuwa najisikia kwani nilikuwa sidhani kama kutakuja kuweko na wanamuziki wanapiga vizuri namna ile. Lakini katika wote mpiga rythm guitar Harison Siwale, aliyejulikana kwa jina la Satchmo, alikuwa na anabakia kuwa mpiga gitaa aliyenifurahisha kuliko wote. Kwanza alikuwa na staili ya peke yake, na mpaka leo nikisikiliza nyimbo zake kama vile Blandina, Mganga no 1, Maria bembeleza mwana au Ewe ndege, nabaki kusifia kuwa huyu bwana alikuwa na kipaji cha pekee. Kuna rafiki yangu aliwahi kumuuliza wakati ule huwa anapataje mawazo ya kupiga gitaa lake kwa staili ile? alijibu kuwa huwa anajaribu kupiga sauti za viumbe mbalimbali wa porini katika gitaa lake.
Wanamuziki waliokuwa katika bendi ya Mkwawa High School, watakumbuka jinsi walivyoweza kupata nafasi ya kupiga pamoja na bendi hii kila ilipokuja Iringa mjini, maana hizo ndiyo zilikuwa taratibu wakati huo. Bendi ikifika katika mji, kama mji ule una bendi basi nao watapata nafasi ya kushirikiana na wageni. Wakati huo Mkwawa ilikuwa na wanamuziki kama vile Sewando, Manji, Mpumilwa,Kakobe waliweza pia kubadili hata muziki wao kutokana na kupiga na bendi hizi zilizokuwa kubwa wakati huo. (Pichani toka kushoto- Harison Siwale, Mbaraka Mwinyshehe na Abdul Mketema)

Kuzaliwa kwa Bana OK


Baada ya kifo cha Franco, Lutumba Simaro ndie alie liongoza kundi zima la TPOK Jazz kwa miaka minne. Ilionekana kuwa ili warithi wa Franco waendelee kufaidi matunda ya kundi hilo, wazo lilitolewa kuwa Simaro abakie na wanamuziki wote na familia iendeshe utawala mwingine wote, na warithi wawe wanapata asilimia 40 ya mapato yote, ambapo dada yake Franco ambaye ndiye alikuwa kiongozi wa familia angeyasimamia shughuli hizo. Dada wa Franco, baada ya kushauriana na nduguze aliamua kuwa familia ipewe asilimia 30,na isijihusishe kabisa na mambo ya bendi. Baada ya makubaliano haya bendi ilianza kazi na safari yake ya nje ya kwanza ilikuwa Tanzania na Kenya. Hali ilikuwa ngumu baada ya kifo cha Franco, lakini mambo polepole yalianza kuwa mazuri. Ghafla magazeti yakaanza kuwa na barua za wasomaji zikimlaani Simaro kuwa anaendesha bendi kama mali yake peke yake na kutokutoa msaada wa maana kwa watoto wa Franco. Hatimae akaandikiwa barua rasmi kuwa arudishe vyombo vyote vya muziki nyumbani kwa Franco.Hiyo ilikuwa mwishoni mwa mwaka 1993. Wakati huo huo mwanasheria wa familia ya Luambo alienda kwenye TV na kutangaza kuwa Simaro si kiongozi tena wa bendi.

Ilikuwa ni pigo kwa Simaro ambaye alijiunga na OK Jazz tangu 1961, na kupitia kwake wanamuziki kama Femi Joss, Kwammy, Isaac Musekiwa, Defao, Albino Colombo waliweza kuwika katika OK Jazz, na wote walikuwa wameondoka akabaki mwenyewe na sasa alikuwa akifukuzwa kupitia TV.

Katika onyesho lake la mwisho aliwaomba watu wa TV ya RTNC kuhudhuria,na kwa kutumia nafasi hiyo nae akatangaza kuwa yeye si mwanamuziki wa TP OK Jazz tena, ilikuwa ni tangazo la kusikitisha lililoleta simanzi kwa wengi. Na ndio ukawa mwanzo wa Bana OK, wanamuziki walikutana walikutana katika ukumbi wa Bar ya Zenith na kuamua kuanzisha bendi chini ya Rais wa Lutumba Simaro. Ilikuwa tarehe 4 January 1994. (Habari na picha kutoka www.afropop.org kwa ruksa ya Banning Eyre)

Upinzani...........

Leo hii kuna neno maarufu limetokana kwa wasanii wa Kimarikani-BIF. Si kwamba ni utamaduni mgeni, ila utekelezaji wake ndo umekuwa tofauti siku hizi, na kwetu hapa kumekuweko na utamaduni wa ushindani ambao kwa kuchochewa mara nyingine na vyombo vya habari ukageuka upinzani. Katika kipindi fulani cha miaka ya sitini muziki wa jiji la Dar katika nyanja ya Band za rumba ulitawaliwa na bendi mbili, Dar es Salaam Jazz- Majini wa Bahari na mtindo wao wa Mundo, na upande wa pili Kilwa Jazz. Ulikuwa mpambano mkali uliofikia hata wapenzi wa bendi hizi mbili kutandikana makonde. Bendi zilitungiana nyimbo za mafumbo moja maarufu ulikuwa ule wimbo wa Dar Es Salaam Jazz Mali ya mwenzio siyo mali yako, ukiwadhihaki kilwa Jazz kutokana na eneo la Klabu yao kuwa na utata wa kodi. Morogoro kulikuwa na miamba wawili, Morogoro Jazz na Cuban Marimba, ushindani wao uliweza kuwasha moto wa upenzi Afrika ya Mashariki nzima, watu walikuwa wanajitahidi kuwepo Morogoro siku za wikiendi, Morogoro Jazz wakiwa na mtindo wao wa Sululu, Cuban Marimba na mtindo wa Ambianse. Nao pia walitunga nyimbo zenye vijembe nyingi zilizowatia kiwewe wapenzi wao, Cuban walikuja na mtindo wao Subisubi, wakijisifu kuwa wao ni Jini Subiani linanyonya. Tanga kulikuwepo na vijana wa Barabara ya 4 Atomic Jazz wana Kiweke , wakipambana na Jamhuri Jazz Band na mitindo yao mingi kama vile Dondola na Toyota. Ushindani huu uliendelea katika bendi mbalimbali, kama vile Juwata na Sikinde. Kuna ushindani mwingine ulikuwa zaidi wa kufikirika kama ilivyokuwa inadhaniwa na wengi kati ya Vijana Jazz na Washirika Stars, kiasi cha kwamba kuna wakati ule wimbo wa Nimekusamehe lakini sintokusahau ulitafsiriwa kuwa ulikuwa umetungwa na Hamza Kalala kwa ajili ya kumtaarifu Hemed Maneti, japokuwa si Maneti wala Hamza ambae niliongea nae kuhusu wimbo huo karibuni aliyesema kuwa aliutunga kwa ajili hiyo. Kwa wapenzi wa muziki enzi za uhai wa Maquis Du Zaire, na Orchestra Safari Sound wanakumbuka ushindani mkubwa ulio kuwepo kati ya hizi bendi mbili ambazo kuna wakati huo zote zilikuwa zikiwa na makao makuu jirani, Maquis wakiwa Ubungo na OSS Kimara. Maquis walipoasisi mtindo wao wa Ogelea piga mbizi, OSS wakaja na Chunusi, wakiwa na maana ukiogelea kiboko yako Chunusi. Katika mtiririko wote huu wa ushindani mara chache sana ulifikia wanamuziki binafsi wakashikana mashati kwa sababu za ushindani. Na ushindani ulikuwa wa maana kwa kuwa kweli bendi zilipiga muziki tofauti, Jamhuri na Atomic zote za Tanga lakini kila moja ilikuwa na muziki tofauti, na vivyo hivyo Moro Jazz na Cubano, au Tabora Jazz na Nyanyembe Jazz. Kila Jumanne asubuhi, Radio Tanzania ilikuwa na kipindi kilichorusha nyimbo zilizorekodiwa katika studio yake, Misakato. Ilikuwa si ajabu kukuta wanamuziki wa bendi yenye ushindani ukisikiliza nyimbo mpya za washindani wao. Na hata kutoa sifa pale ambapo zinastahili, na kutokea hapo watu wanajipanga kutengeza kazi bora kuliko hiyo. Nakumbuka Tancut Almasi ilikuwa Morogoro wakati Vijana Jazz wakirushwa nyimbo zao za Ngapulila, Adza kwa mara ya kwanza katika kipindi cha misakato, ilikuwa uhimu kusikiliza kazi yao kwani wakati huo Shaaban Wanted ndio alikuwa kahama Tancut na kujiunga na Vijana, na mfumo wa vyombo wa Vijana ulikuwa sawa na Tancut na Washirika pia yaani Solo gitaa, Rythm Gitaa, Second solo, Keyboards, bass, na vyombo vya upulizaji. Hii haikuleta upinzani bali iliongeza ushindani, hapo tulikaa chini na hata kurekibisha baadhi ya nyimbo tulizoziona ziko chini ya kiwango cha vijana, matokeo yake ndio ile album, yenye nyimbo kama Helena Mtoto wa Arusha, Masikitiko na kadhalika

Saturday, July 31, 2010

Mbaraka Mwinyshehe Mwaluka 1



Ukikaa na kusikiliza muziki wa Mbaraka kwa makini unajifunza mengi sana, kwa mashahiri ya nyimbo hizo unapata picha ya maisha yalikuwaje enzi hizo. Furaha, machungu, vicheko, vilio na kadhalika. Upigaji wake wa gitaa, ni somo zuri sana kwa mpigaji anaetaka kujiendeleza katika upigaji wa solo. Katika vipindi vyake vya kuanzia Morogoro Jazz hadi Super Volcano alipitia staili nyingi za muziki, baadhi kama Sululu, Likembe, Masika Zolezole na kadhalika. Tofauti na bendi nyingi ambazo hubadili majina ya mitindo bila kubadili muziki wenyewe, staili za Mbaraka zilionyesha mabadiliko. Nyimbo katika staili ya Likembe zilikuwa tofauti na zile za Masika Zolezole. Kipindi hicho wapenzi wa muziki waliweza kuondoka Dar es Salaam na kwenda Morogoro kufaidi wiki endi ya muziki aidha wa Cuban Marimba, au Morogoro Jazz. Picha ya juu Mbaraka Mwinyshehe, ya chini toka kushoto Sulpis Bonzo, Mlinzi Mustafa(huyu baadae alipigia Urafiki Jazz), Shaaban Nyamwela, Abdul Mketema (mwenye Saxaphone),Samson Gumbo,Mbaraka Mwinyshehe.Hapa wakiwa Morogoro Jazz Band

Friday, July 30, 2010

Mwanamuziki Mheshimiwa Paul Kimiti


Kwa muda mrefu nilikuwa na nia ya kuweka taarifa kuhusu wimbo wa kumsifu Nyerere ambao uliimbwa na Mheshmiwa Paul Kimiti. Nilijitahidi kutaka kupata taarifa kutoka kwake ikawa haikuwezekana lakini karibuni nilisoma maelezo ya Mheshmiwa mwenyewe kuhusu kazi hiyo, ambayo alisema walifanya akiwa Mwenyekiti wa wanafunzi kutoka Tanganyika katika chuo kikuu cha Netherlands kati ya mwaka 1962 na 1965. Akiwa na wanamuziki wenzake wakiwa na kundi waliloliita Safari Brothers walirekodi nyimbo hii nzuri sana kuhusu Mwalimu Nyerere. Mheshimiwa alisema walitoa dola 20,000 walizozipata kutoka Philips records kwa Mwalimu alipotembelea Netherlands April 1965, pesa hizo walitoa ili kuchangia maendeleo ya nchi yetu, na huo ndio ulikuwa mwanzao wa uhusiano wake na Mwalimu.

Wednesday, July 28, 2010

Kida Waziri arudi ulingoni

Kida waziri miaka ya 90.

Kida Waziri au kama alivyokuwa akiitwa enzi zake Vijana Jazz Stone Lady amerudi na album yake yenye nyimbo 6 ikiwa na nyimbo kama Wifi zangu, Shingo Feni, Penzi haligawanyiki na nyinginezo, pia ameimba wimbo wa Mary Maria akishirikiana na mwanae Waziri, ambae kajitahidi kuimba zile sehemu za uimbaji wa marehemu babake.

Kida Waziri alivyo sasa.

Sunday, July 18, 2010

Drums

Ukisema drums katika anga za muziki utakuwa umeeleweka kuwa unaongelea zile ngoma za kizungu ambazo hupigwa kwa kutumia miguu na mikono. Uwingi wa drums huanzia ngoma kubwa moja na ndogo moja (snare), na tasa moja (Hi hat), na kuendelea kwa uwingi kadri ya utajiri na uwezo wa mpiga drum. Katika nyimbo za Dar es Salaam Jazz ambazo zilirekodiwa kwenye miaka ya 30, drums zilitumika hivyo si chombo kigeni katika muziki wa Tanzania. Katika miaka ya sitin chombo hiki kilitoweka katika bendi nyingi za muziki wa rumba, lakini kikarudi tena kwa nguvu baada ya kuingia kwa staili ya kavacha kutoka Kongo. Bendi ambazo zilikuwa zikipiga muziki wenye mahadhi ya kimagharibi ziliendelea na drums katika kipindi chote na kuweza kuunganisha na tungo za zao za rumba kwa ufanisi mkubwa kama ilivyotokea kwa bendi kama Afro70. Drum huwa chombo kinacholinda spidi ya wimbo, na staili ya wimbo, kama ni chacha, tango, waltz au ngoma ya Kimakonde au Kipogoro. Drums huweza kuleta utamu sana kama zikimpata mpigaji.
Siku hizi kuna drums za umeme, hizi huwa na uwezo wa kuongeza au kupunguza sauti, na kuzibadili zikalia milio mbalimbali, kwa mfano kulia kama ngoma za kihindi au kulia kama tumba au hata nyingine zinaweza zikipigwa zikawa zinatoa milio ya ndege!!!.Bendi ya kwanza kuwa na electronic drums ilikuwa Chezimba, wakati huo drums zikipigwa na Charles Mhuto, Tanzanite nao wakanunua zao, na kwa upande wa bendi za rumba MK Group, ikifuatiwa na Vijana Jazz na Bima Lee walikuwa wa mwanzo kuwa na drums hizi

Friday, July 16, 2010

Gitaa la rythm




Katika mfumo wa awali bendi zilikuwa zikitumia magitaa matatu, Solo, rythm na Bass. Gitaa la solo lilikuwa na sauti ya juu huku rythm ikiwa na sauti nzito kidogo ya kati, na mwisho Bass likiwa na sauti nzito kuliko magitaa mengine. Kimuundo gitaa la rythm na la solo hakuna tofauti. Yote yana nyuzi 6,lakini katika kutyuni kwenye amplifier, gitaa la rythm hunyimwa treble kiasi na kuongeza bass zaidi kuliko gitaa la solo ambalo huwa na treble zaidi ya magitaa mengine. Inasemekana kaka yake Dr Nico, ndie aliyeanzisha mtindo wa kuongeza gitaa la nne lililoitwa second solo. Hili lilikuwa likipigwa kwa mifumo mbalimbali katika bendi mbali mbali. Bendi nyingine zilitumia second solo kama gitaa lililokuwa linajibizana na solo, na bendi nyingine lilikuwa linajibizana na rythm. Bendi ya Cuban Marimba chini ya Juma Kilaza liliongeza ubunifu na kuongeza gitaa la 5 na kuliita chord guitar. Lakini leo tuzungumzie gitaa la rythm. Chombo hiki bado kinapigwa katika bendi nyingi lakini umaaarufu wake umeshuka sana. Katika kipindi cha miaka ya 60 na 70, gitaa hili lilikuwa na umuhimu mkubwa na wapigaji wake waliweza kubuni staili zao wenyewe. Kati ya wapiga rythm maarufu namkumbuka Satchmo, hilo ndio lilikuwa jina la kisanii la Harrison Siwale mpiga rythm wa Jamhuri Jazz. Yeye alikuwa na staili peke yake ya kupiga rythm, sikumbuki kusikia mtu mwingine akipiga rythm ya aina yake kabla ya hapo. Rythm yake ilitawala nyimbo za Jamhuri wakati huo. Kumbuka wimbo kama Mganga no 1 na 2, au Blandina. Marehemu Mzee Kasim Kaluwona nae alikuwa na staili tofauti ya upigaji uliyoifanya Tabora Jazz kuwa na staili yake peke yake, kumbuka gitaa lake katika wimbo Asha, au Dada Lemmy. Charles Kazembe akiwa na Morogoro Jazz anakumbukwa katika upigaji wa rythm kwenye nyimbo kama Wajomba Wamechacha. Hao ni wachache tu kulikoweko na wengi marufu. Katika kipindi hiki huko Zaire kulikuwa na mipigo mbalimbali ya gitaa la rythm, ila kitu kipya kikaanzishwa ambapo katika ufungaji wa nyuzi ,wapiga rythm wakauondoa uzi namba nne na kuweka uzi namba moja, hivyo kukawa na nyuzi namba moja 2 katika gitaa, hapo ndipo akina Vata Mombasa wakaweza kuleta utamu mpya katika upigaji wa rythm. Wakati huo Orchestra Kiam wakawa wanajivunia kupiga rythm kwa spidi kali sana,vibao kama Kamiki, Bomoto ni ushahidi wa kazi hizo. Utamu wa ufungaji wa nyuzi kwa staili hii uliweza kusikika vizuri katika gitaa lililopigwa mwanzo kabisa wa wimbo Andoya. Leo vionjo vya upigaji huo vinarudi kwa njia ya ajabu sana. Vikundi vya taarab vimeanza 'kuachia rythm' gitaa moja kubaki linapiga peke yake, japo wao hupiga gitaa la solo lakini staili ni ile ya enzi. Siku hizi kelele huwa nyingi kiasi unaweza ukatembelea bendi 3 ukaona mtu anapiga gitaa la rythm lakini husikii anapiga nini.

Thursday, July 15, 2010

Uliwafahamu Hot 5 wa Magomeni Kota?

Kuna swali nimeulizwa sina jibu,na kila ninae muuliza hana kumbukumbu nalo. Nimeulizwa kama nilikuwa nalifahamu kundi lililoitwa Hot 5 ambalo masikani yake yalikuwa Magomeni Kota, kundi hili lilikuwepo kabla ya Flaming Stars kuhamia Mombasa.....kuna mwenye taarifa?

Atomic Jazz Band


Atomic ilikuwa moja kati ya bendi zilizowika sana nchi hii. Bendi iliyokuwa na makazi yake Tanga, Tanga wakati huo ikiwa na vikundi vingi maarufu vya muziki, kama vile Jamhuri, White Star, Amboni, Lucky Star, Black Star. Bass katika bendi hii kwa kweli lilikuwa likiingiza upigaji wa bezi katika kiwango kipya,wapigaji wake walileta changamoto hata walipokuja hamia katika bendi mpya. Pichani toka kushoto John Mbula -Saxophone,Rodgers- mwimbaji, John Kilua-Thumba(huyu alikuwa ni ndugu ya Julius Kiluwa ambaye ndiye alikuwa mwenye bendi),John Kijiko-Solo gitaa, Hemed Mganga-rythm gitaa (niliwahi kupiga bedni moja na mzee Mganga kwa wakati fulani. Tulikuwa wote Orchestra Makassy na ndie baba mzazi wa mwimbaji wa kizazi kipya Kassim Mganga),Mohamed Mzee-Bass.
Picha hii ilikuwa ni jarada la santuri iliyokuwa na wimbo maarufu Mado Mpenzi Wangu. Wimbo ulikuwa ni ujumbe wa kweli kutoka kwa mwanamuziki mmoja kwenda kwa mpenzi wake ambae jina kidogo linafanana na Mado ili kuficha ukweli. Mtunzi wa wimbo huu alikuwa mpenzi sana wa bendi hii na bado kwa rafiki zake anajulikana kwa jina la Mado. Siku hizi amekuwa mpenzi tu wa kawaida wa muziki.

Lutumba Simaro wa Ok Jazz


BANNING EYRE ni mwandishi Mmarekani aliyefanya mazungumzo na mwanamuziki Lutumba Simaro mpiga gitaa wa kundi la OK Jazz, kuna mengi ya kujifunza kwa wanamuziki wa Tanzania
SWALI: Nini kinaendelea katika muziki wa Kongo siku hizi?
SIMARO: Kinachoendelea sasa sikipingi, mi ndio baba yao, hawa vijana kuna kitu walichoingiza katika muziki. Wameleta damu mpya na ujana kweli lakini,kuna monotony mno, Huwezi kutofautisha bendi moja na nyingine. Wanavyoimba, wanavyocheza na wanavyopiga mgitaa katika kile wanachoita seben. Kuna mtangazaji mmoja anaitwa Gaspar wa Studio Maximum, ana kipindi kimoja ambapo nilikuwa nasikia wimbo wa Werrason lakini alikuwa JB anecheza na wimbo wa JB ukichezwa show na Werra, kwa kweli huwezi kuona tofauti ya muziki wa hawa wawili.
Enzi za OK Jazz, Franco alikuwa mtunzi mzuri sana, mimi nikajiunga nikaleta style yangu, Josky alipokuja nae akaleta staili yake. Ndombe nae pia akaja na staili yake. Wote tulikuwa OK Jazz, gitaa la Franco ndilo lilitawala na kuweka nembo ya staili zetu mbalimbali. Papa Wemba akiimba najua ni Papa Wemba ana staili yake. Mdogo wangu Kofi nae anastaili yake, Zaiko ya Nyoka Longo pia wana staili yao
Kama wangeweza kunisikiliza ningewaambia hivi hawa vijana wanajitoa Wenge na kuanzisha makundi yao, ni muhimu kuja na utofauti, wana waimbaji wazuri sana, watunzi wazuri na wamepata bahati kuweza kurekodi katika studio za kisasa wana jukumu la kuendeleza ubunifu. Wakati wetu wa enzi za Vicky Longomba, Mujos na Kabasele, kama we ni mwimbaji ulilazimika kuimba aina mbalimbali za muziki. Muziki wa Ulaya au Marekan na kwa staili mbalimbali. Mtu akiomba Tango, unapiga Tango , ukitakiwa kuimba Waltz uliimba style hiyo, lakini waimbaji wetu wa sasa, hakuna kitu. Na wapiga magitaa pia, tulikuwa na wapiga magitaa wakali kama Papa Noel, na Tino Baroza, na hata Franco. Wapiga magitaa siku hizi ukiwauliza unamfahamu Nico Kasanda? Tuno Baroza? Kimya kinatawala. Muhimu kujua staili zao ili kujitafutia stail mpya. Nina mpiga gitaa ana miaka 20, wiki iliyopita nilimpa sanduku zima la santuri akafanye mazoezi, nashukuru ameanza kuniuliza maswali mengi kuhusu upigaji mbalimbali. Utunzi nao unapwaya pia utakuta wimbo unataja majina ya watu 200, wanaita “mabanga”, nawauliza majina mengi ya nini wananiambia hawa huwa wanawalipa vizuri.
Vijana wana bahati wana teknolojia nzuri, wana TV nyingi na nzuri za kuweza kuwafanyia promotion, Wakati wetu tulikuwa na radio moja tu, hivyo ililazimu kufanya kazi nzuri ili ujulikane. Nawakumbuka Soki Dianzenza na Soki Vangu walikuja na kitu kipya, Nyboma, Pepe Kalle wote watakumbukwa kwa aina yao ya uimbaji.
Nimeitafsiri kwa ruksa ya Banning Eyre. Kwa habari nyingi zaidi angalia www.afropop.org

SAFARI ZANGU NA BENDI sehemu ya kwanza.

  TANCUT ALMASI ORCHESTRA  wakiwa Jamhuri Stadium Dodoma   Sikumbuki ni safari ngapi za kimuziki nilizowahi kuzifanya hapa nchini katika m...